'Producer' wa muziki nchini, Geof Master ambaye alikuwa anafanya kazi kwenye studio ya Tongwe Records amefariki dunia leo Januari 26, 2024 saa 4 asubuhi kwenye Hospitali ya Saratani ya Ocean Road alikokuwa anaendelea na matibabu.
Akizungumza mdogo wa marehemu Hollad Batista, amesema kifo cha kaka yake kimetokana na saratani ya kichwa.
Hollad amesema, Novemba mwaka jana Geof alianza kusumbulia na uvimbe puani na akafanyiwa upasuaji kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini baada ya wiki tatu hali yake ilibadilika, uvimbe ukazidi ndani na nje ya pua.
Anasema baada ya hali hiyo, Januari 16 walimrudisha tena Muhimbili ambako walimpa rufaa kwenda Ocean Road ambako waliambiwa ndugu yao ana saratani ndani ya kichwa.
Kwa mujibu wa Hollad, msiba wa Geof upo nyumbani kwao Tegeta jijini Dar es Salaam na mazishi yatafanyika Jumatatu jioni saa 10, katika makaburi ya Tegeta Wazo.
"Msiba upo Tegeta tunaendelea na taratibu nyingine, lakini mazishi yatakuwa siku ya Jumatatu kwenye makaburi ya Wazo."
Geof katika uhai wake alifanya kazi na wasanii mbalimbali akiwemo mwanamuziki wa Hip-Hop nchini, Roma Mkatoliki ambaye muda mfupi uliopita ameposti picha ya marehemu kwenye mtandao wa Instagram na kuandika: "Nimempoteza kaka yangu, pacha wangu, rafiki yangu producer wangu (Tongwe Records), Rest in Peace Geof Master, PUMZIKA MSUMULE."