Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tasnia ya sanaa kama ajira rasmi yaipaisha TaSUBa

79ab89ee810fd2f790b797c03606237d Tasnia ya sanaa kama ajira rasmi yaipaisha TaSUBa

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAASISI ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imepata ongezeko kubwa la wanafunzi mwaka huu wa masomo kutokana na mwamko mkubwa walionao vijana kutumia tasnia ya sanaa kama ajira rasmi.

Mkuu wa taasisi hiyo, Dk Herbert Makoye alisema hivi karibuni alipozungumza na HabariLEO kuwa mwaka huu wamedahili wanafunzi 400 jambo linalodhihirisha kuwa tasnia hiyo sasa inalipa na chuo hicho kimeaminiwa.

Dk Makoye alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 1981 ikiwa na wanafunzi 24 pekee, hakijawahi kudahili wanafunzi wengi kama mwaka huu.

Alisema hatua hiyo pia imetokana na kuanza kwa mfumo mpya wa kupokea wahitimu wa elimu ya sekondari moja kwa moja kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na hamasa kubwa walioipata vijana kuhusu tasnia ya sanaa.

“Hivi sasa watu wamejua kuna maisha kwenye sanaa na utamaduni na elimu ni muhimu sana ili kufanikiwa malengo. Msanii mmoja wa muziki kwa mfano ana watu wengi kama wataalamu wa taa, walinzi, madereva, waandaji wa majukwaa, video, sauti, hawa wote hawawezi kufanya kazi hiyo bila elimu hata kama msanii ana uwezo kiasi gani,” alisema Dk Makoye.

Alisema ukiacha vijana, TaSUBa imezalisha zaidi ya asilimia 80 ya maofisa utamaduni waliopo kazini hivi sasa tangu kianzishwe, kimezalisha zaidi ya wahitimu 900 na wengi wao wameajiriwa serikali, sekta binafsi na kujiajiri.

Dk Makoye aliwataka wasanii na watu walio katika sekta ya utamaduni, kuhakikisha wanapata mafunzo na elimu kuhusu maeneo yao ya kazi ili kuongeza thamani ya kazi zao na kuongeza ubora wa kazi unakaowezesha kupata masoko zaidi ndani na nje ya nchi.

Alisema mwamko wa sasa kwa vijana katika elimu ya sanaa ni mkubwa na ni udhihirisho kuwa, wametambua sanaa inalipa na hasa ukiwa na elimu kwani utafanya kazi kwa ujuzi na ustadi mkubwa na kwa viwango vya kitaifa na kimataifa.

Mkuu huyo wa TaSUBa aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi kupata elimu kwani ndio ufunguo wa maisha na njia pekee ya kuwezesha kazi zao kuwa na tija na thamani zaidi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz