Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Diamond, Harmonize wateka mkesha wa mwaka mpya

Video Archive
Thu, 2 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma/Dar. Wakati kila mmoja akiuaga mwaka 2019 kwa staili yake, wasanii nyota nchini, macho ya wengi yalielekezwa kwa Diamond Platnumz na Harmonize ambao walikuwa pembe mbili za nchi-- kusini na magharibi.

Nyota hao wawili walikuwa vinara wa kampuni ya Wasafi, lakini Harmonise aliamua kujitenga mwaka huu kuanza kufanya kazi peke yake na macho ya mashabiki wa muziki Tanzania, sasa yanawaangalia wawili hao kwa jicho la kupambanisha.

Platnumz, nyota wa kikao kilichotamba Afrika cha “Number One” na alikwenda Kigoma kwa treni maalum iliyojaa wasanii, alikuwa na lengo la kuadhimisha miaka 10 tangu aanze muziki na kuwashukuru mashabiki wake wa mkoa huo walioingia bila ya kulipia kiingilio.

Harmonize naye alienda Tandahimba mkoani Mtwara kwa staili yake. Alikuwa usafiri wa helkopta na alisalimia na kutoa shukurani Wilaya ya Masasi, Newala na mjini Mtwara.

Na usiku wa kuamkia jana, kazi ilikuwa kwa mashabiki kuhamahama kutoka chaneli moja iliyokuwa na matangazo ya moja kwa moja kutoka Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma ambako Diamond alikuwa akitumbuiza na Uwanja wa Majaliwa mjini Tandahimba ambako Harmonise pia alikusanya mashabiki wake kuukaribisha mwaka mpya.

Mazingira yalikuwa ya kuvutia kwenye Uwanja wa Lake Victoria, ambako nyuma ya jukwaa ilikuwa ni mithili ya ukuta ulionakshiwa kwa marumaru na wenye ngazi.

Diamond, ambaye jina lake halisi ni Naseeb Abdul, alipanda jukwaani saa 6:00 kamili baada ya mwaka 2020 kuingia, lakini kwa staili ya aina yake. Lilitangulia kundi la madansa ambao wote walivalia nguo za rangi nyekundu--juu na chini.

Madansa hao wapatao 30 walicheza kwa dakika chache kabla ya muziki kuzimwa na saa kuanza kuhesabu sekunde zilizosalia hadi ilipofika saa 6:00 kamili.

Muda huo ndipo taa jukwaani zilipowashwa na Diamond akaonekana amesimama mbele ya madansa hao na kusababisha mashabiki kuanza kupiga kelele wakisema “simba, Simba, simba” kumaanisha jina ambalo msanii huyo amejipachika.

Alidansi vipande viwili vya nyimbo zake kabla ya kuimba wimbo wa “Baba Lao” ambao unamtaja Rais John Magufuli kuwa ni ‘baba lao’ waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Utamaduni, Harrison Mwakyembe pamoja na yeye Diamond kuwa ni ‘babalao’.

Huku akishangiliwa na baadhi ya mashabiki kutaka aendele kuimba, Diamond alisimamisha muziki na kueleza sababu za kwenda Kigoma kufanya onyesho hilo kuwa ni kurudi nyumbani kwao baada ya kufikisha miaka 10 katika muziki, ili kushukuru mashabiki.

“Kuna waliotaka kujua watalipia shilingi ngapi, lakini nimeamua nisichukue fedha yoyote kutoka kwenu,” alisema Diamond akiwa ameegemea moja ya spika.

“Badala yake, ile fedha uliyoweka ya kiingilio, katoe sadaka. Uwe Mkristo au Muislamu, nenda katoe sadaka umshukuru Mungu. Na hata kama ndugu ako amefariki. watoe sadaka kuwaombea Mungu awasaidie huko waliko.”

Magufuli ‘ndani ya” ya shoo

Wakati Diamodnakiendelea kutumbuiza, Rais John Magufuli alimpigia simu saa 7:54 usiku na kusema Diamond ni mwanaume apige kazi.

Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ndiye aliyepokea simu hiyo na kuipeleka jukwaani na kuwaambia mashabiki kuwa wana bahati kwa kuwa aliyepiga ni Rais.

“Piga shangweee …..Mheshimiwa shikamooo,” alisema Diamond kabla ya kuweka simu katika kipaza sauti.

“Nakutakiwa wewe heri ya mwaka mpya pamoja na na wanakigoma wote huko,” alisikika Rais akisema huku mashabiki wakipiga kelele za wakisema “babu! babu! babu”.

“Rais amesema alitamani na yeye angekuwepo hapo, lakini amemtuma Polepole na wengine waliokuja hapo,” alisema Diamond huku akimwambia Rais akisema “baba watu tunakupenda sana na tunakuhakikishia awamu inayokuja unapita kwa kishindo sana. Tunapiga mia kwa mia, Magufuli oyeeee!CCM oyeee”.

Na Rais akasema: ”Ninawahakikishia wanakigoma hiyo barabara kutoka Kigoma kwenda Nyakanazi yenye zaidi ya kilometa 300 lazima ikamilike kwa lami, lakini nawapongeza sana wanakigoma.”

Harmonise aingia kimtindo

Mjini Tandahimba hali pia ilikuwa ya aina yake. Harmonize alishuka akiwa anaelea hewani akitumia Crane ya kushushia mizigo.

Mkononi akiwa ameshikilia kinasa sauti, Harmonize alipanda jukwaani akipita juu ya mashabiki uwanjani hapo ambao walilazimika kunyanyua vichwa kumtazama huku wakimshangilia kwa nguvu na kupunga mikono hewani.

Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Harmonize kujaza mashabiki akiwa nje ya WBC. Awali ilikuwa ni katika shoo yake ya “Twendenzetu Tukaijaze Tandahimba” alipokuwa chini ya WBC.

Mama, Baba Harmonize wakutana

Wakati Harmonize kuamua anampandisha jukwaani mama yake mzazi aliyeimba wimbo wa “Atarudi” akiwa amevaa gauni la dash dash la rangi ya pinki na kiremba cha rangi ya dhahabu, baba yake mzee Kahali alikuwa jukwaani akishuhudia namna kijana wake anavyotoa burudani.

Wazazi wa nyota huyo waliachana siku nyingi, lakini wamekutanishwa katika uwanja huo na kijana wao na kuzungumza lugha moja.

Nyota huyo wa “Uno” aliimba baadhi ya nyimbo zake maarufu, akiwa jukwaani na kwenye crane.

Chanzo: mwananchi.co.tz