Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO:Baada ya kushindwa BSS mara tatu, Meshack aibuka mshindi 2019

Video Archive
Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hatimaye fainali za mashindano ya Bongo Star Search (BSS) nchini Tanzania, msimu wa kumi yamefika ukingoni huku Meshack Fukuta kutoka mkoani Mbeya akiibuka mshindi.

Fainali za BSS zilifanyika usiku wa kuamkia leo Jumatano Desemba 25, 2019 katika ukumbi wa Next Door Arena, Masaki Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo viongozi serikalini na wasanii maarufu.

Kwa upande wa viongozi wa Serikali alikuwapo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Juliana Shonza ambaye alikuwa mgeni rasmi na Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Onesmo Kayanda.

Fainali hizo ambazo huu ni  msimu wa kumi kufanyika, zilianza saa 4:00 usiku kwa washiriki walioingia tano bora kuonyesha uwezo wao wa kuimba jukwaani na zilifika tamati saa 7:06 usiku kwa Meshack kutangazwa kuwa mshindi.

> Washiriki hao waliochuana na Meshack ni Leonard Sunday, Patricia Zephania, Frank Charles, Patrick Alsina.

Meshack  ambaye ni mshiriki kutoka Mbeya, kutokana na ushindi huo amejitwalia Sh50 milioni ambazo ni zawadi kwa mshindi wa mwaka 2019 huku mshindi wa pili akiwa ni Leonard Sunday na mshindi wa tatu akiwa ni Frank Charles walioondoka na televisheni.

Kama vile haitoshi ukiachilia mbali fedha, amepata ofa ya kusimamiwa muziki wake kwa mwaka mzima ambapo pia atakuwa na meneja.

Akizungumzia ushindi huo, Meshack amesema, "haikuwa kazi rahisi kufika hapa kwani mchuano ulikuwa mkali na sio kwamba mimi ndio nilikuwa naimba kuliko wote,".

 

Amesema mpaka anapanda jukwaani hajaamini, ukizingatia kwa siku tatu mfululizo alikuwa anaumwa malaria na alikuwa kwenye sindano za saa.

Msanii huyo amebainisha hii sio mara yake ya kwanza kushiriki mashindano hayo, kwani alishashiriki mwaka 2014 hakufanikiwa kupenya hata ngazi ya mkoa.

"Sikukata tamaa mwaka jana tena nikashiriki nikafanikiwa kuingia kwenye 20 bora walioenda Dar es Salaam lakini nikatolewa kipindi cha kwanza, hivyo nashukuru mwaka huu umekuwa wangu nimeshinda," amesema Meshack.

Kupitia ushindi huo, ameeleza alichojifunza ni kutokukata tamaa na kumuomba Mungu kwa kila jaribu linalokukuta kwa kuwa kuumwa kwake alijua tayari kazikosa fainali za mashindano hayo.

Baadhi ya wasanii waliohudhuria fainali hizo ni pamoja na Dogo Janja, Linah Sanga, Rachel Kizunguzungu.

Wengine ni Angel Bernard, Kala Jerimiah, Kayumba na Ruby ambao pia  walitumbuiza usiku huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz