Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCHOKOZI WA EDO: Mmakonde na mlinda amani katika urafiki wa korosho

27816 Pic+edoTanzaniaWeb

Tue, 20 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Natabasamu. Najaribu kukumbuka jinsi maisha yanavyokwenda kasi sana pengine kuliko unavyoweza kufikiria. Sasa tupo mwaka 2018. Miezi 36 iliyopita ulikuwa mwaka 2015. Kule kwa Wamakonde ilikuwa hadithi tofauti.

Jemedari wa wakati ule alikumbana na wakati mgumu kutoka kwa Wamakonde. Kisa? Walikuwa wamechachamaa hawataki gesi itolewe Kusini ipelekwe Dar es Salaam. Inawezekana walikuwa sahihi au hawakuwa sahihi.

Huwezi kubishana na Serikali. Kilichoendelea wanakijua. Mwishowe kabisa Wamakonde walisalimu amri, wakanyoosha mikono gesi ikaruhusiwa kutoka. Ni matukio ambayo hayatasahulika.

Haikuwa kazi rahisi kwa Serikali kwa sababu Wamakonde walikuwa wamedhamiria kwelikweli kuhakikisha haitoki. Wenyewe walikuwa wana usemi wao. Mtu mmoja anauliza “Gesi?” halafu wengine wanajibu “Haitokiii”.

Baada ya walinda amani kwenda kule na kuimarisha amani ikawa mtu mmoja akiuliza “Gesi?” wenzake wanajibu “Inatokaaaa”.

Leo watu walewale waliokuwa wanahakikisha gesi inatoka ndo wanahakikisha kwamba mkulima wa Kimakonde anapata maisha mazuri na ya raha kwa korosho zake kununuliwa. Maisha yanaenda kasi.

Miaka mitatu nyuma alikwenda kulinda amani na usalama miaka mitatu baadaye anakwenda na fedha. Shukrani kubwa kwa Anko Magu. Maisha yapo kasi sana.

Hakuna ubaya wa mtu aliyekuwa na sura yenye mikunjo akirudi na sura yenye tabasamu. Inaonyesha mabadiliko ya nyakati na misimamo.

Kitu cha muhimu ni kumshukuru Mungu na kukumbuka jinsi gani anatupa pumzi za kushuhudia mabadiliko ya nyakati na dhamira.

Kuna mtu anaweza kujiuliza, mbona leo Edo haeleweki? Inawezekana kweli sieleweki lakini jibu la msingi ni kwamba tuitazame kesho.

Watawala wajue kwamba kuna kesho. Watawala wajue kwamba kitu cha msingi ni meza za majadiliano.

Leo mtu mmoja amekwenda na wema lakini nyuma ndugu yake alikwenda bila kutaka majadiliano.

Ni watu walewale, kutoka katika familia ileile ambayo inaamini kwenye misingi ileile. Mungu ibariki Tanzania.



Chanzo: mwananchi.co.tz