LISHE bora ni msingi wa uhai, ukuaji na maendeleo ya binadamu kimwili na kiakili. Lishe huongeza uwezo wa mtu kufanya kazi hivyo huchangia katika kuongeza tija kwa shughuli za uzalishaji mali kwa kaya na taifa kwa ujumla.
Umuhimu wa lishe katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi umepewa kipaumbele na kuwekewa mikakati ya utekelezaji katika malengo ya maandiko mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Miongoni mwa malengo hayo ni ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030, Malengo ya Baraza la Afya Duniani ya mwaka 2025, Ajenda ya Afrika ya mwaka 2063 pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.
HALI YA LISHE ILIVYO
Takwimu zinaonesha kuwa hali ya lishe nchini inazidi kuimarika kutokana na kupungua kwa kiwango cha utapiamlo kwa baadhi ya viashiria.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFCN), Dk Germana Leyna anasema kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano ambao ni kiashiria kikuu cha utapiamlo kimepungua kutoka asilimia 34.7 mwaka 2014 hadi asilimia 31.8 mwaka 2018.
Dk Leyna anasema licha ya kupungua huko lakini kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 1995 kiwango bado kinaashiria hali mbaya ya lishe nchini na inakadiriwa kuwa kuna kiwango cha watoto zaidi ya milioni tatu waliodumaa. “Idadi kubwa ya watoto iko katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Mara, Dodoma, Geita, Tanga, Ruvuma, Mbeya, Morogoro na Tabora.
Anasema kiwango cha ukondefu kimepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2014 hadi asilimia 3.5 mwaka 2018 lakini pamoja na kupungua kwa kiwango hicho bado kuna watoto 600,000 wana utapiamlo mkali na wa kadiri.
“Tatizo la uzito pungufu limeongezeka kutoka asilimia 13.4 mwaka 2014 hadi asilimia 14.6 mwaka 2018. Aidha kwa watu wazima tatizo la upungufu wa damu miongoni mwa wanawake walio katika umri wa uzazi miaka 15-49 limepungua kutoka asilimia 44.8 hadi asilimia 28.8,” anasema.
Kuhusu tatizo la uzito uliokithiri kwa wanawake walio katika umri wa kuzaa, Dk Leyna anasema limeongezeka kutoka asilimia 29.7 mwaka 2014 hadi asilimia 31.7 mwaka 2018. Mikoa inayoongoza ni Kilimanjaro, Arusha, Mbeya na Unguja, Mjini Magharibi.
“Uzito uliokithiri ni chanzo kikuu cha magonjwa sugu yasiyoambukiza yanayosababishwa na ulaji duni pamoja na mtindo mbaya wa maisha japokuwa tunajitahidi kupunguza tatizo la udumavu na utapiamlo kuna tatizo hilo la ongezeko la uzito uliokithiri na kiribatumbo.
Anaongeza: “Tatizo hilo ni chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza kama vile saratani, kisukari, magonjwa ya moyo, figo na mengine.
JITIHADA ZA SERIKALI
Dk Leyna anaeleza kuwa ili kukabiliana na matatizo hayo serikali imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuboresha hali ya lishe ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya, uongezwaji wa madini joto kwenye chumvi, kutoa virutubisho vya nyongeza kwa makundi maalumu.
“Makundi hayo yanahusisha wajawazito pamoja na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.“Jitihada zingine ni kuhimiza kanuni za ulishaji sahihi kwa watoto wadogo na wachanga, kutoa chakula na dawa kwa ajili ya kuwatibu watoto wenye utapiamlo na wa kadiri pamoja na kuanzisha siku maalumu kuadhimisha mafanikio ya jitihada zinazoendelea,” anabainisha.
Anasema pia wanahamasisha umma kwa kutoa elimu kuhusu faida ya lishe bora na athari za utapiamlo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
LENGO LA MAADHIMISHO
Siku ya Lishe Duniani huadhimishwa kila Oktoba 23 lengo ikiwa ni kuwaleta pamoja wadau wa lishe ambao ni viongozi, wanasiasa, watendaji, wataalamu, wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi.
