Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amesema Tamasha la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki (Jamafest) kwa mara ya kwanza litafanyika Tanzania, huku akiwataka Watanzania kukaa mkao wa kula kujitangaza kibiashara na kitamaduni
Dk Mwakyembe amesema hayo leo Jumatano Machi 20, 2019 akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu tamasha hilo.
Amesema tamasha hilo lilianzishwa mwaka 2002 likuwa na lengo la nchi za Afrika Mashariki kujitangaza kupitia sanaa na utamaduni kwa kuonyesha vivutio, shughuli za sanaa na bidhaa zinazozalishwa ili kukuza uchumi wa nchi zao.
"Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa tamasha hili, Tanzania tumetapa bahati ya kuwa wenyeji hivyo litafanyika nchini kuanzia Septemba 21 hadi 28," amesema.
Amesema tamasha hilo ni kubwa kwa maana ya wingi wa ushiriki, zaidi ya nchi sita kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki zitashiriki na wageni kutoka sehemu mbalimbali watahudhuria.
"Tamasha hili litakuwa na vionjo mbalimbali ikiwamo tukio la watu sita kutoka nchi sita kupanda mlima Kilimanjaro wakiwa na bendera za nchi zao. Pia, kutakuwa na ziara za kutembelea vivutio, mashindano ya insha, filamu na muziki wa asili," amesema.
Amesema ni la kipekee lenye fursa pekee ya kujitangaza kwa mtu mmoja mmoja lakini nchi kujitangaza na kwamba kupitia tamasha hili Tanzania utapata watalii wengi na kukuza uchumi wetu," amesema.