Mwmbaji wa injili aliyevuma mapema mwaka 2020 na wimbo wa ‘2020’ Justina Syokau ameendeleza mfululizo wa kukiri kwake kwa wasanii na watu maarufu wa humu nchini ambao aliwahi wakosea.
Katika video ya hivi karibuni, Syokau amekiri kwamba si tu Andrew Kibe na pasta Ezekiel Odero aliowakosea bali pia aliwahi vurugana na mchekeshaji aliyegeuka kuwa mwanaharakati, Eric Omondi.
Katika video hiyo aliyofanya akilia kwa uchungu, Syokau alikiri kwamba wakati Omondi alitoka akiwashtumu vikali wasanii wa injili kwamba wamelala na hakuna msanii anayeimba muziki wa injili Kenya, Syokau alimtukana vibaya kwa hasira.
Amesema kwamba alimwambia Omondi kuwa hana haki wala mamlaka ya kuzungumzia muziki wa injili wakati yeye anavaa kama mwanamke, pia akiongezea kuwa alikuwa shoga.
“Eric Omondi wakati aliongelelea muziki wa injili, akasema wasanii wa injili tumelala, mimi nilimtusi nikasema anavaa kama mumama, kama shoga. Nisamehe Eric, wewe unajua vizuri sana ni rafiki yangu. Mimi Eric nisamehe tu nipate kazi,” alisema akilia.
Msanii huyo alisema kuwa amekuwa katika maombi na kufunga akimwambia Mungu kumkumbusha aliowakosea wote na kuwaomba msamaha.
“Eric nisamehe, wewe ni rafiki yangu, umekuwa ukipost nyimbo zangu kila ninapotoa kila mwaka,” alisema.
Msanii huyo pia aliomba msamaha kwa wasichana wanaofanya kazi katika mataifa ya Uarabuni akisema kuwa alikumbuka siku moja aliwahi fanya video akisema wanaouawa kule ni wale wa kujiuza kimwili.
“Nisamehe, nafikiri naongea sana na mdomo umeniharibia kazi, kwa hiyo naomba tu wale wote mlioko pale mnisamehe. Nafikiri nimekosea sana nisamehe mimi nimeokoka na nimekuwa nikiomba Mungu kujua ni nini kinaniathiri kama mtu,” alisisitiza kwa kulia.