Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuna safari ndefu udhibiti maudhui ya filamu, muziki

Sat, 23 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni kazi ngumu kumwambia msanii kuwa video yake haifai kuonyeshwa kwa kuwa ina maudhui yasiyoendana na mila na desturi za Kitanzania. Kila mmoja anajitetea kuwa hayo yamepitwa na wakati kwamba ili video au sinema ipendeze ni lazima iwe na wanawake wanaonyesha asilimia 95 ya miili yao.

Nakumbuka niliwahi kuhudhuria uzinduzi wa filamu moja pale Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Ilikuwa filamu nzuri iliyojaa ucheshi kiasi cha kuufanya ukumbi ule kuzizima kwa vicheko vya kila namna.

Lakini ghafla ni kama kila aliyekuwapo alipigwa ganzi baada ya kuonekana vipande vya wasanii wakiwa chumbani. Miguno ya kimahaba na vitendo katika filamu ile vilimfanya kila aliyekuwamo ndani ya ukumbi ule ajikute kashikwa na ganzi fulani hivi.

Bahati nzuri nilikaa karibu na mwigizaji wa kipande hicho, nilipomtazama naye nilimwona hana raha kama watazamaji wengine. Alishikwa na fadhaa. Hakika hakikuwa kipande kinachovutia kutazama. Sijui labda kingefaa kutazama ukiwa peke yako.

Kipande hicho ni sehemu tu ya uwakilishi wa filamu zetu na video za muziki. Sijawahi kuelewa ni kwa nini wasanii wanarekodi vipande hivyo vya mambo ya chumbani. Unapoona watu wazima wawili wanaingia chumbani, wakafunga mlango au labda kuzima taa, inatosha kujua kitakachoendelea.

Nakumbuka zamani tukitazama filamu za nje hasa Marekani na Ulaya lazima mkubwa wetu akae na rimoti tayari kusogeza mbele filamu pale kinapofika kipande cha watu wazima. Siyo utamaduni wetu, siyo mambo yetu na haifai kujilazimisha. Yanafadhaisha. Ukija kwenye nyimbo za wasanii ndio utachoka. Asilimia kubwa ya video zinazoonyeshwa sasa zinahusisha wanawake wakitikisa makalio au kuonyesha asilimia 95 ya maungo yao. Kinachofunikwa ni sehemu tu ya mwili.



Chanzo: mwananchi.co.tz