Mshindi wa shindano la ulimbwende Nchini Japan (Miss Japan) ambaye ni mzaliwa wa Ukraine amejivua taji lake baada ya ripoti kufichua uhusiano wake na mwanamume aliyeoa.
Karolina Shiino mwenye umri wa miaka 26, alitawazwa kuwa ‘Miss Japan’ wiki mbili zilizopita lakini ushindi wake ulizua mjadala wa umma kutokana na asili yake.
Wakati wengine wakibariki ushindi wake kama raia halali wa nchi hiyo, wengine walisema hakuwakilisha maadili ya kitamaduni ya urembo ya Kijapani.
Wakati hayo yakijiri jarida moja la eneo hilo lilifichua kuwa mlimbwende huyo alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi mwanaume aliyeoa ambaye ni mshawishi na Daktari ingawa mwanaume huyo hajazungumza lolote kuhusiana na sakata hilo.
Katika ripoti ya awali waandaaji wa shindano hilo walimkingia kifua Bi Shiino wakidai kuwa mrembo huyo hakujua kuwa mwanamume huyo alikuwa ameoa
Hata hivyo baadaye waandaaji hao waliweka wazi kuwa Bi Shiino amekiri kufahamu kuhusu ndoa na familia ya mwanamume huyo.
“Alikuwa ameomba radhi kwa kupotosha na waandaaji walikubali kujiuzulu kwa taji lake,” Chama cha Miss Japan kilisema.
Bi Shiino pia aliwaomba radhi mashabiki wake na umma kwa ujumla katika taarifa yake siku ya Jumatatu, ambapo alisema ametenda kwa woga na hofu wakati wa kutoa majibu kuhusu ripoti hiyo.
“Ninasikitika sana kwa shida kubwa niliyosababisha na kuwasaliti wale walioniunga mkono,” alisema.
Taji la Miss Japan sasa litaendelea kuwa wazi kwa mwaka mzima, ingawa kulikuwa na washindi kadhaa.
Bi Shiino alitawazwa kuwa Miss Japan mnamo tarehe 22 Januari akiwa ni mtu wa kwanza mwenye asili ya Ulaya kupewa heshima hiyo.
Alizaliwa Ukraine kabla ya kuhamia Japan na mamake akiwa na umri wa miaka mitano na kuchukua jina la mwisho la baba yake wa kambo wa Kijapani.