Dar es Salaam. Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limesema wasanii Steve Nyerere na Irene Uwoya hawajasajiliwa na baraza hilo kufanya shughuli za sanaa.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Julai 17, 2019 na kaimu katibu wa baraza hilo, Onesmo Kayanda baada ya kumalizika kwa kikao kati ya baraza hilo na wasanii hao.
"Tumezungumza nao mambo mbalimbali lakini katika maongezi pamoja na mambo mengine tumegundua hawakusajiliwa na baraza na tayari tumewapa maagizo wafanye hivyo mara moja," amesema Kayanda.
Kuhusu Uwoya kuwarushia fedha wanahabari katika tukio lililotokea juzi Jumatatu Julai 15, 2019, Kayanda hakutaka kuweka wazi jambo hilo.
“Tunalaani kitendo hicho kwa nguvu zote na tumekuwa tukifanya hivyo mara zote kuwaasa wasanii kufanya mambo yenye kujenga jamii badala ya kuibomoa, ”amesema.
Kwa upande wake Steve amesema “Nawaomba msamaha waandishi wa habari na Serikali kwa ujumla, kuhusu vifaa vilivyoharibika tumeanza kuzungumza na baadhi yao na tunalifanyia kazi suala hilo.”
Habari zinazohusiana na hii
- Alichofanya Uwoya chalaaniwa kila kona
- Irene Uwoya awaomba radhi waandishi wa habari, asema alitaka kuwatunza