Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uzinduzi wa filamu na tija katika kukuza tasnia

18650 Pic+filamu TanzaniaWeb

Sat, 22 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Soko la filamu Bongo limeendelea kulalamikiwa kushuka licha ya waigizaji kutafuta mbinu hizi na zile kuhakikisha linarudi.

Wanatamani kuliona likiwa linachanua kama wakati ambao kulikuwa na kituo cha runinga kimoja, hakuna mtandao utakaowawezesha watu kupakua filamu za nje na hakukuwa na filamu za Kifilipino, Kinigeria wala za Kihindi zilizotafsiriwa Kiswahili.

Filamu hizo za kutoka nje, licha ya kuwa ni ngeni machoni mwa Watanzania hivyo kuongeza hamu ya kutizamwa, lakini zimeigizwa kwa kuzingatia vigezo karibu vyote vya kimataifa.

Kuanzia hadithi, waigizaji, eneo lilitumika kuigizia, sauti na bila kusahau kutangaza maudhui ya tamaduni zao.

Filamu nyingi zinazoonyeshwa kwenye runinga za hapa nchini na kuwa gumzo kama vile za Kina Angelo wakati ule, Jamal Rajah na hata za kutoka Uturuki ikiwamo Sultan ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ziliwahi kuzinduliwa kwa kishindo kwenye nchi husika.

Zilifanya vizuri mara baada ya kuzinduliwa na zilikuwa zinastahili ndiyo maana miaka saba au 10 baadaye zimeletwa Bongo na zimepata mashabiki.

Wasanii wa nje hufanya movie premier, yaani filamu inaonyeshwa kwa mara ya kwanza, wakiwa na malengo maalumu , hivyo licha ya kuandaa ukumbi mzuri ka ajili ya kuonyeshea filamu hiyo, pia huiandaa kikamlifu.

Huu ni wakati muhimu kuanza kuingiza kipato kwa mwongozaji wa filamu. Kama kazi nzuri huwa inatarajiwa angalau asilimia 25 ya gharama za maandalizi hurudi wakati huu.

Filamu inapoonyeshwa kwa mara ya kwanza huwa ni tukio muhimu sana katika biashara nzima na hutoa mwelekeo wa mauzo.

Uzinduzi hufanyika wakati filamu imeshasambazwa kila kona. Baada ya kuonyeshwa kwa mara ya kwanza asubuhi yake filamu hii huanza kupatikana katika maduka na mitandao.

Uzinduzi huleta gumzo ambalo huwa chachu ya mauzo. Baada ya uzinduzi huendelea kuonyeshwa katika majumba ya sinema mfululizo na huku hurudisha angalau asilimia 80 ya gharama za filamu na inapoanzwa kuuzwa huwa imebakiza gharama kidogo kurudisha mtaji na kuanza kutengeneza faida.

Hapa nchini, miaka mitano iliyopita hakukuwa na utaratibu wa kuzindua filamu, lakini lilipokuja azimio la kufufua tasnia ukaibuka mtindo huo wa uzinduzi wa filamu ukiwa ni mpya kabisa.

Kumeshuhudiwa uzinduzi wa filamu za Foolish Age, Nipe Changu, Heaven Sent, Bei Kali, Home Coming na nyingine nyingi.

Kati ya hizo zipo ambazo hazikuingia sokoni kabisa na watayarishaji wamekuwa na sababu nyingi.

Swali la kujiuliza kibiashara ni kuwa kulikuwa na haja gani ya kuzindua filamu ilihali hata mapatano ya kuitoa au wa kuinunua hayakuwepo.

Mtindo huu umegeuka kama kijiwe cha kuonyesha mavazi, nywele na tambo zisizokuwa na tija kwa waigizaji wala tasnia.

Matukio ya uzinduzi kwa bahati mbaya , badala ya kudhaniwa yataifufua tasnia naona yameizamisha kabisa , kwa sababu kinachokwenda kuonyeshwa sicho kilichokusudiwa.

Hata hivyo msanii wa siku kwenye tasnia ya filamu Single Mtambalike maarufu Richie Richie anasema kuwa hadi mtu anaamua kuzindua filamu yake na kuiingiza sokoni anakuwa amejiamini.

Amesema kuwa “Tupo wengi ambao tunadhani tuna uwezo na tunafanya vitu vizuri =, ingawa viwango vyetu bado, ”anasema Mtambalike.

Mtambalike anafafanua kuwa binafsi anapoandika hadithi, humpa mwanafunzi au mtayarishaji mwenzake kuipitia, kabla ya kutoa maoni ua dosari.

Anasema kisha jopo hukaa kuijadili , kuiangalia na kuifanyia marekebisho kabla ya kutoa maoni.

“Hupita kote huko ili kujiridhisha na nipo tayari kukosolewa bila kujali gharama, inawezekana nina picha sina filamu, au nina hadithi sina filamu, ”anasema.

Anaeleza wanaozindua filamu wanakuwa na majibu ya maswali yote kuhusu filamu zao, kama hawana hawawatendei haki watizamaji wao.

“Kuna filamu unaitayarisha mwanzo mwisho , unaona kabisa hii nitarudisha mtaji pekee na unakubali matokeo, ”anasema.

Mtambalike anaungwa mkono na mwigizaji wa siku nyingi Mahsein Awadh Dk Cheni anayesema kuwa “Tunataka kwenda kuzindua kwenye majumba ya sinema, lakini hatujakuwa tayari kwenda theatre kuonyesha kazi za filamu”.

Anasema kabla ya kuzindua filamu kwenye kumbi za sinema ni vema kuwe na jopo la wataalamu watakaoitizama na kutoa maoni kama inafaa au laa.

“Tumekuwa tukiwachosha mashabiki wetu, wakitumia muda wao na gharama zao kuja kuangalia filamu za kawaida.

“Tusijipange kufanya ‘suprise’ isiyo na kitu, tushirikishane na ninashauri turudi tukajipange kwa sasa sidhani kama tupo tayari, ”anasema Dk Cheni.

Akiunga mkono hoja hiyo Rado ambaye alifanya uzinduzi rasmi wa filamu ya “Bei Kali”, anasema uzinduzi wa filamu kwa kuiga hauna tija.

Anasema walio wengi wanataka kuiga kila kinachofanywa na mtu, matokeo yake wanawasumbua watu kujazana ukumbini na kitu cha maana hakuna.

“Mfano mimi ninaandaa filamu nyingi, lakini bei kali ambayo niliiandaa kwa viwango vya kimataifa nikaamua kuizindua kwa sababu ilikuwa na sifa za kufanya hivyo, ”anasema Rado.

Rado anasema inawezekana wasanii wanatafuta jinsi ya kutoka kutokana na soko la filamu kushuka, badala ya kujenga wanabomoa zaidi.

“Ukianzisha kitu kwa lengo zuri, halafu usipotimiza lengo kusudiwa ambalo kwa namna yoyote ile ni ubora wa ulichokusudia kukifanya, unakuwa umeharibu, ”anasema Rado.

Chanzo: mwananchi.co.tz