Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sugu alivyowaunganisha wabunge, mashabiki Dodoma

26532 Pic+sugu TanzaniaWeb

Sun, 11 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. "Niliimba mbele ya Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na Spika Job Ndugai wakafurahi. Nilitumbuiza mbele ya Tundu Lissu mjini Nairobi akafurahi sana na leo (jana) naimba mbele ya mashabiki na wabunge nanyi mfurahi, " ni maneno ya mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema),  Joseph Mbilinyi 'Sugu'.

Usiku wa Sugu, ndio jina la shoo ya mwanamuziki huyo iliyofanyika jana Novemba 10,  2018 mjini hapa na kuhudhuriwa na mamia ya mashabiki, wakiwemo wabunge.

Mwaka 2010 Sugu ndio alichaguliwa kuwa mbunge akitokea katika mafanikio makubwa ya muziki wa Bongo Fleva kuanzia miaka ya 90 na tangu awe mwakilishi wa wananchi wa Mbeya bungeni amekuwa akiendelea kufanya muziki ingawa si kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, pengine majukumu ya kibunge yamembana.

Hana nyimbo mpya nyingi na katika shoo zake huimba nyimbo zake za zamani ambazo hadi sasa zikipigwa watu hunyanyuka kwenye viti na kucheza kama si kutikisa vichwa wakiwa wameketi.

Ndivyo ilivyotokea katika shoo hiyo ya jana iliyofanyika klabu 77 Dodoma. Wapo walioshindwa kujizuia na kucheza tangu Sugu alipoanza kutumbuiza hadi alipomaliza usiku huo.

Kabla ya Sugu kupanda jukwaani wanamuziki Mchizi Mox na mbunge wa Mikumi (Chadema) Joseph Haule 'Profesa J' walianza kutoa burudani na kuwapagawisha mashabiki.

Pia wapo waliokuwa wakitikisa vichwa tu huku wakirusha mikono juu na kuna wale walioonekana wazi wameshindwa kujizuia na kuanza kukumbushana maisha yao ya nyuma kupitia nyimbo alizokuwa akiimba Sugu.

Ana miaka chini ya 18 na  Sugu moto chini ni baadhi ya nyimbo alizoimba Sugu katika shoo hiyo huku mara kadhaa akiwatambulisha wabunge waliohudhuria shoo hiyo wakiwemo Anthony Mavunde (Dodoma Mjini),  William Ngeleja (Sengerema), Pascal Haonga (Mbozi), Frank Mwakajoka (Tunduma) na Wilfred  Lwakatare (Bukoba Mjini).

Mbali na kuwapongeza wabunge wenzake kwa kuhudhuria, Sugu pia aliwaeleza mashabiki kuwa wabunge ni kitu kimoja na ndio sababu hata wa vyama vingine walijitokeza katika shoo hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz