Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

So! tuoe wacha Mungu au tubaki na wala nauli?

Ireneuwoya8 284815578 1208784399940606 6698401308714093280 N So! tuoe wacha Mungu au tubaki na wala nauli?

Mon, 17 Oct 2022 Chanzo: Mwananchi

Onyo la msingi sana. Kwenye mishe za mahaba usiache kutumia pesa. Zile stori za penzi siyo pesa waachie njiwa, paka, inzi, nyoka, ngedere na pofu wa Tarangire. Kuna washikaji wana maisha magumu kama jiwe. Lakini hawaachi kuhonga. Akili kubwa hujadili na kachanganua mawazo ya watu. Akili ya wastani hujadili na kupenda matukio ya watu. Akili ndogo huzungumzia na kujadili maisha ya watu tu. Na wapo wenye akili ndogo zaidi zisizo na akili kabisa za maisha.

Hawa ndio wale wanaoingia kwenye ndoa kwa sababu na siyo upendo. Ama kwa kuchoka kuishi na wazazi wake. Au kwa mkumbo tu wa kuiga wenzao waliooa ama kuolewa. Hata kwa sababu tu kapata bwege lake la kubeba majukumu ya mzazi wake. Wengi hawajui wajibu wao kwenye ndoa. Wanalazimisha tu. Na ujue kulazimisha mapenzi, ni alama ya kutojiamini, ujuha, kutojitambua, uwezo mdogo wa akili na ukomavu. Yes! Tunaishia kuzalisha wezi wa waume na wake za watu.

Jiulize mtoto wa kike anaishi Dar. Hasomi chuo, hauzi duka wala siyo msusi. Hafundishi chakechea, hukopeshi vijora wala kuuza duka. Siyo fundi cherehani, hauzi pombe wala mihogo barabarani. Hana mume, mchumba wala boyfriend. Lakini anakula vizuri, anavaa vizuri na wikiendi mitoko haikauki. Amepanga upande, ana simu janja ‘fulu’ bando. Kila wiki anabadili misuko na kulewa kila siku. Hatuchukii na kuumizwa na maisha yake. Atueleze tu anafanya kazi gani?

Au mnataka Serikali ianze tozo la kuishi mjini? Yaani ukiishi ‘tauni’ kibwege unapigwa na tozo flani hivi amazing. Yes! Maana kuna watu hawana lolote wanalofanya mjini, lakini wanachangia kujaza chemba za maji machafu.

Na kuna madogo wanalambalamba midomo tu mjini na wanaishi vizuri. Siyo kwa kupambana sana na mtaa, ila ni kwa kulelewa tu kibwege. Yaani kijana anawaza avae vipi, atoke vipi, atembee vipi na aongee vipi kama pisi kali. Ili tu alivutie ‘Lianti’ flani hivi limlee.

Na nyie baadhi ya kina mama, wale ‘Maanti’ wa mjini. Upuuzi wenu huo wa kupetiwa na watoto hauna nafasi tena. Mnaharibu vijana wa kiume, wanaanza kuishi kama dada zao badala ya kaka zao. Kama kijana wa kiume hana uwezo wa kusimamia shoo nzima ya maisha wa nini. Wanawake wenye akili kubwa na wa mjini kweli kweli. Pindi wakitokewa na mabishoo walamba lipsi, swali lao la msingi ni moja tu.

“Unajishughulisha na nini?” Swali hilo linalenga kuangalia kama dogo anaweza kugharamia zigo. Lakini kuna washamba washamba wa kike. Ambao hupambana sana na maisha kwenye kusaka pesa. Kama haitoshi anaanza kupambana sana, kusaka penzi la mabishoo wa mjini. Siyo tu ushamba, bali ni akili ndogo sana ndani ya mwili mkubwa wenye nguvu.

Ukiona mwanamke analea mtoto wa mtu wa kiume. Mtazame vyema! Ni dhahiri utapata picha kwamba ana nguvu nyingi kuliko akili. Hizi pigo za kulea madogo ziliondoka na Ukawa 2015. Unaleaje mtoto wa kiume kwa faraja ya faragha? Itoshe kusema wewe ni mwanamke usiye na akili timamu. Kinachokera zaidi ni kuona huyo mwanamke anayefanya upimbi huo ni mke wa mtu. Aiseee! Yaani mke wa mtu, anayepewa kila kitu na mumewe. Anatumia sehemu ya kile anachopewa kwenda kutafuna na kibishoo flani tu. Kiwe cha mtaani au kazini kwake. Na maeneo ya kazi kuna ujinga mwingi sana huko. Uliza watu!

Mke anaenda kazini akimuwaza zaidi ‘bebi’ wa ofisini kuliko hata kazi yake. Tazama hata hapo ofisini ulipo, kuna wake za watu ambao huleta mazoea ya kibwege bwege na madogo. Hii ni kama ‘prinsipo’ kwa sasa. Wanaitana ‘bebi’ wenyewe kama majuha.

Msichana asiye na ndoa hutamani sana maisha ya ndoa. Na akiolewa husahau kabisa maumivu ya kukosa ndoa na kutamani maisha ya nje ya ndoa.

Yaani kiwango cha maumivu ya kutamani ndoa kwa wasio na ndoa ni sawa na kiwango kutamani maisha ya nje ya ndoa kwa wenye ndoa. Kifupi kero ya nje ya ndoa sawa na kero ya ndani ya ndoa. Yes! Ndio maana yake.

Maisha yetu ni kama mnyoo, hayana mwelekeo maalumu. Yule wa elimu kubwa ni maskini, wa elimu ndogo ni tajiri. Kuna maskini kwa sababu ya kukosa elimu, na kuna tajiri kwa sababu ya elimu yake. Na wote hawa wana kinyume chake. Wakati wewe unawaza ufanye nini ili ufanikiwe zaidi, kuna anayetamani afikie hata nusu tu ya maisha yako.

Tamaa ya maisha ya wengine ndiyo yanayopelekea dunia kuwa sehemu hatarishi kuishi. Utatamani pesa za wenzako, magari, nyumba, vyeo na mwisho utatamani mke au mume wa mwenzako. Uzinzi ni zao kubwa la kutoka shamba la tamaa. Ukiwa na mwenzi awe mume au mke mwenye tamaa sana. Iwe tamaa ya mali au ya kimwili ni kutemana naye fasta tu. Na jinsi ya kumtema mpenzi wako kama umemchoka, kwanza lia sana, kulia huondoa maumivu yako na kuzuia kitu kama kuua. Usimpigie simu au kumtumia meseji angalau kwa wiki nne. Mgeukie rafiki au ndugu unayeweza kuwasiliana naye mara kwa mara. Kuhuzunika ni lazima, hata na yeye huko aliko pia atahuzunika tu. Mpe jina jipya, kama ni Julie ‘msevu’ ‘Kimeo’. Kama Levy ‘msevu’ ‘Sanduku la Barua’. Usiache kumsengenya kwa watu wako, hii itafanya upunguze zaidi hasira. Usimfuatilie mitaani au mitandaoni. Usitake kujua ana furaha au huzuni bila wewe.

Kama mlienda baa wote sasa nenda kanisani peke yako. Kama mlienda kanisani pamoja nenda baa kivyako. Ina maana kama wa baa kakushinda utapata wa kanisani. Na kama wa kanisani anakusumbua jaribu kusaka wa baa. Yes! Utanishukuru kesho.

Mimi binafsi ‘nadiklea interesti’ kwa kusema limbwata lipo. Aliyepigwa limbwata hufanya yale yasiyotakiwa kufanywa. Mnaposhangaa na yeye hushangaa kwa nini mnamshangaa. Ombea katika mishe zako za penzi usipigwe limbwata. Waambie wana wakiona umepigwa kitu wakushtue fasta. Ukileta ubishi wakubebelee kinguvu ukaombewe.

Kama familia inaamini nguvu za giza, basi wakupelekea kwa mtaalamu. Limbwata ni kama sindano ya nusu kaputi, hujijui. Wapo wasemao limbwata ni mambo ya kufikirika. Eti unakuwa umewekwa katika laini tamu ya penzi mtambuka. Ila mimi binafsi nasema ukweli kuwa limbwata lipo. Nimekwepa sana kwa michepukozi wakati ule nikiwa pale Bandari Tanga miaka ya 80.

Kama wewe ni kapuku lofa na mbavu za mbwa, sasa kwa lipi hasa mpaka upewe limbwata? Huna pesa, huna sura, huna nguvu za kiume. Hakuna mwanamke wa kubeba hiyo dhambi kiboya kwa lofalofa.

Limbwata lipo maalumu kwa wenye pesa, nguvu na mvuto. NASISITIZA! Mke wa mtu hapendwi kwa kuwa ni mrembo sana. Hapana! Sababu kuu mbili ni kwamba.

Mosi. Hasumbui kabisa. Pili. Hana mizinga ya ovyo ovyo. Lakini wapo baadhi yao huchepuka ili kujifariji nafsi zao. Nao wana sababu kuu mbili.

Mosi. Migogoro isiyoisha ndani ya ndoa. Pili. Kwa uhuni wake tu. Sasa sikiliza ndugu, kuna dada alikuwa na nyodo ndani ya ndoa. Kisa anatoka na bosi wake ofisini. Akijichetua na kumdharau mume. Akamwagwa mchana wa jua kali. Imefikia hatua hata mbwa akibweka anaitika “Abeee!” Heshimuni ndoa kina dada. Mke mzinifu mshahara wake talaka tu.

Chanzo: Mwananchi