Msanii Mkongwe Bongo katika muziki wa hip hop, Professor Jay amesema wasanii wa zamani bado mchango na muziki wao vinahitajika kwa sana kinachotakiwa ni wao kujipanga na kurudi upya.
Jay ambaye hivi karibuni ameachia ngoma inayokwenda kwa jina Pagamisa ameiambia Clouds TV yeye amekuwa akifanya muziki toka 1995 akiwa na kundi na hadi sasa anatoa ngoma na watu wanazipokea.
“Lakini niwaambie wasanii wa zamani watu bado wananaheshimu, wamekuwa kama wamechonga barabara ambapo wasanii wa sasa wamepata mifano kwao, hii ni game wasikate tamaa, watu bado wanawamisi, bado wanapenda nyimbo zao, watu wanapenda mashairi yao,” amesema Professor Jay.
“Nimeshakuwa na kundi langu la Hard Blaster mabingwa wa Tanzania mwaka 1995 wasanii wengi wa sasa hivi ndio walikuwa wanazaliwa lakini hadi sasa natoa ngoma kutokana na mazingira yaliyopo na watu wananipokea vizuri,” ameongeza.
Tangu Professor Jay kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mikumi amekuwa si msanii wa kutoa ngoma mara kwa mara ukilinganisha na hapo awali, ngoma alizotoa hivi karibuni ni pamoja na Kibabe na mpya ya sasa.