Mwimbaji nyota wa muziki toka Nigeria, Temilade Openiyi maarufu kama 'Tems' ametangaza kushindwa kutumbuiza kwenye tamasha la "Tukutane" jijini Nairobi, nchini Kenya.
Tems ambaye ni mkali wa ngoma kama Damage na Free Mind amesema kushindwa kuhudhuria tamasha hilo ni kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake.
Tems amewaambia mashabiki wa Kenya kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa hata yeye binafsi amesikitishwa na jambo hilo, anatazamia wakati mwingine kutua Kenya na kufanya onesho ambalo mashabiki wanastahili kupata.
Hata hivyo maelezo hayo ya Tems yanapishana na yale yaliyotolewa na waandaji wa tamasha la "Tukutane" (SIC) ambao wao kupitia taarifa yao waliyoitoa wameeleza kwamba, nyota huyo alishalipwa gharama zake zote siku 15 zilizopita.
Wameongeza kuwa tayari tamasha lilikuwa limepangwa kufanyika Oktoba 15, mwaka huu, lakini ghafla meneja wa Tems akawaambia Tems hatoweza kuja kwenye onesho hilo, hajisikii kuja Kenya. Waandaaji hao wameeleza walishtushwa na taarifa hiyo iliyowavunja moyo.
Aidha, wameomba radhi kwa mashabiki kufuatia kadhia hiyo na wanatazamia kupanga tarehe nyingine mpya kwa ajili ya tamasha hilo.