Dhana ya usanii inapaswa kuelezwa vema shuleni na wasanii wenyewe pia wanaweza kuieleza vizuri kupitia kazi na matendo yao.
Tafsiri inayojengeka vichwani mwa watu wengi pale wanaposikia mtu akisema “Fulani ni msanii” hujenga tafsiri kuwa ni mwongo, mzushi na tapeli.
Pia, ni mbabaishaji na tabia zote mbovu tuzijuazo. Jambo hilo siyo sawa hata kidogo, hiyo ni tafsiri potofu ya usanii.
Usanii ni taaluma. Usanii ni ubunifu wa vitu mbalimbali unaofanana na uumbaji. Msanii ni mtu anayejishughulisha na usanii na kile anachokibuni au kukiumba.
Kwa kupitia kazi zake au vitu anavyoumba kama vile picha ya kuchora, fasihi au muziki; msanii wa kazi za sanaa hupata fursa ya kueleza hisia zake za ndani kama vile furaha na huzuni yake au ya wengine. Wakati mwingine lengo la kazi ya sanaa huwa ni kuonya, kukosoa, kuelimisha au kuburudisha.
Msanii ni mtu muhimu katika jamii kwa sababu kwa njia ya sanaa ni rahisi kufikisha ujumbe kwa watu wengi kwa wakati mmoja hasa sanaa ya uimbaji au uigizaji. Sanaa ya uchoraji huchukua muda kufikisha ujumbe au burudani lakini ni sanaa inayotunza ujumbe au kuvutia kwa muda mrefu zaidi.
Kwa mfano, uchoraji wa vibonzo au katuni umekuwa nguzo muhimu katika kufikisha ujumbe katika lugha nyepesi katika magazeti, majarida na vyombo vingine.
Nchi za Ulaya na Marekani, sanaa ya uchoraji inathaminiwa kwa kiwango kikubwa, ikilinganishwa na namna inavyochukuliwa katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.
Baadhi ya wazazi, walezi na hata walimu wamekuwa wakiwakatisha tamaa watoto na vijana wanapowaona wakijishughulisha na uchoraji au kuimba
Sanaa ina nguvu ya kuvunja minyororo ya dhuluma. Mwalimu Richard Mabala aliwahi kutoa kisa kimoja cha mchekeshaji ambaye alikuwa akisimama mbele ya mfalme na kuchekesha katika himaya fulani.
Msanii huyo kuna wakati aliweza kusifia, kuelimisha, kuburudisha na hata kumkosoa mfalme kwa kutumia sanaa hiyo ya ucheshi kiasi cha kumfanya mfalme afurahi badala ya kukasirika.
Mfalme alifurahia ucheshi huo kwa sababu ulimsaidia kupata mrejesho wa namna himaya yake inavyoutazama utawala wake.
Ukweli huo uliogopwa kusemwa na wapambe wake na hata wasaidizi wake lakini kwa kutumia sanaa iliwezekana. Hivyo, sanaa inapotumika vizuri ina faida nyingi.
Siku hizi watu wanaolaghai au kutapeli huitwa kwa jina la ‘wasanii’. Ni matumizi mabaya ya neno ‘usanii’.
Ingawa watu hao wababaishaji pengine hutumia chembe chembe za sanaa au ule uwezo wao wa kushawishi wa hali ya juu kiasi cha mtu anayeibiwa kuamini; watu wa namna hiyo hatupaswi kuwaita wasanii. Hao siyo wasanii, hao ni wezi au matapeli.
Msanii halisi hutumia sanaa zake kama za maigizo, ucheshi, mafumbo, mashairi, riwaya, tamthiliya na ubunifu mwingine kufichua uovu kwa kuonyesha ukweli katika sura au namna tofauti ili aweze kueleweka zaidi. Lakini wapo watu katika jamii ambao hushindwa kueleza ukweli.
Kwa mfano, katika ulingo wa siasa, mwanasiasa ambaye leo anashangilia kile ambacho jana alikikejeli na kukiponda hadharani; huyo hafanyi usanii. Matendo hayo anayofanya yanapaswa kuitwa ghiriba, unafiki na uzandiki.
Kwa hiyo, jamii haipaswi kuchanganya maovu hayo na sanaa. Matendo hayo maovu hayana sifa za kuitwa ‘sanaa’ au ‘usanii’ hata kidogo.
Kitendo cha wasanii kunyamaza au watu kuremba mambo hayo kwa kuyaita usanii, ndiko kunakoitafuna jamii na kujikuta inashindwa kuelezana ukweli kuwa huo ni wizi, ulaghai na unafiki.
Sanaa ni taaluma. Watu huweza kusoma na kupata astashahada mpaka shahada za juu za usanii.
Hata hivyo, jamii inaweza kuchanganya pale inapoona kwa mfano kuna wasanii ambao wamefanikiwa kiuchumi kwa kutumia vipaji vyao pasipo kuingia katika darasa rasmi kujifunza.
Hao waliweza kujitambua na kutumia nguvu ya ndani waliyojaaliwa na Mola kufanya sanaa.
Lakini hilo haliwezi kuondoa ukweli na maana ya sanaa kuwa taaluma kama taaluma nyingine. Sanaa ina miiko na kanuni zake.
Pia, wasanii ni kioo cha jamii. Wasanii huimulika jamii, huikosoa, huishauri na mwisho huiburudisha.
Fikiria dunia ambayo haina sanaa ya muziki au fikiria dunia pasipo vyombo vya habari; fikiria dunia pasipo michoro wala mapambo, pasipo ubunifu wa mavazi na pasipo fasihi na burudani.
Itakuwa dunia yenye ukiwa. Sidhani kama kuna mtu atatamani kuiishi dunia ya hali hiyo. Kwa sababu, watu watakuwa na misongo ya mawazo, watu watakasirika hovyo, watu hawatakuwa na matumaini na watakosa faraja maana hata kumfariji mtu ni sanaa pia.
Sanaa haiwezi kutenganishwa na maisha yetu ya kila siku. Viongozi wa dini, walimu, wanasiasa, wahandisi, matabibu na wengineo hutumia sanaa katika kazi zao.
Wapo wanasiasa wazuri ambao hutumia sanaa vizuri kwa kutotumia usanii kuficha ukweli wa mambo. Hawa huitwa wanasiasa halali. Nao tunawahitaji katika jamii yetu ili tuweze kufikia maendeleo endelevu.
Hivyo basi, uvamizi wa makanjanja wa sanaa umesababisha kushusha hadhi ya sanaa nchini.
Msanii ambaye hutambua thamani ya sanaa yake, kazi zake zitaheshimika na kudumu kuliko yule msanii anayefanyia tumbo na kujikuta wakati mwingine akivunja miiko ya usanii na sanaa.
Ni vema jamii ikaungana kwa pamoja na kukuza uwezo wa watoto na vijana katika misingi imara ya kufanya kazi za sanaa kuanzia shuleni kama taaluma na siyo kama kichaka cha uovu.