Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCHOKOZI WA EDO: Dada Jokate kaanza na mguu mzuri

27903 Uchokozi+pic TanzaniaWeb

Tue, 20 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Maisha rahisi kwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Dada Jokate Mwegelo. Ana wafuasi 3.5 milioni katika mtandao wake wa Instagram. Kabla ya kibarua hiki cha kisiasa aliwahi kuwa staa nchini.

Sasa anaendelea kung’arisha nyota tu. Kazi yake ya kung’arisha nyota ni rahisi. Anachofanya ni kutupia tu mitandaoni kazi zake anazofanya Kisarawe.

Watu 3.5 milioni mimi nikiwa mmojawapo zinatufikia. Mtandao wake umegeuka kama kituo cha televisheni. Tunajua anachofanya kila alipo.

Kazi kubwa ipo kwa wale ndugu zangu wengine ambao wanalazimika kutumia nguvu nyingi kwa ajili ya kujulikana walipo au wanachokifanya.

Baadhi ya hawa huwa wanafanya kazi kubwa ya kuchokonoa mambo ili tuanze kusambaziana kazi zao katika makundi ya Whatsapp.

Hawa ndio wale wanaofokea watumishi hadharani na kuwatia ndani kwa mbwembwe nyingi. Baadaye tunasambaza video zao katika makundi ya Whatsapp huku tukiwashangaa.

Hawajali sana kama jamii inawaonaje, wao wanachojali ni kuendelea kupata umaarufu kirahirahisi.

Kuna vimbwanga kwelikweli nchi hii. Wakati mwingine anayewapa presha hii bila ya kujijua ni Namba moja mwenyewe. Wote wanataka waonekane wanafanya kazi.

Wote wanataka kuiga staili yake ya utawala. Kumbe kuna yeye mmoja tu. Yupo kama alivyo. Ukimuiga unaonekana unaigiza, unabakia kuchekesha na kukorofishana na jamii ambayo utakutana nayo muda wowote baada ya kutumbuliwa.

Huyu Dada Jokate hajawahi kumfokea mtumishi wala kuamuru polisi imtie ndani mtendaji. Nadhani hataki ‘kiki’ za namna hii. Kitu cha msingi ni kwamba anapata muda wa hewani kupitia Instagram, basi. Watu milioni 3.5 si mchezo.

Aendelee tu kufanya kazi kwa staili hii hii ili mradi habari zake tunazipata kupitia mitandao yake. Ana mwanzo mwema na amewakilisha vizuri vijana wachache ambao wanaweza kuongoza bila ya kiki, kufokafoka, kutukana wazee, kudhalilisha watumishi kupitia polisi na mengine mengi ambayo huwa tunasambaziana kila siku katika makundi yetu ya Whatsapp.

Kuna maisha ya vyeo. Wengine wataishia pabaya. Inatabirika.



Chanzo: mwananchi.co.tz