Mila na desturi zetu zilikuwa zikihimiza, kabla ya vijana hawajaamua kuingia kwenye ndoa, ilikuwa ni lazima wazazi kufahamu familia ambayo kijana wao au binti yao anataka kuingia.
Wazazi wetu zamani hawakuwa wajinga walipokuwa wanachunguza familia ya mahali binti yao anapotaka kuolewa au kijana wao anapotaka kuoa. Walikuwa hawajui chochote kuhusu ‘saikolojia’, lakini walijua kwamba tabia mbaya au nzuri zinaweza zikatembea katika familia.
Wataalamu wamethibitiaha kwamba, familia ambazo wazazi ni walevi, au wavuta bangi, ni rahisi sana kuwarithisha watoto wao kuliko watu wanavyofikiria.
Baadhi ya tabia mbaya hujitokeza kwa watoto wakifikisha umri wa miaka 13 hadi 19, lakini wakati mwingine tabia hizo huweza kujitokeza ukubwani. Tabia huwa inaambukizwa bila hiyari ya mtu na kujikuta tu tayari anahiyo tabia kwa hiyo mzazi au wazazi wanapokuwa na tabia mbaya, watoto hudaka tabia hizo kwa haraka sana.
Katika jarida la Abnormal Child Psychology limebainisha kwamba, ni mara chache kukuta mtoto hajaathiriwa na tabia za wazazi wake ambazo hujitokeza sana katika familia.Mfano kati ya watoto watano wa wazazi walevi, anaweza kupona mtoto mmoja tu.
Awali watoto wanaweza kuzichukia, lakini baadaye ukubwani wakazitumia kwa sababu ndizo njia pekee wanazozijua katika kukabiliana na matatizo ya kimaisha.
Mwanamke: Hebu fikiria kwamba, umepata mchumba, handsome boy, ana fedha zake na amesoma madarasa ya kutosha. Anataka kuwa na uhusiano nawe, tena pengine uhusiano wa kudumu yaani kuoana. Je utaangalia tu uzuri, elimu na fedha zake au utakwenda mbali zaidi?
Mwanaume: hebu chukulia kwamba, umekutana na msichana, jicho-jicho, guu-guu, kalio-kalio na anajua mahaba, halafu amekubali kuwa rafiki yako, nawe umebabaika na anataka haraka sana muitwe mke na mume. Je unajitendea haki kuishia kwenye guu-guu tu au unapaswa kwenda mbali zaidi?
Familia anayotoka mtu ina mchango mkubwa sana kuhusiana na tabia za mtu huyo. Anaweza asioneshe tabia hizo wazi na hata akizionesha kwa kiasi fulani tunaweza kushindwa kujua kwamba, ni tabia ambazo hawezi kujiepusha nazo, kwani ni za familia kwa sababu hatujui familia yake.
Kwa hiyo badala ya kuishia kwenye guu-guu au jicho-jicho na kuishia kwenye u-handsome, elimu au fedha, inabidi twende mbali zaidi. Kama kweli tunataka kuwa na familia bora na imara, inabidi twende mbali zaidi tunaposema tumempenda fulani.
Usipoenda mbali utampata handsome ambaye amerithi kupiga mke, amerithi ulevi, amerithi ghubu na mengine yanayofanana na hayo.
Kwa kuwa umempenda utakaa kwenye ndoa ya mateso na vipigo, ambapo watoto wenu nao watakuwa ni wa kupiga wake au kupigwa na waume zao na kuwavumilia. Hapo mtakuwa mnaendeleza familia yenye matatizo.
Ni jambo la kusikitisha kukuta binti anajua vizuri familia ya mpenzi wake kwamba, baba wa mpenzi wake huwa anampiga sana mkewe, mbaya zaidi, inawezekana mmeshaanza kuona dalili za mkono mwepesi wa kupiga kwa huyu mpenzi wake. Lakini bado anang’ang’ania kuingia kwenye ndoa na mpenzi huyu mkorofi.
Ukweli ni kwamba ukienda kuoa kwa wapewa na watoa talaka, jiandae kwa kutoa au kupewa talaka. Huna haja ya kujidanganya kwamba, utaweza kubadili tabia hii kirahisi kama unayeoana naye anayo kutoka katika familia yake.
Ukweli mchungu, kula chuma hicho.