Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Siri ya Magufuli na namba tano

Magu Pic Data Siri ya Magufuli na namba tano

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa Rais wa tano, John Magufuli ambaye kesho atapumzishwa kwenye nyumba ya milele nyumbani kwao Chato mkoani Geita ameondoka duniani akiwa na siri ya namba tano.

Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Yafuatayo ni baadhi ya matukio likiwemo moja la kimichezo yaliyomhusisha na namba tano inayoangukia katika siku (Jumatano), mwezi (wa tano - Mei) na mwaka.

Mgeni rasmi Simba, Kagera

Kwa mara ya kwanza, Mei 2018, akiwa Rais, Magufuli alikwenda uwanjani kushuhudia mechi ya Simba na Kagera Sugar ikiwa ni kutikia mwaliko alioupata kutoka kwa mabingwa wa Tanzania Bara (Simba).

Akiwa mgeni rasmi katika mechi hiyo aliwakabidhi Simba kombe la ubingwa wa Ligi Kuu huku akiwapa wasia wa kujituma zaidi uwanjani baada ya kufungwa bao 1-0 na Kagera Sugar, mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa (sasa Mkapa) jijini Dar es Salaam Mei 19, 2018. Kabla ya kuwakabidhi Kombe hilo, Rais Magufuli aliwaambia wachezaji wa Simba SC hajaridhishwa na kiwango chao na kuwataka waboreshe kuelekea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hivi sasa Simba inahitaji pointi moja katika mechi mbili ilizobakiza kwenye kundi A ili kufuzu robo fainali ya michuano hiyo msimu huu.

Kiapo urais

Katika awamu zote mbili za uongozi wake, Rais Magufuli aliapishwa Novemba 5. Awali ilikuwa Jumatano ya Novemba 5, 2015 alipokabidhiwa kijiti na Jakaya Kikwete.

Tukio la pili ni lile la Novemba 5, 2020 alipoapishwa kwa muhula wa pili kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 28. Katika siasa mara ya kwanza kabla ya kuwa Rais, Magufuli aliwania ubunge wa Chato na kuingia bungeni mwaka 1995.

Miaka mitano, miezi mitano

Hadi mauti inamkuta, Rais Magufuli alikuwa amedumu madarakani kwa miaka mitano na miezi mitano kasoro siku chache kutimiza miezi sita. Baada ya miaka mitano ya awali, katika muhula wa pili wa uongozi wake, Rais Magufuli alidumu madarakani kwa miezi minne na siku 17 hadi mauti ilipomkuta Machi 17, saa 12 jioni.

Itakumbuka kuwa Magufuli pia alikuwa ni Rais wa tano katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Kiongozi huyo ambaye alifariki siku ya Jumatano wiki iliyopita atakumbukwa pia kwenye michezo kwa kuialika Taifa Stars Ikulu na bondia Hassan Mwakinyo ili kuwapongeza kufuatia ushindi walioupata Machi 23 na 24, 2019.

Stars iliichapa timu ya taifa ya Uganda mabao 3-0 na kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika (Afcon). Mwaliko huo ulikuwa Machi 25 ambapo aliipongeza Stras na Mwakinyo ambaye Machi 23 alimchapa Sergio Eduardo Gonzalez wa Argentina nchini Kenya. Leo, Jumatano, mwili wa Rais Magufuli utaagwa jijini Mwanza na kupelekwa nyumbani kwao Chato ambako kesho utaagwa na keshokutwa utapumzishwa katika nyumba ya milele.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz