Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tamasha la Nafasi Art Space kurindima kesho

F73cb889f74a9a23c03c647960a860ff.jpeg Tamasha la Nafasi Art Space kurindima kesho

Fri, 25 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAMASHA la muziki na sanaa la Nafasi Art Space lililositishwa kwa miezi miwili kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (covid-19) litazinduliwa kesho na kujumuisha wasanii wa kada mbalimbali.

Ubalozi wa Ufaransa ndiyo unaofadhili tamasha hilo ambalo litajulikana kama Weekend live festival series na mgeni rasmi atakuwa Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier na Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza ambalo wananchi wataingia bure kupata burudani za aina mbalimbali.

Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Maendeleo na Utamaduni ubalozi wa Ufaransa, Cécile Frobert alisema ubalozi wa Ufaransa na mtandao wa shule za kifaransa Tanzania walikuwa wakisaidia wasanii wa Tanzania kipindi cha janga la corona kwa kuandaa matukio kupitia njia ya mtandao.

“Tunafurahi kuwakutanisha watu tena katika tamasha hili la kusherehekea sanaa na utamaduni kwa kuwakutanisha wasanii wengi wenye vipaji wa Dar es Salaam,”alisema

Alisema wataonesha sanaa za wasanii maarufu pamoja na mitindo, utoaji zawadi na nyinginezo kuanzia saa nne asubuhi na kuanzia saa tisa alasiri kutakuwa na shughuli za sanaa na utamaduni kwa ajili ya wana familia.

Frobert alisema kundi maalumu kwa ajili ya kutoa burudani kwa watoto litakuwa la watoto yatima kutoka kituo cha Chakuwama ambao wataonesha michezo na shughuli nyingine za watoto, ikiwa ni pamoja na kuchora, kupaka rangi na michezo wakisaidiwa na mwalimu wa sanaa, Ernest Mtaya na Anthony Hall.

Alisema kuanzia saa 12 jioni kutakuwa na onesho la sanaa linaloitwa ‘Altered State’litakaloshirikisha wasanii kama Raza Mohamed, Masoud Kibwana, Lazaro Samwel, Aman Abeid na Valerie Amani.

Usiku kutakuwa na tamasha la muziki mubashara kwa burudani itakayotolewa na wasanii kama Shabo Makota, Bahati band, Wahapahapa, One the incredible, Tara Jazz na Leop Mkanyia na wachezaji dansi kutoka Muda School na Magu Jugglers.

Akizungumzia tamasha hilo, Mratibu wa Sanaa za Majukwaani kutoka Nafasi Art Space, Kwame Mchauru alisema tamasha hilo ni muhimu kwa utoaji elimu ya sanaa nchini kwa kila mwaka wamekuwa wakialika wasanii wa kada mbalimbali kutoa elimu kwa wasanii wachanga.

Alibainisha wahudhuriaji wanaongezeka kutokana na kuwa na vionjo vya kitanzania na kiafrika ambapo lililopoanza baada ya kuvunjwa kwa nyumba ya sanaa walihudhuria watu 150, lakini mwezi Juni kabla ya corona walifikia watu 1,200 huku tamasha la Jumamosi linatarajia kuhudhuria watu zaidi ya 500.

Chanzo: habarileo.co.tz