Bila takwimu rasmi, lakini kwa sasa vinasikika visa vingi vya mauaji, ukatili, unyanyasaji na mengine mabaya yanayofanywa na binadamu kwa binadamu wenzao. Hebu tumia dakika yako moja kusoma kisa hiki cha kutunga, lakini naamini kinaweza kubadili kabisa huo mtazamo wako ulionao kwa sasa.
Kuna mwanamke mrembo alichoka na maisha yake ya ndoa na alitaka kumuua mumewe. Asubuhi moja alimkimbilia mama yake na kumwambia; “Mama, nimechoka na mume wangu, siwezi tena kuvumilia upuuzi wake, nataka kumuua, lakini naogopa sheria itaniwajibisha, tafadhali unaweza kunisaidia mama?”
Mama akajibu; “Ndiyo binti yangu naweza kukusaidia, lakini kuna kazi ndogo unatakiwa uifanye kabla.
Binti akauliza; “Kazi gani? Niko tayari kufanya kazi yoyote ili kumtoa tu roho mume wangu.”
Mama akasema; “Sawa, lakini itabidi utengeneze naye amani ili mtu asije akakushuku wewe umehusika na kifo chake. Utalazimika uwe msafi, ikiwezekana ujirembe mno ili uonekane kijana na wa kuvutia zaidi kwake. Unapaswa kumuhudumia vizuri na uishi naye vizuri sana na uwe na shukrani kwake.
“Unapaswa kuwa na subira, upendo na usiwe na wivu. Kuwa na masikio zaidi ya kusikiliza kuliko mdogo wa kuongea kisha ongeza heshima maradufu kwake na uwe mtiifu.
“Kisha tumia pesa zako kwake na usikasirike hata anapokataa kukupa pesa kwa chochote. Usipaze sauti yako dhidi yake, bali himiza amani na upendo ili kamwe usihisiwe wakati atakapokuwa amekufa.
“Je, unaweza kufanya yote hayo?” Binti akajibu; “Ndiyo naweza.” Mama akasema; “Chukua unga huu na kumwaga kidogo sana kwenye mlo wake wa kila siku, polepole utamuua.”
Baada ya siku 30 binti akarudi kwa mama yake na kusema kwa sauti ya huzuni mno; “Mama sina nia ya kumuua mume wangu tena. Kwa sasa nimekua nikimpenda kwa sababu amebadilika kabisa, sasa ni mume mtamu sana kuliko nilivyofikiria. Je, nifanye nini kuzuia sumu ulinipa nimuwekee isimuue? Tafadhali nisaidie mama.”
Mama akajibu; “Usijali binti yangu. Nilichokupa ni unga wa maandazi tu. Hautamuua kamwe. Wewe ndiye ulikuwa sumu ambayo ilikuwa ikimuua mumeo polepole kwa mivutano na chuki.
“Ni pale ulipoanza kumpenda, kumheshimu na kumthamini ndipo ulipomuona akibadilika na kuwa mume mzuri na mtamu. “Wanaume siyo waovu kweli, lakini ninyi wanawake ndiyo huamua majibu na hisia zao.
“Mwanamke ukiweza tu kuonesha heshima, kujitolea, upendo, kujali na kujitolea kwa mumeo, basi atakuwa 100% kwa ajili yako.”