Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usiyoyajua kuhusu penzi la Juma Nature na Sinta (Part 3)

Sinta Naturee Usiyoyajua kuhusu penzi la Juma Nature na Sinta (Part 3)

Fri, 15 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maelezo ya Nature, Sinta alimuomba awe naye waende kula bata Billicanas Club (ukumbi wa Mheshimiwa Mbowe ambao ulishavunjwa, usiutafute hauko kwenye ramani tena).

Nature alimkubalia kwa mujibu wa ngoma hiyo, hapa Kiroboto alitaka kutuaminisha Sinta ndiye aliyekuwa na Shobo sana kwake, lakini ukweli huwa haujifichi hata uufiche vipi, ukweli una kawaida ya kujitokeza wenyewe, kupitia wimbo wa Inaniuma sana, utaona kwamba ni kwa namna gani Nature alikuwa na Maumivu na kuvunjika kwa penzi lake na Sinta, maana aliimba kwa hisia kali sana, Nature anasema,

Unadai unakwenda shooting kumbeee eeeh unakwenda kufanya booking mbona haujitangazi kuwa hivi sasa we unauza ili kuwasave washikaji ili nao wapate kujiuguza we mwana hebu angalia huo uthamani wa wa utu wako halafu tofautisha na uthamani huo wa upumbavu wako kwa kucheza dili na magazeti ili waweze kuharibu jina haya sasa hili swala kubwa ni lako mama usimsingizie Nina Endelea kuponda mali mtoto naye Mungu atakusaidia kila akitoka tu mpenzi wangu andika umeumia wanaume wapo wengi wanene na wenye fedha fedha nyingi ambao wanapenda mademu kama nyinyi wenye wanaume wengi wenye nguvu za simba na wasio ogopa risasi na wenye kuhonga twelve million or six dollars,

Hapo Nature alizungumzia jinsi Sinta alivyomuaga kuwa anakwenda Mwanza kushiriki video tu na si vinginevyo, kumbuka kuwa Nature hakutaka Sinta akashiriki kwenye hiyo video, msichana akamtuliza, tulia baby mimi ni wako peke yako...

Naenda kushuti tu video hakuna kingine" hii ishu ilimuuma sana Kiroboto, akajikuta akiwa na bifu la chini kwa chini na Cool James mtoto wa Dandu, Nature anaposema kucheza dili na Magazeti, anamaanisha Sinta alipenda sana Skëndo, alikuwa na tabia za kupenda kiki.

Hii Nature aliona ni kama Sinta alitaka kumuharibia jina, Kwa hakika huu ulikuwa wimbo bora zaidi wa masimulizi wakati huo, nadhani hadi leo ndio wimbo unaoweza kukimbizana na ‘Zali la Mentali’ kwenye historia ya nyimbo za masimulizi ya mapenzi ya Bongo Fleva zilizoshika sana.

Juma Nature alimtaja jina Sinta kisanii, akieleza kuwa alimsaliti na mlevi mmoja ndiye aliyetoboa siri. Nature anasema

Niliuzunika sana hii kitu mimi sitosahau ulipigwa denda mpaka gari ikagoma kwenda mlijiona mpo new york city starehe kugeana mirenda kabla hujaondoka uliniomba hela ya kwenda, ukaniambia nisiwe na hofu mimi nipo peke yangu Siri ikafichuka mlipo toka mlipo kwenda kuna mlevi mmoja alilewa akalopoka Huko tulikokwenda noma kweli, Sinta na jamaa mmoja si walinyonyana, ulimi njenjeee… hadi kupata ajali wakati mumewe yu safari…”

Kwenye mistari hiyo Watu wakaunganisha matukio, kweli Sinta aliwahi kupata ajali ya gari akiwa na Cool James Dandu, wakitoka kufanya video ya wimbo.

Turudi siku ya uzinduzi wa albamu ya Ugali, jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake ilihamia Diamond Jubilee, Nature akaandika historia ya kuujaza ukumbi ule hadi ukatema.

Kila mmoja alitaka awe wa kwanza kuula ugali uliokuwa unapakuliwa mle ndani. Ukitaka kujua Nature alifanya balaa, ni Sean Paul peke yake wakati huo ndiye aliyekuja kuujaza pia ukumbi huo, ingawa bado ya Nature ilifurika na kucheua sana.

Kuanzia hapo, ndipo alipopewa heshima ya kuitwa Sir. (Sir. Juma Nature). Kwa Uingereza, Malkia ndiye anayeweza kukubatiza wadhifa wa Sir. kutokana na kazi nzuri uliyoifanya kwenye eneo lako.

Nature uso kwa uso na Sinta ni jijini Mwanza, Baada ya uzinduzi huo, Sir. Nature na timu ya Bongo Records wakafanya ziara kwenye majiji na miji mikubwa yote kuwalisha watu ‘Ugali’. Kila walipofika, walaji walikuwa na njaa ya maana na kumbi zilifurika.

