Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa hali ya upweke imekuwa kipaumbele cha afya duniani ambapo limezindua Tume mpya ya ‘Uhusiano wa Kijamii’ kwa ajili ya kushughulikia suala hilo huku ikielezwa kuwa athari za upweke zinaweza kuwa mbaya kama kuvuta sigara 15 kwa siku na ni kubwa kuliko athari zinazohusiana na unene na kutofanya mazoezi ya mwili.
CNN imeripoti kuwa Tume hiyo inalenga kushughulikia upweke kama tishio kubwa la kiafya, kukuza na kuwezesha mahusiano ya kijamii kuwa yenye kipaumbele na kuharakisha utafutaji wa suluhisho la upweke duniani.
Tume hiyo inaongozwa na Daktari Mkuu wa Upasuaji wa Marekani Dkt. Vivek Murthy na Mjumbe wa Vijana wa Umoja wa Afrika Chido Mpemba huku ikijumuisha Mawakili 11 na Mawaziri wa Serikali kama vile Ralph Regenvanu, Waziri wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini Vanuatu, na Ayuko Kato, kutokea nchini Japan.
Ndani ya miaka mitatu Tume itatoa ripoti itakayobainisha jinsi upweke na hali ya kutengwa na jamii inavyoathiri afya ya kimwili, kiakili na kihisia ambapo kwa mujibu wa Dkt. Murthy, athari za upweke zinaweza kuwa mbaya kama kuvuta sigara 15 kwa siku na ni kubwa kuliko athari zinazohusiana na unene na kutofanya mazoezi ya mwili.
Hali ya upweke ilizidi kuwa mbaya baada ya janga la COVID-19 wakati ambapo Watu hawakuruhusiwa kujumuika na wenzao kwenye Jamii.