Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwoya wa Insta na Barua ya Steve Jobs

36336 Pic+uwoya Uwoya wa Insta na Barua ya Steve Jobs

Sat, 12 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

‘Nadiklea interesti’. Uwoya ni sampuli ya viumbe uzao wa Eva. Anayefanya tuvimbe kwa Waganda na Wakenya. Angekuwepo zama za Leonardo da Vinci (mchoraji bora kuwahi kutokea duniani), viganja vyake vingeacha taswira yake badala ya ile ya Monalisa. Achana na mengine huyu ‘demu’ anazingua akili za marijali.

Ndikumana Katauti Hamad (marehemu). Hakuona lolote kwenye viunga vya laana ya warembo halisi pale Kigali. Akafumba macho. Pamoja na onyo la Ray Kigosi, hakutaka kusikia la muadhini wala mnadi swala. Alidata na Irene aliyemuona katika filamu ya Oprah.

Ndiku hakuwa juha ukikutana na Irene lazima upasuke. ‘Eneweyi’. Umemfuatilia insta huyu mrembo zao la Miss Tanzania mwenye malezi ya Bongo Movie? Anachofanya kabla yake alikuwapo Wema Sepenga. Naye aliishi kama Beyonce na kufanya kila kitu kama Kim Kardashian. Katika zama zake, Sepenga alifanya Kajala asiende lupango. Ogopa sana Sepenga yule.

Ilikuwa ngumu sana Sepenga kumzungumzia kisanaa. Mara nyingi alitajwa kwa matumizi makubwa ya pesa. Akiitwa madam. Msanii mkubwa bila kuwa na filamu yoyote mtaani. Akawa mfano wa kuigwa kwa utajiri usioeleweka huku akiikoroga jamii kwa tabia zake zenye ‘kunuka’. Alifunika kila kitu kwenye tasnia yao.

Mfanyabiashara kwa biashara zisizojulikana. Utawala wa Mkwere tena. Utamwambia nini Sepenga, China alienda Jumamosi akarudi Jumatatu. Akihitaji kupunga upepo, haikuwa ajabu kukodi ndege kwenda Arusha na wapambe wake. Sijui staa gani amewahi kuishi kama yeye kwa siku za karibuni?

Happiness ‘Millen’ Magesse, aliingiza pesa kubwa, mbali kabisa na yeye. Ila hakuwahi kufanya nusu ya vurugu zake. Flaviana Matata kila siku ana mikataba minono yenye pesa nyingi, lakini akija nyumbani huwa yupo tu. Utamuona Mlimani City au Dar Free Market, mavazi ‘simpo’ tu. Na tabasamu lake lile kama anataka kucheka.

Hata siku moja hawakuwahi kuishi maisha hayo. Ni kwa Sepenga tu ndiyo tuliona maisha ya nchi ya ahadi. Ila hapana. Subiri kidogo. Hata hapo nyuma kidogo tuliona ladha ya maisha ya namna hii. Japo haikuwa kama hii, ila ilikuwa karibu na hii. Wolper wa Dallas aliishi huku pia. Walewale wenye vimelea na makuzi ya Bongo Movie.

Wolper alifanya kila jambo gumu kufanywa na binti, kuwa jepesi kama unyoya. Kumiliki magari ya kifahari kama tajiri wa Mirerani. Akitumia pesa kama pedeshee wa utawala wa JK. Mwisho akaamua kuishi kama waziri wa Mambo ya Nje, akipaa kila kona kama kunguru. Namuongelea Wolper yule siyo huyu fundi cherehani.

Aliyemchangia Sajuki (RIP) pesa ya tiba. Akisema sanaa inalipa nd’o maana mtoto wa kike anamiliki magari na fedha nyingi. Aliyebadili dini na kuitwa Ilham. Akiapa kuwa hata iweje hawezi kurudi katika Ukristo na kuvaa rozali. Alisimama kwa kujiamini, akitueleza kuwa kila kitu kinawezekana ukifanya kazi kwa bidii. Pesa bwana!

Wasichana wa mjini wale wa blog za U turn na BBM kabla ya insta walitamani sana maisha yake. Akawadharau waliosema mali na pesa siyo zake bali anahongwa tu. Jack alikuwa juu. ‘Maprodyuza’ walimuogopa kwa dau, na wasanii walimpapatikia kwa mkwanja wake. Nani hataki kuguswa na shombo la pesa za Wolper?

Kila mmoja alihitaji nafasi ya kuwa karibu naye. Ila sasa mambo yamebadilika. Baada ya Wolper kuwa hoi ndipo akaibuka Sepenga yule wa Endless fame na kufanya fujo nyingi sana bila huruma. Duru sasa limekamatwa na Uwoya. Ni muda wake bwana. Ni muda wa kuvimba na kufanya kila alichotamani kufanya na usiweze hapo kabla.

Wapi alikuwa hajafika? Vazi gani alitamani kulivaa? Ni suala la kujaza kabati sasa. Maisha yake kwa wasanii ni maumivu. Wengi wako juu ya mawe hivi sasa. Ni zaidi ya mawaziri na wabunge kibao katika utawala huu usio na pesa za kibwegebwege.

Huku semina, tripu na posho za hovyo zikitoweka kama panzi mjini.

Ni vile bendi zimepigwa ‘fatwa’ na kupoteza hadhi. Wakati ule jina lake lingetajwa na wanamuziki Sepenga alifanyiwa hivi. Ndiyo maisha. Maisha waliyochagua Bongo Movie pale wapatapo mkwanja. Anapotokea ghafla kiumbe fundi wa kutumia pesa kipumbavu hutekwa kikatili ili nao wafaidi robo ya maisha ya dunia ya kwanza.

Katika mastaa wa kike wenye thamani ya juu mitandaoni Uwoya namba moja kwa sasa. Anafuatiliwa na mashabiki wenye kupenda mwonekano kuliko sanaa yake. Hata mastaa wenzake wanatamani kuwa yeye kwa kubadili pamba kila siku. Leo hii huko insta lazima Uwoya atakuwa na vazi jipya tofauti na jana.

Wanaanza namna hii ghafla utasikia kaagiza kontena la samani za ndani au la vifaa vya mbwa. Sepenga aliwahi kufanya hivi au Uwoya akawa zaidi yake. Mbali na mafanikio aliyonayo Jide, hajawahi kuishi katika dunia ya hawa Bongo Movie. Anaacha kula bata muda wote anafanya kazi tu? Hana maana!

Bongo Movie wakipata hugeuka pedeshee, kila mwanamuziki wa bendi atataja jina lake asifie, na kisha akamjaze pesa. Kwa sababu vipato vyao hutoka kwa watu wa aina hii. Kwani tatizo nini? Wamechagua maisha haya. Kufanya kazi kwa bidii? Kuumiza vichwa? Wanasubiri ziletwe kimiujiza ili watambe.

Badala ya kutumia umaarufu kuwapa mizuka watoto kama kioo. Wao wanaaminisha kuwa ustaa na mrembo ni utajiri. Unatajirikaje? Hapo hawaweki wazi wanaishia kusema sanaa inalipa. Kwa namna gani bila filamu mitaani? Wanakuuliza nao kwani tatizo nini? Life is a game of chance, bwana! When you get it, use it effectively.

Karibu sana Irene Uwoya katika maisha haya. Utapata faida na thamani ya usanii. Siku hizi ndoto siyo kwenda kimataifa kama zamani, bali kupata maisha matamu kwa muda mfupi. Haya ndiyo maisha aliyoishi Wolper na mwisho hana kitu baada ya kutoswa na Dallas. Leo katulia anajua anachofanya.

Maisha ya kutambia vitu ambavyo hatujui kama kesho vitabaki katika maisha yenu. Mama la mama Sepenga aliishi hivi. Utajiri usioeleweka na kutamba kiasi cha kila msichana atamani kuwa yeye ofisi yake ikabaki jengo badala ya kufanyia kazi. Karibu Uwoya. Ni filamu kama tunayoijua mwisho wake. Ni ‘steringi’ kufia kwenye maua.

Barua ya Steve Jobs

Nilifikia kilele cha mafanikio katika biashara duniani. Kwa macho ya wengine, maisha yangu ni kielelezo cha mafanikio. Hata hivyo mbali ya kufanya kazi nina furaha ndogo. Kwa jumla utajiri ni uhalisia tu wa maisha ambayo nimeyazoea.

Nipo kitandani mgonjwa nikikumbuka maisha yangu yote, nagundua ufahamu wa utajiri nilionao umefifia kwa kuwa hauna maana kifo kinapokaribia. Niko gizani nauona mwanga wa kijani katika mashine zinazonisaidia kuendelea kuishi, nasikia mungurumo wake, nahisi pumzi za Mungu na za kifo zinakaribia.

Sasa nafahamu kwamba tunapolimbikiza utajiri wa kutosha inatupasa kufuatilia mengine ambayo hayahusiani na utajiri. Kiwe kitu muhimu zaidi. Uhusiano, labda ni sanaa, au ndoto inayoanzia katika siku za ujana.

Kutafuta utajiri muda wote humuingiza mtu katika maisha yasiyofahamika. Ni kama mimi. Mungu alitupa hisia za kutambua pendo katika kila moyo wa mtu na siyo mauzauza yanayoletwa na utajiri. Utajiri nilioupata maishani mwangu siwezi kuondoka nao.

Ninachoweza kuondoka nacho ni kumbukumbu zilizojaa upendo. Huo ndiyo utajiri wa kweli utakaokufuata na kuungana nawe. Upendo unaweza kusafiri maelfu ya maili. Maisha hayana kikomo. Nenda unapotaka. Fika katika kilele unachotaka. Ni kitanda gani cha gharama duniani? Ni kile wanacholalia wagonjwa.

Unaweza kuajiri mtu kuendesha gari lako na kukuingizia fedha, lakini huwezi kupata mtu wa kubeba ugonjwa wako. Vitu vilivyopotea vinaweza kupatikana, lakini kuna kitu kimoja ambacho hakipatikani pindi kikipotea. Ni Maisha.

Mtu akienda chumba cha upasuaji atagundua kuna kitabu hajamaliza kukisoma, ‘Kitabu cha Maisha ya Afya.’ Hata ukiwa katika daraja gani la maisha muda ukifika utakabiliana na pazia la maisha litashuka. Thamini upendo kwa familia yako, mpende mwenza wako, wapende marafiki zako. Jitambue vyema. Wathamini watu wengine.

Steve Jobs alipomaliza kuandika barua hii, Izraeli aliyekuwa ‘araundi’ akipasha misuli moto akaitwaa roho yake na nd’o ukawa mwisho wa maisha yake huku akituachia wasia bora kabisa. Maisha nd’o haya.



Chanzo: mwananchi.co.tz