Achana na 'drama' za insta na pisi za 'tauni'. Konde Boy, gemu lote analichezea atakavyo. Uwanja unainuka kwake. Kwa macho ya wazi na ya siri yanakiri yupo kileleni na kumiliki mchezo.
Kazichanga karata vyema na wote wanafuata nyuma. Ni 'denti' aliyesoma vyema na kulielewa somo la kiki alipokuwa kwa waalimu wake kule WCB. Wapo matomaso, hawaelewi kuwa Konde ndiye mkuu wa msafara kwa sasa.
Zamani walipokezana vijiti, leo ni kiki tu. Kiki zimetunga mimba na kuzaa kitoto kiitwacho chawa. Ndani ya kiki ni chawa ndani ya chawa kuna kiki. Kiki ni tendo au tukio, chawa ni utu ama mtu. Kujitoa akili.
Na bingwa wa kiki ni Mondi. Ndiyo masta wao, sumu hii kaisambaza kwa waliopita kwake. Lakini ni wazi Mondi anahitaji akili mpya. Kuna pahala 'Big' kabaki palepale. Kulijua hili, unahitaji akili mpya pia.
Matokeo yake denti wake kageuka 'Jasiri muongoza njia wa kiki' zake. Konde Boy ni denti aliyefaulu elimu ya kiki na chawa mjini. Kila anachofanya Konde na Mondi anafuata direct or indirect. Chawa wa Konde wote aliwabeba Mondi.
Konde Boy kutoka kusimamiwa na Mondi, mpaka kuwa mshindani wake, kwake ni ushindi. Kwani haikuwahi kutokea Bongo hii, Mondi kukimbizwa kwa kiki mjini. Konde kaweza na kamtuliza.
Miaka yote Mondi alitamba kwa kiki za pisi. Leo eneo hilo lipo chini ya 'Jeshi'. Nchi nzima stori ni za Konde na madem zake, Mondi naye kageuka kuwa mfuatiliaji wa machongo ya Konde na Madem zake.
Any way hata kwenye muziki jamaa yuko vizuri. "Made For Us" hii album unahitaji kuiskiliza hata kama humpendi huyu jamaa. Utajua kuwa Konde Boy ni noma. Kuna muziki na wanamuziki na kuna Konde Boy.
DULLY SYKES: Kwa muonekano utamuona kama bishoo, mtoto wa mama na kila neno lenye maana ya kijana legelege. Utakosea.
Ni mtoto wa mjini tena siyo wa kuiga. Kazaliwa Ilala na kukulia Kariakoo. Utu uzima akiupatia mitaa ya Mnazi Mmoja. Utamwambia nini?
Wengi walitoweka kimuziki kwa tabia mbaya na kutojitunza kisanaa. Wakajali muonekano na sauti. Wakasahau moyo safi. Heshima. Na nidhamu ya kazi.
Tuliowaamini kama vichwa na siyo mabishoo au lelemama na watafutaji. Bado wanaishi kisela, Dully ni baba wa familia tangu na tangu.
Anakuonyesha kuwa muonekano na tabia kwake ni Simba na Yanga. Haviendani kamwe. Alikiba, Mr Blue, Chid Benz na wasanii wengi wenye makuzi ya Ilala na Kariakoo, wamepita katika mikono ya Dully. Kipaji ni jambo moja. Kujisimamia ni jambo lingine kubwa zaidi.
Vijana wa umri wake wengi walipoteza nguvu kazi kwa dawa za kulevya na ulevi mwingine. Unachotakiwa kujua Dully ndiye aliyeupenyeza muziki huu unaowapa pesa kina Diamond, katikati ya muziki wa kufokafoka.
Mwanzo alidhihakiwa akiitwa mwanasesere na manguli wa Hiphop. Akakomaa nao. Dully kafika hapo siyo kwa bahati mbaya. Anastahili heshima.
DIAMOND: Moja kati ya akili mbovu tuliyonayo waswahili ni kutopenda mtu awe juu kila siku. Tunataka kuona mtu anapanda na kushuka.
Furaha ya Waswahili ni kuzalisha masikini wenye majina makubwa. Wapo ambao tunakerwa kuona Mondi anazidi kupaa. Hatupendi mtu mmoja kuwa juu kila siku.
Hasira za kutopenda hilo tunahamishia katika kutafuta mtu wa kumfunika Diamond. Wabongo wamelazimisha upinzani kwa wasanii.
Daraja la Mondi hivi sasa siyo la kuimba shida za Mwananyamala au Matombo. Mondi ni mali ya dunia na muziki wa dunia siyo ujumbe tu, bali ni kelele zilizopangiliwa vizuri.
MR BLUE: Na moja kati yake sifa kuu ni kuua anapopewa shavu kwa wimbo wowote. Awe msanii mchanga au mkongwe, hakuachi salama. Na ole wake wimbo ufanyiwe video. Utajuta. Swaga, mitambao, pozi, unyama, kunyuka na mikato ya kinyamwezi. Kwake ni kama makao makuu ya chama na serikali.
Hata kama ulimpoteza kwenye mashairi, nyuma ya kamera za video lazima urushe taulo chini. Na utajuta kumfahamu.
Siyo jambo dogo. Kutoka utotoni hadi ukubwani na mashabiki waendelea kusimama kando yako. Hili jambo wengi liliwashinda. Blue kaweza na anaendelea kufanya yake kwenye muziki.
Roho yake safi anapoombwa 'kolabo', imesaidia wasanii wengi. Kuna lundo la wasanii ambao mpaka kesho wanaishi vyema kwa sababu yake.