Pengine ni sahihi kama tukianza kuizungumzia Temeke kwa kuutaja uwakilishi wa mwanzo kabisa wa kundi lililofahamika kama Gangstaz With Matatizo ama kwa kifupi GWM.
Humo aliyesikika zaidi alikuwa Kaka Rashid Ziada (KR MULLAH CD 700 MUZIKI MKUBWA, JIBABA) akiwa sambamba na Dotto D Chief)
GWM MAZIMWI walianza game KITAMBO huko 90's na kutajwa na wakongwe wengine na kushirikishana na waasisi wengine kama Sugu kwenye ngoma ya YAMENIKUTA, baadaye sana wakamwita Nature kwenye chorus ya KAMUA.
GANGWE MOBB ni kundi lingine la awali kabisa kuipeperusha bendera ya Temeke chini ya UONGOZI imara wa Haruna Kahena, Inspector Haroun Babu akiwa sambamba na Karama Masudi Ngengemkeni Mitomingi aliyeona kama mwenzake anajiita INSPEKTA basi yeye ajiite LUTENI, hivyo akawa LUTENI KARAMA.
Simulizi la ufasaha ilikuwa album kali sana japo upepo ukawa unayumba na kuipeperusha GANGWE na kufanya kila mmoja kuangalia ustaarabu wake.
Inspekta alikuwa na nguvu sana mpaka akawa kiongozi mkuu wa ukoo mkubwa wa WALUMENDAGO lakini baadaye nyota ikaangukia kwa Juma Nature.
SIR NATURE alianzia kwenye chorus za Wana wa TMK lakini pia alishiriki kwenye vesi zao ikiwemo MTULIZE. Baada ya hapo, akaanza kutoa magoma yake na kujinyakulia ufalme wa Temeke.
Nature alifanya chorus za makundi madogomadogo yote yaliyokuwa na asili ya Temeke ndipo walipoona wamezoeana, wakaona bora wavunje makundi madogo na kusimamisha kundi moja kubwa.
MANDULI MOBB ilikuwa ina vichwa vitatu; Mangi Amani James Temba, mkali wa mpira wa kikapu almaarufu Fundi Mheshimiwa Temba, Man Tsuki, PRODUCER wa TBT Records na Daz P Bwana Mkubwa mzee wa " Kama unataka KUJA HOME, iliyorudiwa kivingine na Mnyakyusa Raymond.
MABAGA FRESH ni jina linalorejelea Hali ya ulemavu waliyo nayo members wa kundi lakini wakaona wakijiita MABAGA pekee ingekuwa kama walikuwa WANYONGE, wakaongeza neno FRESH kuonesha kwamba japo walikuwa walemavu lakini walikuwa kamili, poa, au vizuri.
MTULIZE, 770, TUNATEGA MABOMU na MAISHA YA KISELA FT YP ni vyuma vya Hatari sana kutoka kwa Hawa wajomba.
WACHUJA NAFAKA ni kundi lingine dogo ambalo, ukitoa Nature na KR niliowazungumzia hapo juu, basi humo alikuwepo DOLLO. YA LEO KALI, RADHIA, KUISHI NA WATU FT DOMOKAYA na KUWA NAWE TENA FT JOSLIN ni ngoma ambazo alifanya makamuzi makubwa.
MANYEMA FAMILY ni kundi lingine dogo lililokuwa na tofali lake kwenye ujenzi wa familia kubwa ya Temeke.
Kulikuwa na vichwa vitatu humu lakini nyota njema iling'aa zaidi kwa Said Chegge Chigunda mvunja nazi kwa ugoko ambaye alipata usajili wa kudumu kwenye familia ya WANAUME huku wenzake wakipotea.
ADHABU ULIYONIPA FT INSPECTOR, na NDIVYO ILIVYO FT NATURE ni ngoma zilizowatambulisha, kabla ya mdude wa maana ulioitwa LONG TIME AGO. Chegge akaubeba mgoma huu na kuurudia na familia yake ya WANAUME.
SIDE FELLA, Mtanzania ALIYEKUWA akifanya mishe zake Bondeni kwa Wazulu alikutana na vijana wenye HASIRA kali ya muziki na wakaona waunganishe nguvu; wenye vipaji na mwenye pesa. Hapo ndiyo ukawa mwanzo halisi wa familia kubwa kujengeka.
SANTANA NUNDA SWEBE alikuwa injini kubwa sana kwenye umoja huu wa Temeke ambao mpaka kufikia hapo haukuwa na jina kamili. Ndipo Swebe alipoona members wote ni wanaume, HAKUNA mwanamke na wote walitokea Temeke ndipo ikapendekezwa wajiite TMK WANAUME FAMILY, japo jina likapokelewa vibaya na baadhi ya watu wakisema lilibagua wanawake.
YP NA Y DASH ilikuwa pacha bora sana kwenye game. Yessaya Ambilikile, "sauti ya pombe kali - YP" alianza kuingia kwenye familia na walipoenda Mwanza kupiga shoo, wakavutiwa na Y Dash na kurudi naye mjini.
Ufanano wao wa karibu wa sura na sauti ukafanya wasimame kama kundi dogo ndani ya kundi kubwa na kuibuka na SHEMSA, UMEWAONA, MAPENGO MATATU, TUKO CHIMBO FT CHELEA MAN, na PUMZIKA.
MANYIGU walijipa jina lililobeba maana ya ukali wao. Kuna mdude unaitwa MKAO WA KULA, oyaaa! Kuna mdude unaitwa KALA MNYAMA, Kuna traki iliitwa TUTOKE, unazikumbuka?
Makamuzi humo yalifanywa na watu wabaya; LUKENZA MAN, MZIMU, STICCO na BK.
TMK WANAUME HALISI ilizaliwa baada ya Nature kuona mambo hayakuwa sawa chini ya mikono ya Fella, " umetunyonya vya kutosha, we mnene si wembamba" hahahahah huyu mwamba alinifurahisha sana kwa line hii. Hapa kulikuwa na vichwa kama; RICH ONE mzee wa HATUNA KITU FT NATURE na NDIVYO NILIVYO FT NATURE NA INSPEKTA.
Baba Levo, promax chawa wa kizazi kipya alikuwa ubishini, ugumuni kipindi hicho. Alikamua kwenye ngoma ya MZAMIAJI
KG SON alikuwemo pia kwenye hili chama, alikamua kwenye ngoma iliyoitwa SHUKRANI.
MALIPO pia alikuwemo humu, alipita kwenye goma liitwalo SHUKRANI.
TMK UNIT ilijimega pia baada ya fagio kupita kwa mara nyingine tena ndani ya WANAUME HALISI
Hapa sasa linaongezeka jina ambalo sikulitaja hapo juu, Jebby Mubarak. Unazikumbuka; WANAPAGAWA, ORODHA, SWAHIBA FT AFANDE SELE na WAMADAU? Jebby huyo.
YP, JEBBY na BK walishafariki.
P Funk, Dunga, Papa Love, Producer Jonas, Mika Mwamba, Marco Chali na Man Walter ndiyo wapishi wakuu wa magoma mengi kutoka kwa vichwa hivi.