Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umesikia! Harmonize ndiye 'role model' wa Rayvanny

Harmonize Tz Tz Harmonize

Mon, 6 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ukitenga muda na kuchunguza kwa umakini, utabaini kuwa Rayvanny amekuwa akimtazama Harmonize kama mfano wa kuigwa (role model) kwake na hilo ndilo linafanya mashabiki kuona kama wanashindana ila sivyo, kuna mmoja anafuata nyayo za mwenzake!.

Wawili hao walitolewa kimuziki na WCB Wasafi miaka zaidi ya saba iliyopita na chini ya lebo hiyo walishirikiana katika wimbo mmoja tu, Paranawe uliotoka Desemba 2018.

Hata hivyo, hivi karibuni wamekuwa katika bifu na kutupiana maneno mtandaoni lakini hiyo haiondoi kweli kuwa Rayvanny amekuwa akiiga mambo mengi kwa Harmonize kama ifuatavyo;

Mosi; Januari 5, 2023 Harmonize aliachia video ya wimbo wake ‘Wewe’ ambayo Miss Dar City Centre 2005 na Mshiriki wa Big Brother Africa (BBA) 2013, Feza Kessy ametokeo, huku kukiwa na tetesi za wawili hao kuwa na uhusiano.

Kufika Januari 27, 2013 Rayvanny akaonekana studio kwake, Next Level Music (NLM) akiwa na Feza Kessy na siku iliyofuata wakaongozana pamoja kwenye hafla ya uzinduzi wa albamu ya Marioo, The Kid You Know pande za Mlimani City.

Pili; Wakati anaanza muziki Rayvanny alitambulika kama Raymond baadaye ndio ikaja hiyo Rayvanny, wakiwa wote bado wapo WCB Wasafi, Harmonize akaanza kujiita Konde Boy, haikuchukua muda Rayvanny naye akaja na Vanny Boy.

Basi Harmonize akaona isiwe kesi, akaamua kujiita ‘Tembo’ kama utambulisho wa ukubwa wa muziki wake, Rayvanny naye akapita mule mule na kujipachika jina la ‘Chui’.

Tatu; Oktoba 20, 2019 Harmonize alizindua Konde Boy Mgahawa, licha ya mradi huu kutofanikiwa, ulikuwa ni mpango wa kutoa chakula bora kwa watu ambao hawana uwezo ambapo utaratibu wake ulikuwa ni gari la Konde Boy Mgahawa kupita mtaani kila Jumapili.

Septemba 3, 2019 Rayvanny naye akatangaza kufungua mgahawa wake, Havanna, Dar es Salaam ikiwa ni biashara ya kwanza kubwa kwake ingawa kuna madai kuwa yeye sio mmiliki kwa asilimia 100.

Nne; Oktoba 2019 Harmonize alitangaza rasmi kufungua lebo yake, Konde Music Worldwide na ndani ya muda mfupi ikawasaini Ibraah, Anjella, Country Boy, Cheed, Killy na Young Skales wa Nigeria.

Ilipofika Machi 2021 Rayvanny akatangaza kufungua lebo yake, Next Level Music (NLM) na kumsaini Mac Voice ambaye uimbaji wake unashabiana na Ibraah ambaye ni wa kwanza kusainiwa Konde Music.

Tano; Februari 8, 2020 Harmonize aliachia video ya wimbo wake wenye mahadhi ya Singeli ‘Hajanikomoa’ na kutamba kuwa ndio video ya kwanza ya singeli kufikisha ‘views’ milioni 1 YouTube ndani ya wiki moja na hadi sasa imefikisha milioni 2.9.

Kufika Machi 29, 2020 Rayvanny akaachia video yake ya Singeli ‘Miss Buza’ na kutamba kuwa ndio video ya kwanza ya Singeli kufikisha ‘views’ milioni 1 YouTube ndani ya siku tatu na hadi sasa imefikisha milioni 11.

Sita; Mara baada ya kujitoa WCB Wasafi, Desemba 2019 Harmonize alienda kufanya shoo yake ya kwanza na ya bure nyumbani kwao, Mtwara na kufanyiwa tambiko kwa kupakwa damu ya ng’ombe.

Hata hivyo, haikuchukua zaidi ya wiki mbili, naye Rayvanny akafanya shoo nyumbani kwao, Mbeya katika tamasha alilolipa jina la ‘Home Coming’ ambalo lilikuwa halina viingilio pia!.

Saba; Machi 14, 2020 Harmonize aliachia albamu yake ya kwanza ‘Afro East’ ikiwa na nyimbo 18 na kuwa albamu ya pili iliyokuwa na nyimbo nyingi mwaka huo baada ya ‘Slave Become A King’ ya Darassa iliyotoka Desemba 24, 2020 ikiwa na nyimbo 21.

Februari 1, 2021 naye Rayvanny akaachia albamu yake ya kwanza ‘Sound From Africa’ ikiwa na nyimbo 23, hii ndio albamu pekee iliyotoka na nyimbo nyingi zaidi kwa mwaka huo.

Nane; Baada ya Harmonize kuachia ngoma yake ‘Attitude’ akimshirikisha Awilo Longomba aliamua kumleta nchini Tanzania msanii huyo wa DR Congo na kufanya video ya wimbo huo iliyotoka Aprili 23, 2021.

Rayvanny naye akamleta nchini msanii wa DR Congo, Innoss’B aliyemshirikisha kwenye ngoma yake ‘Makelebe’ ndipo wakafanya video ya wimbo huo iliyokuja kutoka Mei 14, 2021 ikiwa imepisha takribani wiki tatu na ile ya Harmonize.

Tisa; Februari 2022 Harmonize aliweka wazi uhusiano wake na Kajala Masanja, binti wa Kajala, Paula akawa karibu na Harmonize na wakawa wanaongozana wote watatu sehemu mbalimbali mjini, huku Konde Boy akiita hiyo ni familia yake.

Haikuchukua hata miezi miwili, Rayvanny akaanzisha uhusiano na Paula na huo ukawa mwanzo wa Harmonize kuachana na Kajala, Rayvanny akawa anamuita Kajala mama (mkwe) yake, tena anaweka na mbwembwe; eti Ma’ake Chui!,

Kumi; Oktoba 2019 Harmonize alidai kuwa alilipa Sh500 milioni kuvunja mkataba wake na WCB Wasafi ingawa baadaye alisema ni Sh600 milioni, fedha ambayo hakuwa nayo hadi kupelekea kuuza nyumba zake tatu!.

Januari 2023 anaibuka na kumshangaa Harmonize kulia kulipa Sh600 milioni, anadai yeye alilipa Sh1.3 bilioni ili kuondoa WCB Wasafi, fedha ambayo ni zaidi ya mara mbili ya ile aliyolipa Harmonize lakini hakuwahi kulalamika popote.

Chanzo: Mwanaspoti