Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TaSUBa kutumia sanaa kuongeza ajira, kukuza uchumi

Fd23ed2af918602fe1b6853f71309e11 TaSUBa kutumia sanaa kuongeza ajira, kukuza uchumi

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAASISI ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imedhamiria kutengeneza ajira kupitia tasnia hiyo zitakazozalisha sanaa za viwango ili ziuzwe ndani na nje ya nchi na kukuza uchumi wa mtu na Pato la Taifa (GDP).

Uongozi wa taasisi hiyo umesema unafanya hivyo kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 na maagizo ya viongozi yakiwemo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa Novemba 13 mwaka jana alipozindua Bunge jijini Dodoma.

Mkuu wa TaSUBa, Dk Herbert Makoye aliyasema hayo jana wakati akizungumza na HabariLEO ofisini kwake, Bagamoyo.

Dk Makoye alisema, mtazamo wa sanaa na utamaduni uliwekwa mbali na uchumi lakini sasa taasisi hiyo imedhamiria kutengeneza ajira kupitia tasnia hiyo ili kukuza uchumi kwa vijana wa wadau husika na kuongeza Pato la Taifa.

Alisema utekelezaji wake umewekwa katika utoaji wa mafunzo likiwa ni jukumu kuu la taasisi hiyo kupitia maelekezo ya Ilani ya CCM na maagizo ya viongozi akiwemo Rais Magufuli kufundisha kozi fupi kwa njia ya kuwafuata wahitaji walipo.

Dk Makoye alisema sanaa na utamaduni ni maisha yaliobeba watu wengi hasa vijana katika kujipatia kipato, hivyo kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yake, utaongeza ajira kwa watu wengi wanaoitegemea.

Alisema tayari wanashirikiana na wadau wengine ikiwemo Bodi ya Filamu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Idara ya Ubunifu), Chuo Kikuu cha Dodoma (Idara ya Sanaa) na wengine kutoa mafunzo kuwawezesha wahusika kuingia katika soko la ajira.

Kwa mujibu wa Dk Makoye, mafunzo ya kwanza waliyatoa kwa vijana zaidi ya 100 katika Halmashauri ya Mji wa Geita kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 6 mwaka jana.

Aliwaomba watu hasa vijana kujiunga na kupitia Idara za sanaa na utamaduni katika halmashauri zao, kuandika kwao (TaSUBa) maeneo wanayohitaji mafunzo mafupi ili wawafuate walipo kuongeza tija ya kazi wanazofanya katika tasnia hiyo.

Dk Makoye aliwashukuru viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akiwamo Waziri Innocent Bashungwa, Naibu Waziri Abdallah Ulega, Katibu Mkuu Dk Hassan Abbasi na watendaji walio chini yao kwa namna wanavyojitoa kuhakikisha taasisi hiyo inazidi kuwa kituo cha taaluma Afrika Mashariki na Kati katika vyuo vya kati.

Chanzo: www.habarileo.co.tz