Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tunasubiri kiki, Kenya wakimpokea Nyashinski

48153 Pic+nyashiki

Sat, 23 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unaweza usielewe kwa sababu kila siku unawasikia mitaani. Mitandaoni na sehemu kibao. Tatizo sio kusikika, wanasikika kwa lipi? Sauti na mashairi yao yametelekezwa. Hata viuno vyao majukwaani siyo dili tena mjini. Wanasikika kwa mengine kama uhusiano wa mapenzi, ugomvi wa familia na wingi wa pesa badala ya muziki wao.

Diamond anazalisha habari zaidi kuliko nyimbo, wasanii wapya, video wala audio. Mashabiki wamejengwa kwenye njia ya matamanio ya kusikia habari za familia na matukio binafsi kuliko ujio wa kazi zake. Siyo kwamba hatoi kazi, bali habari za maisha binafsi zina nguvu kuliko uzito wa nyimbo mpya. Hili kalitengeneza yeye binafsi.

Hawajabadilika sauti wala ubora wa nyimbo zao. Na pengine hivi sasa wamekuwa bora zaidi kuliko awali. Lakini ukweli ni kwamba mashabiki kama wamekinai na nyimbo zao sasa wanavutiwa zaidi na ubuyu. Umbea juu ya familia za mastaa unakimbiza zaidi ya singo zao. Ndo maana Pierre anakuwa maarufu kwa sababu ya ulevi tu.

Watu kama wamechoka hivi. Mwanzo watu walifuatilia WCB wanatoa ngoma gani. Lakini leo wanauliza Pierre wa Liquid kapata tangazo tena? Ina maana watu wameamua kufuatilia vitu vyepesi kama wepesi wa nyimbo za wasanii wetu. Nyimbo nyingi zimekuwa nyepesi huku nyingi zikiwa

hazina ufundi mkubwa. Fuatilia utagundua.

Wanamuziki wenyewe wanaendeshwa na umbea. Hawaumizi tena vichwa vyao, wanachofanya ni kupita kwenye maeneo yale yale ya umbea. Matokeo yake Hamisa Mobetto anatajwa hata mara tatu katika kila wimbo mpya ndani ya mwezi mmoja. Kwa sababu wanafuata mashabiki wanachotaka. Ubuyu.

Muziki unapotezwa na kiki nyingi za wasanii. Kenya kina Nyashinski wameanza kurudi juu kwa kasi kwenye soko la muziki. Wasanii wetu wengi hapa Bongo, wamekuwa wakitumia kiki kwa ajili ya kutangaza kazi zao. Hili ni jambo baya sana ambalo linaua muziki taratibu. Kiki zenyewe ni zile zile ambazo zinachosha masikioni.

Muziki upo mahala pazuri lakini kiki zinaushusha. Na Wakenya wanarudi maana wao walikuwa juu kabla sisi hatujawaondoa. Punde naona watachukua nafasi yao kwa sababu ya sisi kuendekeza upuuzi. Mbosso anaweza kuwa na wimbo mkali lakini kwa kuwa Diamond ana kiki zile zinazobamba atasikika yeye zaidi. Kipaji cha Mbosso kinauawa kwa kukosa kiki za kizinzi.

Na zaidi hatuwezi kijivunia mafanikio ya msanii mmoja. Miaka kumi sasa akiwa staa pekee mkubwa kimataifa toka kwetu. Kuna daraja kubwa sana kati ya Diamond na wengine kwa mafanikio, umaarufu na kila kitu. Anaanza yeye namba moja mpaka nafasi ya tatu ndo unaanza na wengine. Hatuwezi kujivunia lundo la wasindikizaji wa mafanikio ya Diamond peke yake miaka yote.

Wakati hapo Kenya Nyashinski akiwa amerudi kwa kasi. Huku akidondosha ngoma kali tupu, huku kwetu Fid Q anatoweka. Fid wa miaka mitatu nyuma siyo huyu wa sasa. Siyo kwa kutoa singo nyingi hapana hata majukwaa yanammiss. Nani aandae tamasha la muziki kubwa wakati hana uhakika na biashara ya muziki wetu?

Kila kitu kimehamia mitandaoni hivi sasa. Wanamuziki wanatoa nyimbo zenye kuvutia watu wa YouTube. Nyimbo nyepesi zenye maneno yanayojirudia ambayo ‘yametrend’ mitaani na mitandaoni. Na Wabongo kwa sasa kuna kitu tunakikosa au tuna msongo vichwani kiasi cha kishindwa kutofautisha burudani na utani. Utani utani umetuteka zaidi kwenye maisha halisi.