Alipofika Mwanza, Nature na timu yake walikosa ukumbi wa kuwaweka watu wale ugali pamoja, ikabidi show ipigwe kwenye uwanja wa CCM Kirumba.

Ikumbukwe kuwa wakati huo Sinta alikuwa Mwanza akifanya kazi kama mtangazaji wa redio. Jiji likazizima, watu wakala samaki kwanza kisha wakaelekea CCM kirumba kula ‘Ugali’.

Basi unaambiwa kivutio kikuu, Sinta naye alikuwa miongoni mwa wahudhuriaji akiwa na timu yake.

Muda wa show, Sinta na timu yake walishindwa kuvumilia wakimsikiliza Nature akianika yote kwenye mdundo wa P-Funk pale CCM Kirumba.

Watu wakiwa wamefurika wakiimba naye mstari baada ya mstari. Sinta naTimu yake wakaanzisha fujo hata hivyo haikuathiri chochote, maana iliwahi kudhibitiwa. Unaambiwa ilikuwa show ya aina yake, uwanja ulifurika kama kuna mechi ya Simba na Yanga kumbe ni Sir. Nature aka Kiroboto.

Umati ule naufananisha na show ya bure ya Awilo Longomba aliyowahi kuipiga Mwanza wakati ule akiwa juu ‘mawinguni’ na Mobimba ya Mama. Haya yote nimeyajua kupitia magazeti ya udaku, msiniulize nimejuaje.

Mauzo ya ‘Ugali’ yakapaa, ingekuwa Marekani tungesema labda yalifika ‘Platinum’, ‘Gold’ au ‘Silver’ ila Kibongobongo mfumo wetu ulikuwa hauruhusu kujua nakala ngapi kwa uhalisia. Albam zilikuwa zinauzwa kwenye kanda na sio CD. Mhindi ndiye aliyekuwa anajua ukweli wa nakala alizogonga, wezi nao walijua kunakili na kuuza tena.

Lakini Kupitia mauzo ya albamu hiyo, Nature alinunua gari aina Mark II mpya, ikapata ajali na akanunua nyingine hapo hapo, famasikhara nini!! Unaweza kuona kama masihara ukiizungumzia Mark II kwa sasa, kipindi ambacho wakina Diamond Platinumz wanatembelea magari ya kifahari kama Rolls Royce na Cadillac Escalade.

Nature alikuwa habari ya mjini na Mark II yake. Kwa kifupi, Juma Nature aligeuza matatizo ya penzi lake na Sinta kupiga hela...na akapiga kweli kweli. Baadaye, tukaambiwa Sinta alifanya utovu wa nidhamu kwenye kituo cha redio alichokuwa akifanyia kazi na akaachishwa kazi.

Akarudi Dar es Salaam kuendelea na fani yake ya maigizo ambayo alifanikiwa sana pia kutokana na uwezo wake pamoja na jina alilokuwa nalo.

Hivi sasa Sinta ni mmoja kati ya waandishi wa habari wenye elimu ya juu, aliwahi kuweka wazi kuwa alichukua Shahada ya Uzamili (Master’s Degree) nchini Uganda.

Ukitaka kujua zaidi na zaidi kuhusu Sinta mfuatilie kwenye website yake, Kuhusu Cool James Massive Mtoto wa Dandu, Mwamba alifariki Agosti 27, 2002 kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Makumbusho jijini Dar es Salaam nyota yake ikiwa inang'ara kinoma na kuzua simanzi kubwa miongoni mwa mashabiki wake hususan wanawake ambao walikuwa mashabiki wake wakubwa. Akaenda kuzikwa nyumbani kwao, Mwanza.

Wakati anakufa, alikuwa bado hajamaliza kurekodi kazi zake mpya katika Studio ya Master Jay. Aliacha watoto wawili wakiwa bado wadogo pamoja na mjane, Devotha Rest in peace Cool James Dandu,

Turudi kwa Sir Nature, Ugali itabaki kuwa kati ya albam tano bora za muda wote za Bongo Fleva.

Kwangu mimi kwenye hizo tano bora za muda wote, nyingine ni ‘Machozi Jasho na Damu’ ya Profesa Jay, ‘AKA Mimi’ ya Ngwair "Elimu Dunia ya Daz Baba, Machozi ya Lady Jaydee Comando,

Huyo ndiyo Juma Nature aliyetumia akili nyingi sana kuyageuza Maumivu ya kuvunjika kwa penzi lake na Sinta, kuwa fursa ya kumuingizia mamilioni ya hela, kwa sasa huwezi kuitaja historia ya Bongo Fleva bila kumtaja Sir Nature Ni msanii aliyefanikiwa kuitambulisha vizuri Bongo Fleva ndani na nje ya Tanzania.

Aliwahi kushindanishwa Tuzo ya Video ya Channel O (CHOAMVA), ya Most Gifted East (Video Bora ya Muziki-Afrika Mashariki), na amewahi kutajwa kuwania Tuzo za MTV Europe, kwenye kipengele cha Best African Act (Msanii Bora wa Afrika).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live