Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Tyson alivyolaaniwa na kubarikiwa

Mike Tyson Fall X Rise Tyson alivyolaaniwa na kubarikiwa

Thu, 14 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ni kweli nimefilisika, lakini nina maisha mazuri, nina mke mzuri ambaye ananijali, sina kitu kwa sasa lakini huko nyuma nilifanya starehe sana, kufilisika kumetokea tu, nina furaha. Najua sistahili kuwa na mke wala watoto nilionao lakini nipo nao, hiki ndicho kinachonipa furaha kwa sasa.”

Ndiyo. Hayo yalikuwa ni maneno ya bondia raia wa Marekani, Mike Tyson ambaye mwaka 2003 alitangazwa amefilisika na kuwa na deni la zaidi ya Dola 23 milioni.

Ilikuwa ni kipindi ambacho alifilisika baada ya kuishi maisha ya kifahari kabla ya baadae kuja kupata ahueni kupitia kazi mbalimbali alizofanya ikiwemo uigizaji.

Tyson ni mmoja kati ya mabondia waliofanya vizuri sana duniani miaka ya 1980. Katika miaka hiyo alikuwa mmoja kati ya wanamichezo wanaopokea pesa nyingi duniani. Alianza kupata pesa na umaarufu akiwa na umri wa miaka 20 tu, alipewa majina mengi ya kusifiwa, ikiwa pamoja na mpiganaji bora zaidi kuwahi kutokea kwenye ulingo wa ngumu za kulipwa.

Hapa tunaangalia jinsi alivyokuwa akitumia pesa na kuponda raha hadi akafikia hatua ya kufilisika, kisha baadae kurudi kwenye zama za utajiri ingawa sio kwa kiwango cha hapo awali.

ALIVYOPONDA MALI

Aliishi maisha ya kifahari, alitumia pesa nyingi kwenye kununua majumba ya kifahari, magari, vito na kutoa zawadi kwa wageni na alifikia hatua ya kimiliki hadi duma aliokuwa anawafuga kama mbwa.

Mtu ambaye alikuwa akiwahudumia alikuwa akimlipa Dola 125,000 kwa mwaka.

Alikuwa anamlipa mtu mmoja Dola 300,000 kwa mwaka na kazi yake ilikuwa ni kupiga makelele wakati Tyson anafanya mkutano na waandishi wa habari kuelekea pambano lolote.

Kwenye mapito yake aliwahi kufungwa jela mwaka 1991 hadi 1995 kwa kesi ya unyanyasaji wa kijinsia baada ya kutolewa kwa mujibu wa tovuti mbal mbali, staa huyu aliendelea na maisha yake ya kuponda raha na alitumia zaidi ya Dola 50 milioni kununua vitu mbalimbali.

Alitumia Dola 4.5 milioni kununua magari na pikipiki kwa ajili ya rafiki zake, jumla ya vitu hivyo vilikuwa ni 19.

Alinunua njiwa na duma kwa Dola 400,000, akatumia tena Dola 300,000 kwenye kutengeneza bustani kwenye nyumba zake zote alizokuwa akiishi.

Kiasi cha Dola 240,000 alikuwa akikitumia kama pesa zake za matumizi yake ya kila siku kwenye vinywaji na chakula ama kuwapa watu.

Alitumia Dola 230,000 kwenye kununua simu mpya pamoja na vocha na bili nyingine zinazohusu mawasiliano na alikuwa akihudumia na watu wanaomzunguka pia kwenye sekta hiyo.

Kwa mwaka alitumia Dola 125,000 kwa ajili ya kumlipa mkufunzi wa kuwafundisha duma wake masuala mbalimbali ukiondoa yule jamaa aliyekuwa anawaangalia na kuwahudumia kila siku.

Kwa mwezi alitumia Dola 100,000 kununua mavazi na vito vya madini mbalimbali.

Alikuwa ana nyumba sehemu nyingi Marekani ikiwemo ule mjengo wake ambao baadae ulinunuliwa na msanii 50 Cent, uliopo huko Connecticut.

Nyumba hiyo ilikuwa na baa na sehemu ya kuchezea kamari za aina mbalimbali, ndani yake pia ulikuwa na vyumba 21.

Pia aliwahi kununua nyumba huko Las Vegas, Ohio na Maryland. Mjengo wake wa Ohio ulikuwa na bwawa la kuogelea, pool na kiwanja cha kuchezea.

