Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: ‘Bata’ ilivyofupisha safari ya Diamond kufika Kigoma

Video Archive
Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Safari iliyochukua saa 32 kutoka Dar es Salaam hadi mkoani Kigoma iliyofanywa na msanii Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ na mashabiki zake ilionekana fupi kwa abiria kutokana na matukio burudani au kula bata yaliyofanyika.

Katika safari hiyo iliyokuwa na mabehewa 14, Diamond alilipia mabehewa manane kwa ajili ya mashabiki zake aliosafiri nao kwenda mkoani Kigoma kumuunga mkono katika tamasha la kuadhimisha miaka 10 tangu alipoanza muziki linalofanyika leo.

Kati ya mabehewa hayo, moja lilitumika kama klabu ambako mashabiki walicheza muziki usiku kucha hadi saa 2:30 asubuhi. Behewa hilo lilitolewa viti na kupambwa kama ukumbi wa muziki na kuwekwa spika kubwa ambazo pia Diamond alizitumia kuwaimbia mashabiki katika baadhi ya stesheni.

Usiku wa safari hiyo zilipigwa nyimbo mbalimbali na maDJ, huku Diamond na aliyekuwa meneja wake, Bob Junior wakikumbushia albamu yake ya kwanza ya ‘Nenda kamwambie’ iliyomtambulisha kwenye soko la muziki.

Pia kulikuwemo na ngoma ya ‘kibao kata’ ambayo msanii huyo anaonekana kuipenda kutokana na kuitumia katika shughuli mbalimbali za kifamilia. Kuna wakati alijumuika na wapiga ngoma hao kwa kupiga manyanga.

Kama si hekima za DJ kuzima muziki saa mbili asubuhi ili watu wakaoge na kujiandaa kwa chai, huenda muziki huo ungeendelea hadi saa sita mchana.

Ilikuwa safari ya kula, kunywa

Abiria wote waliokuwamo katika mabehewa hayo manane walikula na kunywa kuanzia asubuhi, mchana na usiku yaani unaweza kusema ilikuwa bata mwanzo mwisho.

Huduma iliyotolewa haikuwa tofauti na zile zinazotolewa kwenye sherehe zenye hadhi ya ‘bufee’, kwani kulikuwa na vyakula vya aina mbalimbali.

Asubuhi ya siku ya pili, abiria walipata supu na vitafunwa mbalimbali. Kwa vinywaji kulikuwa na soda na vileo tofauti.

Katika safari hiyo iliyoanza Desemba 28, saa 2 asubuhi, treni ilifuata utaratibu wa kawaida wa kushusha na kuwapandisha abiria, fursa ambayo Diamond aliitumia kusalimiana na mashabiki zake waliokuwa wakimsubiri.

Katika stesheni 13 iliposimama treni hiyo kutoka Dar hadi Kigoma, stesheni za Nguruka na Uvinza zilitia fora kwa mapokezi. Katika stesheni nyingine, Diamond alikuwa akisalimia mashabiki kupitia dirishani na wakati mwingine kutumia spika, lakini kwa stesheni za Nguruka na Uvinza walimuandalia jukwaa la kuimba.

Hali hiyo ilimlazimu msanii huyo kushuka kwenye treni na kutumbuiza kwa nusu saa kabla ya kuendelea na safari.

Pia katika stesheni hizo, watu wengi walijitokeza kumlaki, mpaka polisi na walinzi wa Diamond walionekana kuzidiwa nguvu wakati wakiwadhibiti mashabiki.

Stesheni ya Nguruka ambayo inasifika vibaya kwa kuwa na matukio ya wizi wa madirishani, siku hiyo matukio hayo hayakuwapo, hali iliyowashangaza baadhi ya abiria.

Hali ilivyokuwa Kigoma

Wakati treni ilipokaribia kufika stesheni ya Kigoma walionekana watu wengi wakiwa wamesimama pembezoni mwa treni na ilipofika karibu walianza kuikimbiza, huku wakiimba ‘Simba, Simba, Diamond Baba Lao”.

Pia nje ya stesheni hiyo kulikuwa na bango la Umoja wa wakulima wa michikichi lililoandikwa ‘Karibu nyumbani Diamond Platnumz’.

Baada ya kuwasili Diamond alipokolewa na mama yake mzazi, Sanura Kassim maarufu kama Bi Sandra na baba yake wa kufikia, Uncle Shamte ambao walikuwapo Kigoma kwa zaidi ya wiki kwa ajili ya maandalizi.

Muda mfupi baadaye walijitokeza watu waliofahamika kama machifu na kumvalisha nguo za asili za ngozi zenye rangi ya kahawia.

Baada ya hapo Diamond alipanda ghorofani katika stesheni hiyo na kuwasalimia wananchi waliokuwa wamefurika kumpokea.

Pia aliwapa nafasi wasanii Linex na Baba Levo kuwasalimia mashabiki, hali iliyoamsha shangwe zaidi hasa pale walipoimba wimbo wa ‘Leka Dutigite’ unaosifia uzuri wa mkoa wa Kigoma ambao ulishirikisha wasanii mbalimbali wanaotokea mkoa huo.

Mashabiki na Polisi

Baada ya kuwasili Kigoma ilipangwa Diamond azunguke maeneo mbalimbali kuwasalimia mashabiki, lakini alishindwa kutokana na umati mkubwa wa watu, huku askari wakiwa wachache.

Askari waliokuwapo walilazimika kutumia nguvu za ziada kuwatawanya wananchi, ili wapate njia ya kupita kumsindikiza msanii huyo hotelini.

Baada ya kupatikana njia, mashabiki hao waliufuata msafara huo hadi hotelini na kukaa hapo hadi usiku, huku wakimtaka Diamond atoke ili awaimbie.

Chanzo: mwananchi.co.tz