Dar es Salaam. Mchekeshaji Steve Nyerere amesema video inayotembea mtandaoni ikimuonyesha akisema mwanamuziki Ommy Dimpoz hataimba tena imekatwa katwa na kuonekana hivyo.
Amekiri kuzungumza na mtangazaji huyo isipokuwa amedai maelezo yake hayakuwekwa katika mtiririko badala yake walichukua vipande na kuviunga.
“Mimi nilisema hivi kwamba Ommy atachukua muda kurudi katika hali yake kutokana na ile hali aliyokuwa nayo tunapaswa kumwombea, kuna vitu vinabadilishwa kwenye hayo maongezi. Jiulizeni kwa nini hawaweki mahojiano hayo mpaka mwisho?” amehoji.
Amesema anaishi na maadui wengi hivyo inawezekana wamefanya hivyo ili kupata maana ambayo itamharibia jina lake.
Akizungumzia hilo, Ommy Dimpoz amesema amemsamehe mchekeshaji huyo aliyejipatia umaarufu kwa kuigiza sauti za viongozi na hana kinyongo naye isipokuwa alimuomba kuwa makini anapozungumzia mambo ya watu hasa wanapokuwa kwenye matatizo.
“Sielewi alikuwa ana maanisha nini kwa sababu Steve ana namba yangu na hata kama hana alikuwa na uwezo wa kuipata. Ajabu sijawahi kupata meseji au ujumbe wowote wa pole kutoka kwake. Tujifunze kutoyazungumzia vibaya matatizo ya watu,” amesema.