Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unataka kuwa staa Bongo? pita njia hii...

65756 Staa+pic

Sat, 6 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukipiga pesa na kuamua maisha yako yawe kwenye uso wa kijamii, unaweza kuundiwa timu bila wewe kujua. Kama wewe ni Pilimbimbi na ikitokea ukamtwaa Kajala, utajikuta tu kwenye Team Pilimbimbi-Kajala na ukatamba Insta, WhatsApp Groups, Facebook na kwingineko.

Harmonize bila muziki, noti na u-WCB. Angeweza kummiliki Wolper? Ukweli usemwe. Kama si mafanikio ya kimuziki japo kidogo aliyonayo. Wolper angeishia kumtazama kwenye video. Ni kama Diamond bila jina na mafanikio, asingetosha hata kuwa houseboy wa Zari.

Mafanikio yanaweza kukupeleka katika dunia ya video uwe unatazamwa. Je, ndivyo unavyotaka? Kama jawabu ni ndiyo basi wewe saka ‘mahela’ kama alivyoimba hayati Albert Mangweha ‘Ngwair’. kisha utaona matokeo na maajabu yako.

Mafanikio hufanya watu wautukuze mkaa kama kitu cheupe. Ukizungumza lafudhi ya kilugha na hujui Kiswahili. Utaambiwa unazungumza kwa swaga, tena watatokea mabwege wa kukuiga unavyozungumza. Utasaidiwa hata kucheka. Kwenye pesa upuuzi hugeuka dhahabu.

Ndicho kinachofanywa na mastaa wetu. Upuuzi umegeuka kuwa kitu cha thamani. Staa anayeishi kwa umakini, akichagua mavazi lugha na vitu vya msingi kwa kujali utu na jamii. Huishia kuonekana bwege na pengine asifike popote kisanii.

Utapewaje tuzo ikiwa huna mashabiki insta wa kukupigia kura? Maana tuzo nazo kama vile unawania udiwani. Unaheshimikaje huna team yako? Unatetewaje na ‘folowazi’ wako wasiofika 200 insta? Fanya upuuzi ufuatiliwe mitandaoni. Ujenge timu yako bila Amunike.

Pia Soma

Sikia. Hii ni moja kati ya sababu nyingi zinazofanya sanaa ya Bongo itoweke au kuwa duni. Kukosekana kwa mashabiki waaminifu wa sanaa. Waliopo wanapenda tu vituko na upuuzi wa wasanii. Unahitaji kufyatua akili yako kidogo ili ufanikiwe kisanaa kwa sasa..

Kupenda vituko vya wasanii ni dhambi kubwa kwa sanaa. Ni vigumu kufahamu mashabiki wanahitaji nini. Unaweza kudhani wanapenda kazi yako lakini utawajua vizuri pindi ukitoa kazi nzuri kama hufanyi vituko. Hawana habari na wewe.

Wema Sepetu. Umaarufu wake ulikuwa mkubwa na uliongezeka kila siku. Licha ya kuwa ni Miss ambaye hakufanya lolote Miss World. Kabla yake alipita Nancy Sumari, aliyefanya vizuri zaidi na kubeba taji la Miss World Afrika. Akishika nafasi ya sita kwa warembo 100 duniani.

Wema hakuwahi kufika hata 15 bora. Alipita kama upepo kwa kila taji alilowania kwa mwaka huo. Miss Tanzania 2009, Miriam Gerald, wakati wake alikuwa kati ya warembo 40 kati ya 100 walioshiriki Miss World. Lakini Wema ni maarufu zaidi ya waliopata matokeo bora Miss World.

Kwanini? Kupitia vituko vyake Wema hasahauliki. Umaarufu wake ni mkubwa akiwa na wafuasi wengi Instagram kuliko yeyote. Anacheza na ameshacheza filamu nyingi. Hata hivyo kuna vichwa vina uwezo tena kwa mbali kabisa mbele yake.

Mashabiki wanapenda msanii aina ya Wema. Mzalishaji wa ubuyu. Migogoro ya wasanii na kashfa kuliko maendeleo ya sanaa. Maisha ya Wema ni ya wazi hasa kwenye mapenzi na misuguano ya mara kwa mara. Picha zake za aibu na mengine, hufanya aendelee kuwa juu kwa jina lake kuliko wenzake.

Kuna watu huwaambii kitu kuhusu Wema. Wanampenda kuliko anavyojipenda. Wako tayari kwa ajili yake kuliko mama yake. Ukiuliza sababu hata wao hawajui kabisa wanachompenda nini bali wanampenda na hakuna sababu zaidi ya vituko.

Kiba na Chibu. Hii ndo kali kuliko. Timu zimetengenezwa kama Simba na Yanga. Nani mkali? Hilo ndo wanalopenda mashabiki zaidi hata ya muziki wa wawili hawa. Mashabiki hata wao wenyewe wamegeuka vituko. Sanaa ya Tanzania inapitia majaribu mengi. Wengi hawataki hata kusikiliza ubora wa upande wa pili.

Simba na Yanga hukiri udhaifu wa timu zao. Na zaidi husema ubora wa mpinzani. Wa Dai na Kiba ni tofauti. Kwanza ni wajuaji kwa kila kitu. Kila upande unataka usifiwe tu. Wa Dai wanataka Dai asifiwe wao tu, na Kiba akosolewe tu. Wa Kiba pia wanataka sifa nzuri kwa Kiba tu, na Dai asemwe vibaya tu.

