Mashabiki wamekuwa wakiwashindani waimbaji wa Bongofleva, Alikiba toka Kings Music na Diamond Platnumz toka WCB Wasafi kutokana na wote kufanya vizuri katika kazi zao.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba wasanii hawa kuna sehemu nyingi wametofauti katika muziki wao na mambo mengine yanayoshabiana na kazi yao iliyowapatia umaarufu wao.
1. Hadi sasa Diamond ametoa albamu tatu ambazo ni Kamwambie (2010), Lala Salama (2012) na A Boy From Tandale (2018), huku Alikiba akitoa tatu pia, Cinderella (2007), Ali K4Real (2009) na Only One King (2021) na First of All - FOA (2022).
Utofauti hapo ni kwamba hawajawahi kutoa albamu pamoja ndani ya mwaka mmoja, pili; Diamond anatoa albamu zake kwenye mwaka unaogawanyika kwa mbili na Alikiba hajawahi kutoa albamu mwaka unaogawanyika kwa mbili.
2. Alikiba hajawahi kufungiwa wimbo wowote na Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) toka kuanza muziki, lakini Diamond nyimbo zake mbili, Hallelujah na Waka zimefungiwa kutokana na kukiuka maadili.
Kwa muktadha huo, Alikiba anaonekana kuwa mwenye kuzingatia maadili zaidi katika muziki wake kuliko Diamond na ndio sababu kwanini hadi sasa hakuna video au wimbo wake uliopigwa marufu za mamlaka yoyote katika nchi.
3. Kabla ya kumiliki lebo yake (Kings Music), Alikiba alikuwa ni miongoni mwa wamiliki wa lebo ya Rockstar400 akiwa na wenzake, Seven Mosha na Jandre Louw, jambo ambalo ni tofauti kwa Diamond anayemiliki WCB Wasafi pekee.
4. Diamond anashikilia rekodi ya kushinda tuzo saba za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) 2014 kwa usiku mmoja, na hakuna msanii mwingine Bongo amewahi kufanya kitu kama hicho.
Katika tuzo za mwaka 2015 Alikiba alikaribia kuvunja rekodi hiyo lakini akaishia kushinda tuzo tano pekee kwa usiku mmoja ikiwa ni idadi sawa na alizoshinda 20 Percent mwaka 2011.
5. Video ya wimbo wa Diamond ‘Nana’ inatajwa kugharimu Dola 40,000 sawa na Sh92.7 milioni, hakuna msanii Bongo aliyewahi kusema amefanya video zaidi ya bei hiyo, anafuatia na Alikiba ambaye video ya ngoma yake ‘Aje’ iligharimu Dola 32,000 sawa na Sh 74.2 milioni.
6. Lebo ya Diamond, WCB Wasafi inasimamia wasanii watano wakiwemo wawili wa kike, wakati Kings Music ya Alikiba ina wasanii watatu na hakuna hata mmoja wa kike.
Lakini wawili hao kila mmoja kamsaini ndugu yake katika lebo yakee, Diamond kamsaini Dada yake, Queen Darleen, huku Alikiba akimsaini mdogo wake, Abdukiba.
7. Februari 2018 Diamond alizindua Wasafi TV na Radio na kuwa msanii wa pili Afrika kumiliki vyombo vya habari baada Youssou Ndour wa Senegal ambaye anaongoza kwa utajiri pia, hii ni tofauti kwa Alikiba ambaye hajafanya hivyo.
8. Wasanii wa WCB Wasafi wana mafanikio kimuziki kuliko wa Kings Music kwa upande wa kushinda tuzo kubwa, kutoa albamu na Extended Playlist (EP).
Rayvanny ana tuzo ya BET 2017 na albamu, Sound From Africa, Zuchu ana tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2020 na EP, I Am Zuchu, Mbosso ana albamu, Definition of Love, Lava Lava ana EP, Promise. Msanii wa Kings Music mwenye EP ni mmoja tu; K2ga, Safari.
9. Ukiachana na muziki, Alikiba ana kipaji cha kucheza soka na kashacheza hadi Ligi Kuu Soka Tanzania Bara mara baada ya kusajiliwa na Coastal Union kwenye msimu wa 2018/2019, wakati Diamond hajawahi kuwa na mafanikio kwenye mchezo wowote ule.
10. Alikiba hajawahi kurekodi wimbo na mwanamke yeyoye aliyewahi kuwa naye katika mahusiano, lakini Diamond kafanya hivyo na Hamisa Mobetto na Tanasha Donna kutokea Kenya, wote hawa amejaliwa kupata na mtoto mmoja mmoja.
Hata hivyo, Alikiba amewahi kuwatumia warembo wote hao katika video zake, Tanasha akitokea kwenye video ya wimbo wake, Nagharamia, Hamisa katika video ya wimbo wake, Dodo!.