Naibu Waziri Uchukuzi, David Kihenzile ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuweka taa zitakazotumika kuongoza ndege usiku kwenye maeneo ya kimkakati ambayo ni malango makuu ya utalii akiwekea msisitizo mikoa ya Arusha na Iringa.
Kihenzile ameyasema hayo jijini Dar es Salaam ambapo ameeleza Tanzania ni ya nchi ya pili kuwa na vivutio vingi vya utalii duniani na asilimia 80 ya watalii wanapita mikoa ya kaskazini, huku Arusha ikitumika kama lango, hivyo taa hizo ni muhimu kufungwa katika uwanja wa ndege Arusha.
"Niwaombe sana, maeneo ya kimkakati mkamilishe taa za usiku, namba moja pelekeni taa za usiku Arusha na mbili Iringa, kwasababu nchi yetu ni ya pili kwa vivutio vya utalii duniani baada ya Brazil," amesema Kihenzile
Pia ametoa agizo kushughulikiwa kwa malalamiko ya mara kwa mara kuhusu mizigo ya abiria kuchanganywa na mingine kupotea na kuleta usumbufu kwa abiria kufuatilia hmizigo yao na kuutaka uongozi wa mamlaka hiyo kuwabaini wanaosababisha changamoto hiyo na kuwachukulia hatua.
Naibu Waziri huyo ameielekeza TAA kushughulikia malalamiko ya ucheleweshwaji wa abiria katika eneo wanalopita wageni mashuhuri unaosababishwa na utaratibu wa malipo uliowekwa eneo hilo hadi kuleta foleni kutokana na mfumo wa malipo unaoelezwa kuwa sio rafiki.