Hawataki kuona msanii wao anakosolewa kwa ukweli na kumjenga. Wanataka kuona akipambwa tu. Mashabiki wa Kiba na Dai ni vituko zaidi kwenye sanaa. Wanapenda ushindani wa nani mkali kati yao lakini si wapenzi wa sanaa. Mwenye kupenda sanaa atafurahia msanii wake akikosolewa.

Ukitoa ushauri kwa Dai wa kumjenga, utaonekana ni ‘Team Kiba’ umetumwa. Ndivyo ilivyo hata kwa Kiba, zaidi ya kumpongeza ukileta ushauri utabatizwa ‘Uteam Wcb’. Hawaangalii ushauri uliotolewa na msingi wake. Wanajikita kwenye eneo dogo la kwa nini mtu wao aguswe?

Ukiendelea kukaza shingo kwa ushauri. Wataona una chuki. Ili uwe shabiki wa Diamond jitengenezee uso kwamba, hata Kiba afanye vizuri kiasi gani hamuwezi Diamond. Unachotakiwa ni kuiponda tu. Ili uwe kwa Kiba pia jiaminishe kuwa kwa Dai hakuna cha maana. Kila kitu ni kuponda tu.

Mwisho utapata jibu kuwa hao ndo mashabiki wa Bongo. Ndo maana fedha kwa wasanii hazifunguki vyema kwa kukosa wateja wa kweli. Kwa kupenda vituko ndo maana Baba yake Diamond naye ana mashabiki. Ndivyo ilivyo kwa mama yake na kwa kina Gigy Money. Vituko vinawapa wafuasi.

Alikuwepo Sinta. Hakuwa mkali kihivyo wa kuigiza. Lakini alizalisha vituko na Bongo wakamkubali. Alitikisa nchi. Umaarufu kama mlima. Naye alikuwa kileleni kabisa. Kuna watu walifilisika kwa sababu yake. Ni huyo aliyemliza Juma Nature akaishia kujaza nyimbo zake kwenye albamu ya Ugali.

Hujawahi kuwaona Mona, Thea, Riyama na mastaa wengine wenye uwezo mzuri wa kuigiza katika kilele cha umaarufu? Kwa sababu wana tatizo la kutengeneza vibweka. Kiba na Dai? Kuna bifu la Juma Nature na Inspector Haroun. Sister P na Zay B, aliyeshauri wapatane aliwaharibia.

Hakuna aliyemuweza Dataz kati yao. Lakini Wabongo walipenda ‘bifu’ la Zay B na Sister P. Walipopatanishwa ikawa kwa heri. East Coast Team na TMK. Walikuwa katika sura ya ushindani wa Temeke na Upanga, siyo sanaa na ubora wake.

Choki, Muumini na Banza Stone. Baada ya kupatana dansi ikapoteza mzuka wake. Kuna Dudubaya na Mr Nice. Watu wakapuuza kipaji halisi cha Dully, Chilla, TID, Mad Ice na wenzao kisa bifu la Dudu na Nice. Hawakuwa na vipaji zaidi ya vituko na upuuzi. Lakini Wabongo wakadata nao.

Dai na Kiba siku wakirogwa wakapatana. Au wakagonga ngoma pamoja basi. Lazima mmoja atoweke kama kifaduro au wote tuwasahau. Na hapa ndipo alipocheza karata vyema Kiba, baada ya kulisusa ‘gemu’ na kurudi na ‘intavyuu’ ya kumnanga dogo kiaina.

Wakati Kiba akitangaza ujio wa ngoma ya mwana. Kama vile ndo anarudi upya akamchokonoa Dai. Kumbuka wakati huo Dai tayari ni staa. Alishashindanishwa na Mavoko, Belle 9 na Barnaba na akawafunika wote. Kiba akawa kama mkata kiu wa mashabiki wanaotamani Diamond apate mpinzani.

Kosa ni Diamond kukimbiza peke yake kwa muda mrefu. Kumbe watu wanatamani atokee mtu wa kumfanya kama mpinzani wake. Hapa wanaostahili pongezi ni uongozi wa sasa wa Kiba. Kutumia fursa ambayo wakali wengine kibao walishindwa kuitumia.

Unadhani Dai alikuwa kawakosea watu? Hapana. Ni Wabongo kama kawaida yao wanapenda kuona mtu hatulii kwenye kiti. Wanatamani vita ya maneno. Vituko, vijembe na kusutana. Ndo mashabiki wa muziki wa Bongo walivyo. Hata msanii awe mkali vipi atatafutiwa sababu.

Bongo ndo sehemu ambayo shabiki atamponda Q Chilla, Ray C au Afande Sele kuwa wamezeeka. Na wawapishe vijana. Lakini kwenye simu na ndinga zao wana ngoma mpya za Snoop Doggy, Jay Z, Koffi Olomide, Felix Wazekwa na Jennifer Lopez. Wabongo hatueleweki na tuna viroho vya kwa nini?

Sanaa inapoteza mwelekeo mbele ya vituko. Umbea na upuuzi umekuwa na nguvu kuliko kipaji cha Bishanga. Kuliko uigizaji wa Mzee Chillo. Yaani bifu, ngono, umbea na vituko ni zaidi ya sanaa ya Gabo. Tumechagua kuwa wapuuzi. Tumeamua kutengeneza mastaa wa vituko na siyo sanaa.

Umeshapata njia iendayo kwenye ustaa wa Bongo? Alamsik...

Chanzo: mwananchi.co.tz