Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzia: Mwandishi Zungu Fedha afariki dunia kwa ajali ya gari

Zungu Fedha Ajali Zungu Fedha enzi za uhai wake

Sun, 4 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taarifa zilizotufikia hivi punde ni kuwa, mwandishi nguli wa habari, Shakoor Jongo maarufu kama ‘Zungu Fedha’ amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari usiku wa kuamkia leo, Septemba 4, 2022 katika maeneo ya Meridian, Maasai Kinondoni jijini Dar.

Akizungumzia msiba huo, Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka amesimulia namna alivyoonana na Zungu usiku mpaka msiba ulivyotokea.

"Kulikuwa na shoo ya Twanga Pepeta huko Sinza, K-Garden karibu na kwa marehemu Banza Stone, mimi sikuingia ndani sababu nilikuwa natoka kwenye harusi ya Charles Baba, nikiwa pale nikamuona Jongo akipita, nikamuita, 'wewe Zungu njoo' hakunisikia sababu ya muziki, alikuwa akipanda jukwaani kwa sababu muziki ulikuwa unapigwa.

"Baadaye mimi nikaondoka kwenda nyumbani. Nafika tu nyumbani naingia ndani ananipigia simu Kanoute mpiga solo wa Twanga, kwamba wametoka pale Twanga na Zungu, wamekuja sasa yeye Kanoute alikuwa ananunua chipsi, anaangalia anaona watu wapo katikati ya barabara.

"Kwenda kuchungulia anamuona Zungu lakini kagongwa na keshakufa papo hapo na gari imekimbia. Ndipo akaomba wakampakia kwenye gari na kumpeleka hospitali ya Mwanayamala.

Zungu ambaye amewahi kuwa mwandishi wa Global Publishers kupitia magazeti ya burudani Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi na Amani, alikuwa mdau mkubwa wa masuala ya Burudani.

Shakoor ambaye pia alikuwa shabiki kindakindaki wa Yanga, alikuwa miongoni mwa waandishi mahiri katika kuripoti matukio ya burudani hususani katika kumbi za starehe, matamasha makubwa ya wasanii wa muziki, filamu na sanaa kwa ujumla.

Taarifa zaidi kuhusu msiba huo zitakuja baadaye.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live