Nyumba yake ya Las Vegas aliyoinunua Dola 4 milioni ina ukubwa wa eneo la futi 11,000.

Mike alikuwa amemiliki zaidi ya magari 100 wakati maisha yamemfungukia kabla hajafilisika, tena magari hayo yalikuwa ni yale yenye thamani kubwa, mojawapo ilikuwa ni Bentley ambayo wakati anainunua ilikuwa zilikuwa zimetengenezwa 73 tu dunia nzima na alitoa Dola 500,000.

Mwaka 1995 baada ya kwenda kubadilisha oili kwenye gari yake aina ya Range Rover alimwambia fundi aliyefanya kazi hiyo alichukue tu kwani yeye halitaki tena.

Taarifa zinadai kuna muda alikuwa anawaazima marafiki zake magari kisha akasahau kabisa kama aliazimisha.

Aliwahi kununua magari 20 kwenye moja ya yadi ya magari huko Las Vegas kwa muda mmoja na taarifa zinaeleza alitumia Dola 1.5 milioni kufanikisha zoezi hilo.

Alinunua magari matano aina ya Bentley Azures na kwenye yadi hiyo yalikuwepo mawili tu, hivyo mmiliki akaagiza mengine matatu haraka ili afanye biashara.

Moja kati ya vitu vya thamani alivyowahi kununua bondia huyu ilikuwa ni beseni la dhababu alilonunua kwa Dola 2 milioni kumnunulia mkewe wa kwanza Robin Givens.

Kwa mujibu wa watu wake wa karibu, alikuwa akidiriki kununulia watu aliokutana nao dukani tu ambao hakuwa anawafahamu zawadi za bei ghali kama saa zilizokuwa na thamani ya Dola 100,000.

Baada ya kuponda raha kwa kiasi kikubwa bila ya kuwekeza popote akitegemea pesa alizokuwa anapata kutoka sehemu mbalimbali ikiwa pamoja na nje ya ulingo, Tyson akajikuta amefilisika hususani baada ya umri kumtupa mkono na kutokuwa anapigana tena.

Wakati anapigana pambano lililowahi kumpa pesa nyingi zaidi lilikuwa ni lile dhidi ya Lennox Lewis na anadaiwa kupata zaidi ya Dola 140 milioni (zaidi ya Sh300 bilioni).

Hata hivyo, hakukata tamaa ndio akaanza kujitafuta kwa kuigiza na kufanya madili mengine hadi akarudisha walau theluthi ya utajiri wake.

Kabla ya kufilisika alikadiriwa kuwa na utajiri wa zaidi ya Dola 400 milioni lakini kwa sasa ana utajiri wa Dola 10 milioni.

ALIVYOACHWA NA MKEWE

Baada ya kutangazwa amefilisika mwaka 2003, aliyekuwa mkewe Monica Turner ambaye alifunga naye ndoa mwaka 1997 aliachana naye na moja ya sababu zinazotajwa kuwatenganisha wawili hao ilikuwa ni kufilisika kwa Tyson.

Bingwa huyu alikaa hadi mwaka 2009 na hali yake ya kiuchumi kidogo ilitengamaa ndio akamuoa Lakiha Spicer anayeishi naye hadi sasa.

Hadi sasa Tyson ana watoto sita aliozaa na wanawake watatu tofauti ikiwemo mkewe wa kwanza kabisa Robin Givens aliyezaa naye watoto wawili, Michael Givens na William Givens Jensen.

ANARUDI ULINGONI

Baada ya kufilisika alilazimika kufanya kazi mbalimbali nje ya ngumi kwa sababu alishastaafu kuhakikisha anapata tena pesa.

Tyson amekuwa akiigiza, akialikwa kwenye matamasha mbalimbali na amekuwa akilipwa kwa kuonekana kwake, pia pesa alizopata amewekeza kwenye biashara ya uuzaji wa vilevi mbalimbali.

Pia, anatarajiwa kurejea tena ulingoni Julai mwaka huu kwenye pambano dhidi ya Jake Paul ambalo limenunuliwa na Netflix.

Mbali ya kupewa zaidi ya Dola 3 milioni kama malipo ya awali pia Tyson atalipwa pesa ya ziada kulingana na watu walivyotazama pambano hilo kwa kulipia.

Chanzo: Mwanaspoti