Majuzi mameneja wa Diamond na lebo ya muziki ya Wasafi, Babu Tale na Salam SK walikuwa wanaposti orodha ya wasanii wanaodhani wamefanya vizuri kwa mwaka 2022.
Walikuwa na orodha tofauti tofati kama vile msanii bora wa mwaka, ngoma bora ya mwaka, ngoma bora ya hip hop ya mwaka, msanii chipukizi wa mwaka na kadhalika.
Lakini katika orodha hizo mbili, kuna moja, ya Babu Tale Alikiba hakuwepo, na kwenye orodha ya Sallam, Alikiba alikuwa anashika namba saba.
Baada orodha hizo kutrend sana, aliibuka Alikiba na ujumbe mmoja mzito ambao hakutaja jina lakini tuliosoma Cuba tunaelewa alikuwa akiwalenga kina nani.
Kwenye ujumbe huo Alikiba ametokwa povu sana huku akiwakomesha na kuwapiga marufuku Wasafi kuacha kumshobokea na kutaja jina lake kwenye list zao ili mambo yaende.
Baada ya ujumbe wa Alikiba, mjadala ukaibuka wa kwamba Je, alichokifanya Alikiba kilikuwa ni sahihi? Je kulikuwa na ulazima wa Alikiba kuwajibu?
Binafsi naona lilitakiwa kuwa jambo rahisi sana, Wasafi si wanatajwa kuwa na tabia ya wanapotaka kufanya jambo lao fulani huwa wanatengeneza tukio la kuvuta umakini wa watu? Na staili wanayopenda kuitumia mara nyingi ni ya ‘kuwachokonoa’ watu wa nje ya Wasafi, aidha wapinzani wao wa moja kwa moja kwenye biashara yao ya muziki, au watu ambao kwa namna moja ama nyingine waliwahi kuwa na uhusiano na Wasafi.
Ndiyo zile unaingia Insta unakuta Diamond kaposti picha ya kitambo inayomuonyesha yeye na Wema Sepetu, halafu chini kaandika bonge moja la ujumbe wa mahaba. Anafanya hivyo ilimradi tu kumchokonoa Wema Sepetu mwenyewe, pamoja na wapambe wake.
Au zile unakuta Diamond kaandika bonge la ujumbe kuhusu alivyomsaidia Harmonize kutoka kwenye umachinga mpaka kuwa staa mkubwa halafu dogo akaondoka bila kulipa fadhila.
Jambo lingekuwa rahisi kama Alikiba asingesumbuka kuwajibu. Kutokuwepo kwenye list ya Sallam au Babu Tale kunampunguzia nini Alikiba? Na ni wazi kwamba, hata kama dunia nzima tungekubaliana kwamba Alikiba ndiye msanii Bora kuliko wote duniani kwa mwaka 2022, pengine bado Sallam na Tale wasingemuweka kwenye orodha zao kwa sababu na wao wana msanii wao ambaye ni mpinzani wa Alikiba.
Pili mtu akitaja orodha yake hamaanishi inatakiwa iwe hivyo kwa kila mtu. Anamaanisha huo ni mtazamo wake. Ni kama vile Alikiba mwenyewe anavyojiita King. Ni sawa kwa sababu huo ni mtazamo wake na mtazamo wa kila anayedhani Alikiba ni mfalme wa muziki. Lakini swali ni Je, ni kweli Alikiba ni mfalme wa muziki kwa kila mtu? Jibu ni hapana. Kwahiyo hakukuwa na sababu ya msingi ya kuwajibu Wasafi.
Ni kama vile Wasafi wameshajua njia ya kuzifanya kiki zao zibambe wakati wapinzani wao wakiwa hawana wazo la nini kinaendelea kwahiyo wanajikuta wananasa kwenye mtego tu.