Dk Leyna anasema sababu ya kufanya hivyo ni kusaidia kuongeza ufahamu kuhusu umuhimu wa lishe kama msingi wa afya bora na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Anasema kaulimbiu katika maadhimisho hayo ni “Lishe Bora Kinga Thabiti dhidi ya Magonjwa: Kula Mlo Kamili, Fanya Mazoezi, Kazi Iendelee”. “Maadhimisho ya siku hii yanatanguliwa na wiki ya maonesho ya shughuli mbalimbali za afya na lishe na shughuli zilizokuwepo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu utayarishaji mlo kamili kwa makundi kama watoto, vijana, wajawazito na wanawake wanaonyonyesha.
Anasema shughuli zingine wanazofanya ni maonesho ya utayarishaji na maandalizi ya mlo kamili kwa kutumia vyakula vinavyopatikana katika maeneo husika ambavyo vingi ni vya asili. “Tunafanya uchunguzi wa afya na hali ya lishe kwa watu wote pamoja na kutoa ushauri stahiki, maenesho ya bidhaa ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi kutoka shambani au kiwandani (Bio-fortifield and Industriy fortifield).
“Pia vipindi vya redio na runinga zilizopo katika maeneo yao kuhamasisha jamii kula mlo kamili kwa kuzingatia vyakula vinavyopatikana katika maeneo yao pamoja na kuwa na mtindo bora wa maisha,” anafafanua.
CHAKULA BORA NI KIPI?
Kwa mujibu wa Ofisa Lishe Mtafiti, Adeline Munuo, chakula bora ni kile kinachoupatia mwili virutubishi vyote muhimu katika uwiano sahihi kulingana na mahitaji ya mwili.
Munuo anasema ili chakula kiwe bora sifa zinazotakiwa ni pamoja na kuwa na mchanganyiko wa vyakula kutoka makundi tofauti ya vyakula kama yenye asili ya nafaka, mizizi na ndizi mbichi, mchele, mtama, ulezi, ndizi za kupika, mihogo, viazi na magimbi.
“Mchanganyiko mwingine ni wenye asili ya wanyama, vyakula vya baharini, wadudu wanaoliwa, jamii ya mikunde pamoja na mbogamboga na matunda aina zote.
Anasema chakula kinatakiwa kuandaliwa na kupikwa katika mazingira safi na salama kwa muda sahihi ili kuzuia upotevu wa baadhi ya virutubishi.
“Muda gani tunakula ni sehemu muhimu ya mtindo sahihi wa maisha ili kuwa na afya njema. Kuzingatia muda wa kula kuna faida nyingi kiafya ikiwa ni pamoja na kuwa na uzito sahihi na kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Anabainisha kwa kutozingatia muda wa kula ni moja ya sababu zinazochangia mtu kutokuwa na afya bora kwani husababisha ulaji wa chakula kingi kuzidi mahitaji ya mwili.
Aidha, anasema mtu anayekula usiku muda mfupi kabla ya kulala hujiweka katika hatari ya kuongezeka uzito kwa sababu mwili unakuwa katika hali ya mapumziko hivyo hushindwa kumeng’enya chakula ipasavyo.
“Matokeo yake chakula hubadilishwa kwenda kwenye mafuta na kuhifadhiwa hivyo kuongeza uzito pia, usiku ni muda ambao mwili hufanya kazi nyingine ikiwemo kutengeneza seli zilizoharibika.
Anafafanua kuwa ni muhimu kula chakula mchanganyiko kutoka makundi tofauti tofauti ya vyakula kwa kutegemeana na umri, jinsia, aina ya kazi na hali ya kifiziolojia ya mwili.
“Kula matunda na mbogamboga kwa wingi kila siku ili kuimarisha mfumo wa kinga mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali,” anashauri. Anasema ni muhimu kuongeza ulaji wa vyakula vyenye makapi-mlo kwa wingi kama nafaka zisizokobolewa, mbogamboga ili kuwezesha mfumo wa chakula kufanya kazi kwa ufanisi.
“Punguza matumizi ya vyakula vyenye mafuta mengi ili kupunguza uwezekano wa kuongezeka uzito, kupata maradhi. “Punguza matumizi ya sukari na vyakula vyenye sukari nyingi kwani huongeza nishati lishe mwilini na hivyo kuchangia ongezeko la uzito wa mwili,” anaeleza Munuo.