Na mitandao yetu haitumiki kutangaza kazi za wasanii wetu. Kila kitu ni Ushilawadu kwa kwenda mbele. Naanzaje kuongelea kazi mpya ya Fid na Mchizi Mox, wakati watu wanaonifuatilia mitandaoni wanataka kusikia habari za Abdul (Baba yake Diamond)? Dunia imeamua kutupeleka karibu zaidi na kifo kuliko maisha.

Ndiyo maana Alikiba anatoa nyimbo tatu ndani ya mwaka mmoja. Na zote zinaisha utamu wake bila kujua mtayarishaji wake. WCB wanatoa nyimbo tano kwa wakati mmoja zinaisha bila kukariri hata mstari mmoja. Maisha yanaenda kasi na hata vitu vyake na maisha yetu yanatoweka kwa kasi.

Msanii kutoka na fulani kimapenzi siyo kung’aa kisanii. Muziki unaofanya ndo kiki yako. Kutengemea kiki kwa ina maana uwezo wako ni mdogo. Kiki zijitokeza zenyewe kwa sababu katika yale matukio yako. Linajitokeza jambo linavuja nakuwa kiki lakini siyo kulazimisha kwa kutengeneza.

Darasa, Billnas na wengineo wametoa nyimbo karibuni na zimetambulishwa. Lakini hazijapata mapokezi mazuri kwa mashabiki. Asilimia kubwa ya mashabiki kuzoeshwa kiki kabla ya kutoa wimbo mpya. Ndo madhara ya kiki kutumika ‘in negative way’ na mara nyingi wanaoumia ni wasanii ambao hawawezi kuishi kwa kiki.

Alikiba huwezi kumuona akitoa wimbo kwa kiki. Anapojisikia au kwa mipango na uongozi wake. Lakini mashabiki wake ni wale wanaotumia uwepo wa Alikiba kama fimbo kwa Diamond. King Kiba akitoa wimbo wanasubiri WCB na Diamond walikoroge waanze mashambulizi.

Sasa inapotokea WCB wako kimya basi mashabiki wa Kiba nao hukaa kimya mpaka wimbo unatoweka kwenye masikio yao. Hili WCB waliliona kwenye Seduce Me alipotoa Kiba na wao kupandikiza wimbo wao. Wakaamsha waliolala na kumfanya Kiba akimbize mwizi kiulaini. Kifupi Kiba anabebwa na hasira za mashabiki wake kwa WCB.

Kitu kinachoua muziki ni kiki, lakini ndo tulipo huko. Ni tatizo sio kwetu tu hata Ulaya. Kiki huwapa pesa nyingi wasanii za ghafla. Lakini mwisho hupotea kisanii. Ni kama kunywa dawa ya kupunguza maumivu kwa mgonjwa kansa. Atapata nafuu nguvu ya dawa ikiisha maumivu huendelea kama kawaida.

Kwa wasanii wa kike mpaka akae nusu utupu ili iwe kiki ya kutoa ngoma mpya. Ukiona msanii wa kike anatupia picha zenye utatanishi na mikao ya ajabu ajabu ujue anadangia wimbo mpya. Iko wazi kwamba kama staa mkubwa yuko bize mitandaoni anafanya fujo, ujue anataka kutoa ngoma.

Hata Jide kumtakia heri Gardner G Habash, katika siku yake ya kuzaliwa imekuwa nongwa. Waswahili kwa kuwa wamezoeshwa kiki za kina Diamond, wanaamini kuwa hata Jide ni kiki ya mtoko wa ngoma mpya. Yawezekana ikawa kweli ‘Dada la dada’ kaamua kwenda sawa na wakati uliopo. Afanyeje sasa kama dunoa yetu inataka hivyo?

Tofauti na wengi kudhani muziki unakua. Kwa tambo za kina Diamond na wenzao wachache. Ukweli ni kwamba muziki unapoteza nuru yake kibiashara. Shoo nyingi zimetoweka na kibaya zaidi hata tuzo hamna. Ni kazi bure kufanya muziki miaka mingi bila uwepo wa kitu cha kuthaminisha kazi za msanii. Tuzo muhimu sana.



Chanzo: mwananchi.co.tz