Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

SIL

Ukiingia 'gesti' unaandika jina lako?

Hatari Za Watu Kuandika Majina Ya Uongo Gesti Ukiingia 'gesti' unaandika jina lako?

Tue, 16 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ukiingia ‘gesti’ huwa unaandika jina lako halisi? Swali hili lina akisi tabia ya wateja wengi wa nyumba za kulala wageni, ambao aghalabu huandika majina bandia kuandika katika vitabu vya wageni katika nyumba hizo.

Achana na hoteli ambazo kwa kawaida huwa na utaratibu unaolazimu kuchukua taarifa za mteja kabla ya kukabidhiwa funguo za chumba, wakati mwingine hadi kitambulisho kinahitajika, hapa nazungumzia ‘gesti’ na ‘loji’ yaani nyumba za kulala wageni.

Taarifa zilizokusanywa na Mwananchi Digital kutoka kwa wamiliki, wahudumu na wateja wa nyumba hizo, kuna uwezekano kwamba wateja wengi huandika majina ambayo si halisi na wengine hawaandiki kabisa, jambo linaloikosesha Serikali mapato.

Kulingana na wateja hao, shughuli inayompeleka gesti ndiyo itakayoamua aandike jina lake halisi, la uongo au asiandike kabisa.

Wahudumu nao wanasema wamekatazwa na mabosi zao kuhoji taarifa za mteja, wanachopaswa kufanya ni kumpa daftari na kumwacha aandike, ili asiamue vinginevyo.

Hata hivyo, kuna ukimya wa kisheria kuhusu mteja wa nyumba hizo anayedanganya jina, isipokuwa inamlazimu muhudumu kuhakikisha anamwandikisha bila kujali alichoandika ni halisia au kadanganya.

“Kila muhudumu wa hoteli anapaswa kuweka kitabu cha wageni katika hoteli yake kitakachotumika kuandika majina na anwani ya kila mgeni anayepanga katika hoteli hiyo, na taarifa nyingine zitakazohitajika,” inaeleza Ibara ya 18 ya Sheria ya Hoteli sura ya 105.

‘Kuandika inategema umefuata nini’

Uamuzi wa kuandika jina au kutoandika, unategemea na gesti uliyoingia na ulichokwenda kufanya katika nyumba hiyo, kama inavyoelezwa na Benson Mlacha, mmoja wa wateja wa nyumba hizo jijini Dar es Salaam.

“Kwani wao wanataka hela au wanataka kukubana, mara nyingi wao wanaangalia hela tu hawana muda wa kukulazimisha uandike jina,” amesema.

Mtazamo huo unashabihiana na ule wa Nickson Bidodi anayesema shughuli iliyompeleka kwenye nyumba hiyo ndiyo itakayoamua aandike jina halisi au la uongo.

“Kama nimekwenda kwa maovu, mfano nipo na mwanamke asiye mke wangu huwa naandika jina la uongo. Lakini kama nipo mikoani kikazi huwa naandika jina halisia ili lolote likitokea nipatikane,” amesema.

Ameeleza hakuwahi kuhojiwa chochote na muhudumu wa gesti na zaidi anapofika huwa anapewa daftari kwa ajili ya kuandika jina na hakuna anayemsimamia kulifanya hilo.

Katika daftari hilo, amesema anachoandika ni jina lake na baadhi ya taarifa kama siku unayoingia, utakayotoka, unapokwenda na namba yako ya simu.

Hata hivyo, umeonekana ugumu wa kubaini uhalisia wa jina la mteja kwa kuwa anapofika katika nyumba hiyo, hakuna anayemjua.

Kulingana na mmoja wa wamiliki wa nyumba hizo, Ahmidiwe Mmari, haitakuwa kazi rahisi kutambua hilo kwa kuwa  kama anaandika jina la uongo au ukweli hutajua kwa sababu anakuja mgeni humjui anapotokea. Kujua jina lake inabidi muwe mnafahamiana kabla,” amesema.

Mteja mwingine wa nyumba hizo (jina lake limehifadhiwa), amesema kila anapofika huwa anaandika jina lake halisi, akihofu kutotambulika iwapo atapatwa na madhira yoyote ikiwemo kuuawa.

Mmoja wa wahudumu katika nyumba ya kulala wageni mkoani Mtwara, amesema kwanza bosi wake amewakataza wahudumu kumchunguza mteja.

“Haturuhusiwi hata kumuuliza kuhusu kile anachokiandika, yeye akiandika taarifa zake basi anapewa huduma nyingine anazostahili, haturuhusiwi kuchunguza sio jukumu letu,” amesema.

Alipoulizwa iwapo yupo mwenye jukumu hilo ndani ya nyumbani hiyo, amesema hakuna isipokuwa kinachoandikwa na mteja ndiyo hicho hicho kinachohifadhiwa.

Muhudumu mwingine katika moja ya nyumba hizo jijini Dar es Salaam, Mariam Malima amesema wateja wenyewe ndiyo wanaokataa kuandika, akifafanua wengi hawataki ijulikane kama waliingia gesti.

“Unakuta ni mume wa mtu amekuja gesti na mwanamke mwingine, hawezi kutaka aandikwe jina. Analipia anakwambia jina hapana we utaandika unavyojua. Kwa kuwa bosi anataka hela unampokea,” amesema.

Hotelini hutoboi

Mchezo huo si rahisi kuucheza katika hoteli zenye hadhi ya nyota tano, kama inavyosimuliwa na Maselina Rweyemamu, muhudumu katika moja ya hoteli hizo jijini Dar es Salaam.

Amesema taarifa za mteja ni moja ya vitu vinavyozingatiwa katika hoteli na  ni bora kumkosa kuliko kuruhusu aingie bila kuacha vielelezo vyake.

Kulingana na Maselina, kwa wateja wanaotoka nje ya nchi hutakiwa kutoa pasi ya kusafiria, ambayo kimsingi huwa na majina yake kamili, kisha anajisajili.

Kwa wale wa nchini, ameeleza pamoja na taarifa nyingine muhimu lazima waache kitambulisho ama cha uraia, kupiga kura au leseni ya udereva na kisha anaandikishwa ndiyo apatiwe huduma.

“Hilo linafanyika hata kwa mgeni wa mteja, kwa mfano mteja kaingia na vielelezo vyote kakamilisha, baadaye amekuja mgeni wake, hataruhusiwa kuingia hadi kwanza ithibitike ni mgeni wa nani, pia atatakiwa kuacha kitambulisho chake mapokezi hadi atakapotoka ndiyo atapewa,” amesema.

Hayo yote, amesema yanafanyika kudhibiti uhalifu na matukio mengine mabaya katika hoteli.

Mtazamo wa kisheria

Ingawa huduma za nyumba za kulala wageni husimamiwa na sheria ndogondogo zinazotungwa na halmashauri ilipo nyumba husika, Wakili Jebra Kambole amesema ipo Sheria ya Hotel sura ya 105 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2006, inayotoa mwongozo wa huduma hizo.

Ibara ya 18 ya sheria hiyo, inawalazimu wahudumu wa hoteli kuhakikisha wanaweka rejista itakayotumika kuandika majina ya wateja watakaolala katika nyumba hiyo na maelezo mengine yatakayohitajika.

Kulingana na kifungu hicho, kutakuwa na kitabu kitakachowekwa katika hoteli husika kwa ajili ya kuandikia majina hayo kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 15 cha Sheria ya Vileo.

Kifungu hicho cha 15 (2) cha Sheria ya Vileo ya mwaka 1968, kinasema mmiliki wa leseni ya hoteli anapaswa kuweka kitabu cha wageni katika nyumba hiyo, na kumlazimu kila mteja kuandika jina na anwani yake mara tu anapoingia.

Kumbe mapato yanapotea!

Kitendo cha kutoandika jina kwa namna nyingine ni hasara kwa Serikali, hupoteza kinapoteza mapato yaliyopaswa kuingia katika halmashauri ilipo nyumba ya kulala wageni.

Kifungu cha 26 (2) cha sheria hiyo ya hoteli, kinamtaka mmiliki kulipa asilimia 20 ya jumla ya mapato yanayotokana na malipo ya wateja wanaolala kwenye nyumba husika kwa kila mwezi.

Ushuru huo kwa mujibu wa sheria hiyo, unapaswa kulipwa kuanzia tarehe 1 hadi 7 ya kila mwezi.

Kitabu cha wageni katika nyumba hiyo ndicho kitakachotumika kujua idadi ya wateja waliolala na kiwango cha ushuru kitakachopaswa kutozwa. Hii ni kwa wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni ambazo hawajasajiliwa kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Kinyume na kutekeleza hilo, sheria hiyo inaweka wazi kuwa asilimia 25 itatozwa kwa nyumba husika iwapo itabainika imechelewa kulipa ushuru zaidi ya siku saba, kwa mujibu wa ibara ya 32(a).

Lakini ukidanganya mapato na kutokuwa na kitabu cha kumbukumbu itakulazimu ulipe faini ya Sh500,000, huku atakayebainika kutolipa ushuru tangu hoteli ilipoanzishwa atatozwa faini ya Sh2 milioni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live