Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tamasha la Fiesta Dar laacha fukuto mitaani

28884 Fista+pic TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya tamasha la Fiesta lililopangwa kufanyika juzi kuota mbawa, baadhi ya wadau wa muziki na burudani wametoa maoni yao, wengi wakishangazwa na uamuzi wa Manispaa ya Kinondoni kusitisha tamasha hilo kufanyika viwanja vya Leaders Club, siku moja kabla ya tukio lenyewe.

Juzi, waandaaji wa tamasha hilo la muziki ambalo hufanyika kila mwaka, walitangaza kuwa halitafanyika ikiwa ni saa chache kabla ya kufikia kilele baada ya kuzunguka mikoa 15 kwa zaidi ya miezi miwili.

Taarifa za kuzuiwa kwa tamasha hilo zilitolewa na Manispaa ya Kinondoni ikieleza kuwa imepokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa walio karibu na eneo hilo la Leaders na hivyo kuwataka waandaaji kulihamishia tamasha hilo viwanja vya Tanganyika Packers.

Baada ya uamuzi huo wa manispaa, waandaaji wa tamasha hilo walitangaza kuwa halitafanyika tena.

Kufuatia hali hiyo, wadau na wanamuziki walitoa maoni tofauti kuhusu uamuzi huo akiwamo mwanamuziki na mchambuzi wa masuala ya burudani, John Kitime.

Akizungumza na Mwananchi, Kitime alisema maofisa utamaduni wanapaswa kukumbuka wajibu wao katika kukuza sanaa.

Alisema nguvu kubwa inatumika kukwamisha shughuli za sanaa na wakati mwingine kutumia askari katika kufanikisha hayo.

“Rejea andiko langu katika gazeti la Mwananchi la Novemba 24, nimeeleza changamoto zinazosababisha kukwama kwa shughuli za sanaa, maofisa utamaduni hawasaidii na hili unaliona katika mkwamo wa Fiesta,” alisema Kitime.

Mwanasheria Albert Msando kupitia mtandao wa Instagram aliandika, “hatuwezi na hatupaswi kuwa nchi au mkoa ambao mfanyabiashara au mwananchi hana uhakika au hajui maamuzi gani yatatolewa kuhusu maisha yake au jambo lake lolote.”

Aliongeza, “Uamuzi wa kutoa kibali wakati mtu anajua kuna wagonjwa wa moyo ni ya kipuuzi na ya kufuta kibali cha Tigo Fiesta siku moja kabla ya tukio ni ya ovyo.”

Alibainisha kuwa haiwezi kueleweka kwamba baada ya malalamiko ya wagonjwa ndio imebainika kuwa viwanja vya Leaders Club havifai kwa tamasha hilo.

“Uongozi wenye kuacha alama una sifa zifuatazo, usawa, ukweli, haki, busara na ushirikishaji,” alisema.

Wasanii waliopangwa kutumbuiza katika tamasha hilo kila mmoja katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram walichapisha barua iliyotolewa na kamati ya maandalizi ya Fiesta bila kuandika chochote akiwamo Fid Q, Whozu, Lulu Diva, Rosa Ree, G Nako, Mimi Mars na wengine.

Mwanamuziki Fid Q aliandika, “Ama kweli mkamia maji hayanywi.”

Mwanamitindo Miriam Odemba alihoji katika mtandao huo kuwa haikuwezekana kwa tamasha hilo kufanyika katika uwanja wa Taifa au kulikuwa na kitu kingine nyuma ya pazia ambacho hakifahamu.



Chanzo: mwananchi.co.tz