Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uhasama wa Harmonize na Diamond Wafika Pabaya

Mondi Harmo Harmonize na Diamond

Wed, 22 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MSANII Harmonize au Harmo aliachana na Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) miaka miwili iliyopita na kuibua uhasama, lakini mwaka huu uhasama huo umefika pabaya baada ya kufichua siri kubwa kwamba utawala wa WCB ulimtaka alipe shilingi milioni 600 ili kuvunja mkataba.

Hali ilizidi kuwa mbaya mwezi uliopita na kusababisha mjadala mzito kwa wasanii hasa mashabiki wa Bongo Fleva hivyo kuufunga mwaka huu wa 2021 kwa uhasama mkubwa kuwahi kutokea.

Harmonize ambaye anamiliki Lebo ya Konde Gang na Diamond anayemiliki WCB, wamekuwa kwenye mgogoro tangu walipoacha kufanya kazi pamoja huku wafuasi wao wakitoleana maneno makali kwenye mitandao ya kijamii.

Lakini, katika kile kilichoonekana ni Harmonize kushindwa kujizuia, alijikuta akifichua mchakato mzima, akidai kufanyiwa mambo yasiyofaa, ikiwemo kulipishwa shilingi milioni 600 kama faini ya kuvunja mkataba wake wa miaka 10 na WCB ambao ndiyo walimtambulisha kwenye muziki.

Katika harakati za kuvunja mkataba na WCB, Harmonize alidai alilazimika kumtumia Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Pombe Magufuli na viongozi kadhaa, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Juhudi za kumpata Dk Mwakayembe kuzungumzia namna alivyoshughulikia sakata hilo ziligonga mwamba, kwani alipopigiwa simu alisema yupo kwenye mkutano na kutaka apigiwe baadaye, lakini alipopigiwa tena simu iliita bila kupokelewa.

Hata alipotumiwa maswali kupitia ujumbe mfupi wa maandishi hakujibu. Harmonize alifafanua kwamba kwamba ilibidi auze nyumba zake tatu ili apate pesa za kuwalipa WCB!

Alisema alihaha kupata pesa hizo akitaja kampuni mbili kubwa kwamba ndizo zilimpa pesa kukamilisha shilingi milioni 500. Hata hivyo, akatakiwa aongeze shilingi milioni 100, alipewa na meneja wake, Sebastian Ndege au Jembe ni Jembe.

Harmonize alisema aliuza nyumba yake ambayo haikuwa imekamilika kwa shilingi milioni 100 kisha kampuni ya vinywaji ikampa shilingi milioni 200, halafu CRDB wakampa shilingi milioni 200 na meneja wake akampa shilingi milioni 100.

Lakini kuna watu wanasema Harmonize alidanganya; kuna mahali hakusema ukweli. Hata hivyo, upo ukweli kwamba Harmonize alilipa shilingi milioni 500 japokuwa hilo deni WCB hawajawahi kukanusha.

Mwaka 2019, Harmonize alisema aliwalipa WCB shilingi milioni 500, lakini mwaka huu, alisema alizolipa ni shilingi milioni 600, jambo lililoibua mkanganyiko.

Swali la wengi ni kwamba, kwa nini Harmonize na Diamond waligombana? Jibu ni vipengele vya mkataba (contractual terms). Kuna mkataba wenye utashi wa pande zote zenye kusaini.

Mwaka 2015, Harmonize alikuwa kijana mdogo, asiye na pesa, lakini alikuwa na ndoto ya kuwa mwanamuziki mkubwa.

Diamond ni staa aliyekaa juu kimuziki ndani na nje ya nchi na mwaka 2015, Harmonize hakuwa akijua chochote, alimwona kama Mlima Kilimanjaro. Harmonize alipoambiwa na Diamond asaini mkataba, bila shaka alisaini akiwa na furaha iliyopitiliza.

Mwaka 2015, akatoa Aiyola, jamii ikamjua. Mwaka 2016 akatoa Matatizo, akaanza kuona mwanga wa muziki.

Mkataba ni makubaliano ya kisheria na asili ya mikataba ya muziki ni wajibu wa kila upande. Unachotoa na unachoingiza. Masharti lazima yawe sawa kuhusu mzigo ambao kila upande utabeba kwa kuvunja mkataba.

Wasanii wengi chipukizi wanapochukuliwa na mastaa wakubwa, hudhani wanasaidiwa hivyo hunyenyekea na kusaini kiholela bila kujua kwa undani kilichomo ndani.

Kampuni za kurekodi muziki hutaka kummiliki msanii kwa muda mrefu ili ifaidike kwa kupata faida hasa kama msanii huyo ni mzuri.

Kama mkataba wa Harmonize na WBC ungekuwa wazi bila shaka wasingeingia kwenye mgogoro na wangeachana salama.

Lakini ugomvi huo umekuwa na faida kwa wasanii wengine kwamba sasa wawe makini, wasaini kwa miaka michache na itaje nyimbo ngapi ataingia nao mkataba.

Hata hivyo, mwaka 2021 unatajwa kuwa mwaka mzuri kwa Harmonize na Diamond, lakini wameufunga kwa uhasama mkubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live