Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), linalotarajiwa kuanza Novemba 10, 2022 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Bagamoyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abbasi, amesema walitarajia Rais Samia awe mgeni rasmi lakini atawakilishwa na Makamu wa Rais, Dkt. Mpango.
“Uzinduzi utafanyika Novemba 10, mwaka huu na jioni yake tamasha litaanza rasmi ambapo litashirikisha vikundi vya ndani na nje ya nchi. Mgeni rasmi tunatarajia atakuwa Makamu wa Rais Dkt. Mpango ambaye atamwakilisha Rais Samia, kutakuwa na burudani za kila aina na nchi mbalimbali zimeshathibitisha ushiriki wao". Amesema Dkt.Abbasi
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Abdallah, amesema anawakaribisha wadau mbalimbali wa burudani katika tamasha hilo.
Aidha amesema tamasha la mwaka huu linatarajiwa kuwa tofauti zaidi kwani, kutakuwa na tukio la Royal Tour ambapo wadau wa sanaa watatembelea vivutio mbalimbali vya Bagamoyo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSuBa), Dkt. Herbert Makoye amesema jumla ya vikundi 27 vya Tanzania vimethibitisha kushiriki huku nane vikitoka nje ya nchi.
“Kila kitu kinakwenda vizuri kwani tumeshapata ufadhili kutoka kwa watu mbalimbali na tunaendelea kuzungumza na wadau ili watuunge mkono,” Amesema