Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuzo ya Mwalimu Nyerere yazinduliwa, mshindi kubeba Sh10 milioni

Tuzooo Tuzo ya Mwalimu Nyerere yazinduliwa, mshindi kubeba Sh10 milioni

Mon, 12 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amesema uzinduzi wa tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu ni safari na mwanzo mpya wa kuchochea usomaji vitabu ambayo itafungua ukurasa wa soko la vitabu nchini.

Amesema Machi 9, 2022 katika mkutano wa wadau sekta hiyo mkoani Dodoma alielezwa uchapaji na usambazaji wa vitabu bado una ukakasi mkubwa, lakini changamoto hiyo itafika mwisho.

"Sasa tunafungua ukurasa mpya utakaochochoea uandishi na uchapishaji, usambazaji na usomaji wa vitabu hasa za uandishi bunifu. Lengo hii tuzo kuhakikisha soko la uchapishaji vitabu linaendelea kuwepo na kufanya kazi," amesema Profesa Mkenda.

Profesa Mkenda ameeleza hayo leo Jumatatu Septemba 12, 2022 wakati akizindua tuzo hiyo iliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuwa hatua hiyo pia itachochea uandishi na usomaji.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na wasomi wanaotoka katika vyuo vikuu mbalimbali akiwemo Profesa Penina Mlama, mtunzi na mhadhiri mwandamizi aliyejizolea sifa kemkem ndani na nje ya nchi katika masuala ya fasihi.

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda amesema hatua hiyo imetokana na mapendekezo ya wadau ambapo katika bajeti ya mwaka huu, Serikali ilitenga Sh1 bilioni kwa ajili utekelezaji wa mchakato huo utakaochochea uandishi bunifu wa vitabu.

Advertisement Mbali na hilo, Profesa Mkenda amesema kuna kazi kubwa ya kuhakikisha tuzo bora inatolewa akisema mara 100 isitolewe endapo kazi zitakazowasilishwa hazitakidhi ubora unaohitajika.

Hata hivyo, ana imani na kamati inayosimamia mchakato huo inayoongozwa Profesa Mlama.

"Uandishi uwe wenye sanaa ya kina sio kulipua, tunahitaji kazi zenye kukuza utamuduni na maslahi kwa Taifa letu sio mapambio au mabezo. Isiwe kazi za mapambio wala mabezo, lakini sina mashaka timu inayosimamia ipo makini.

Profesa Mkenda amesema kazi itakayoshinda itachapishwa na Serikali na kuinunua na kuisambaza katika maeneo mbalimbali.

Amesema mshindi wa kwanza katika tuzo hiyo atajinyakulia zawadi Sh 10 milioni wa pili Sh 7 milioni na wa watatu Sh 5milioni.

"Kwa maana hiyo mwandishi atajipatia chake, mchapishaji na msambazaji pia. Tunafufua soko la vitabu zaidi na vitapatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi," amesema Profesa Mkenda.

Profesa Mlama amesema tuzo hiyo, itakuwa pia sehemu ya kumuenzi hayati Mwalimu Nyerere aliyekuwa mwandishi enzi za uhai wake.

Pia, amesema Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi mwenye mawazo huru na kuchochea kwa kiwango kikubwa kukuza lugha ya kiswahili iwe ya Taifa na kimataifa.

"Tuzo hii mshindi atapatikana Aprili mwakani itasaidia kuwatambua washindi mahiri wa uandishi bunifu katika nyanja za riwaya na ushairi.Pia tuzo hii itakuza lugha ya kiswahili na kukuza vipaji bunifu vya waandishi nchini," amesema Profesa Mlama.

“Dirisha la mchakato huo, litafunguliwa ramsi kesho Jumanne Septemba 13 hadi  Novemba 30 mwaka 2022 tutakuwa tunapokea mishwada inayoshindaniwa. Miswada itakayowasilishwa kupitia barua pepe ya [email protected]

 “Majaji wataanza kusoma na kutafuta washindi kuanzia Disemba mwaka huu hadi Machi 2023. Utoaji wa tuzo itafanyika Aprili 13 mwakani na ikumbukwe hii tarehe ya kuzaliwa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,” amesema Profesa Mlama.

 Amefanunua kuwa kwa watakaowasilisha riwaya lazima iwe yenye urefu wa maneno kati ya 60,000 hadi 100,000. Wakati mkusanyiko wa mashairi usipungue kurasa 60.

Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk Aneth Komba amesema ameishukuru wizara hiyo kwa kubuni na kuanzisha tuzo hiyo.

Amesema uanzishwaji wa tuzo hiyo ni utelelezaji wa moja kwa moja wa ahadi mbalimbali zilizotolewa na Profesa Mkenda kwa nyakati tofauti.

Chanzo: Mwananchi