Mzazi mwenza wa mwanamuziki Diamond Platnumz, Tanasha Donna ameweka wazi kuwa hataki kufanya kosa la kumtenganisha mtoto wake na ndugu
zake.
Tanasha amedumu kwenye uhusiano wa kimapenzi na Diamond kwa muda wa miezi 14 na kufanikiwa kupata mtoto wa kiume aitwaye Nassib Junior.
Katika mahojiano yake na jarida la True Love la Kenya, Tanasha ambaye ni raia wa nchi hiyo ameeleza kuwa hafikirii kufanya makosa ya kumtenga Nassib na watoto wengine wa Diamond.
Kwa sasa Diamond ana jumla ya watoto wanne wakiwemo wawili Tiffa na Nillan aliozaa na mfanyabiashara mwenye asili ya Uganda, Zarina Hassan maarufu kama Zari thebosslady na Dylan aliyezaa na mwanamitindo Hamisa Mobetto.
Tanasha alisema atafurahi kuona Nassib anakuwa na ukaribu na ndugu zake hao ambao wawili wapo Afrika Kusini na mmoja Tanzania.
Pia Soma
- NDANI YA BOKSI: Ukiyaishi maisha ya King Kiba, joto la corona litapita hivi...
- ANTI BETTIE: Mwaka wa nne sasa sijaonana naye, ila bado anasisitiza nivumilie
- Usichokijua kuhusu mafuta ya nazi
Aliongeza “Sitapenda mtoto wangu akikua anichukie kwa sababu nimemtenganisha na ndugu zake hapana ana haki ya kuwa karibu na wenzie.”
“Pia nikitulia ninataka niwe karibu na mama wa ndugu zake mwanangu ili iwe rahisi kuwaunganisha, watoto hawana hatia wala wanalolijua, yaliyotokea yanatuhusu sisi wazazi kuwatenga wao au kulumbana ni kuwanyima haki zao za msingi,” alisema mkali huyo wa wimbo Gere aliomshirikisha mzazi mwenzake.
Kauli ya mrembo huyo ambaye pia ni mwanamuziki imekuja wakati ambao kuna taarifa kwamba Diamond hana ukaribu na watoto wake hasa wale wanaoishi Afrika Kusini ambao alizaa na Zari.
Mwaka jana Zari alihojiwa na chombo kimoja cha habari na kuweka wazi kuwa mwanamuziki huyo ana muda mrefu hajawasiliana na watoto wake na wala hawahudumii.
Zari alifanya mahojiano wakati Tanasha akiwa mjamzito na alipoulizwa nini anaweza kumshauri alijibu kwa kifupi kuwa ajiandae kulea mtoto wake.
Alichokisema Zari kimekuja kutokea miezi michache baada ya Tanasha kujifungua na hatimaye mwezi uliopita likafungwa pazia la uhusiano huo uliodumu kwa miezi 14.
Hata hivyo Tanasha hakuweka wazi ni namna gani atafanikisha nia yake hiyo ikiwa hadi sasa inadaiwa kuwa watoto watatu wa Diamond aliozaa na wawili na Zari na mmoja na Hamisa, hawajawahi kukutana.
Katika mahojiano hayo, Tanasha alieleza kuwa kwa takribani miezi sita mambo hayakuwa sawa katika uhusiano wake na Diamond.
“Tulijaribu kupambania penzi hili lakini inafika wakati unajiona unapambana peke yako na mwenzio ameshapoteza nia ya kuendelea na uhusiano huo, nikaona hii si sawa siwezi kuendelea kuwepo sehemu ambayo sina furaha,” alisema Tanasha bila kufafanua.