Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi ya safari ya maisha ya muziki ya Zahara

Zahara Msd Simulizi ya safari ya maisha ya muziki ya Zahara

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Siku zote mshumaa ukizimika huacha giza, ndicho kilichotokea kwa wadau na mashabiki wa burudani baada ya kutokea kifo cha Bulelwa Mkutukana ndilo jina lake kabla ya watu kumfahamu kama 'Zahara'.

Zahara alikuwa moja kati ya watunzi na waimbaji wazuri wa nyimbo kutoka Afrika Kusini akitumia lugha yake ya asili Kixhosa na Kiingereza katika uburudishaji. Wengi walianza kumfahamu baada ya kuingia mkataba na 'lebo' ya TSRecords, ambayo katika kuzungumzia mafaniko ya masanii huyu lazima nayo itajwe.

Baada ya kuingia mkataba na lebo hiyo Zahara aliachia albamu yake ya kwanza mwaka 2011 na kuipa jina la 'Loliwe' ambayo wengi walimfahamu kupitia kazi hiyo iliyopata mafanikio makubwa ikiwemo kuthibitishwa kuwa 'platinamu.

Baada ya miaka miwili aliachia tena albamu ya pili iliyoitwa 'Phendula' mwaka (2013), nayo ilipita katika mafanikio kama 'Loliwe' baada ya albamu hiyo kutoa nyimbo tatu bora , zikiwemo 'Phendula', 'Impilo', na 'Stay'.

Kwake ulikuwa kama utaratibu kila baada ya miaka miwili lazima awalishe wadau wa muziki kazi nzuri kutoka, mwaka 2015 alidondosha albamu iitwayo 'Country Girl' ambayo nayo iliingia kwenye 'platinamu' mara tatu.

Baada ya kuachana na 'lebo' ya TS Records mwaka 2017, alitia saini mkataba wa kufanya kazi na 'lebo' ya Warner Music kutoka nchini Marekani, nako hakulaza damu mwaka huohuo aliachia albamu ya nne, iitwayo 'Mgodi', ambayo iliandika historia ya kuuza zaidi na kuthibitishwa kuwa 'platinamu'. Ilipofika mwaka 2021 Zahara alitoa albamu yake ya tano iliyoitwa 'Nqaba Yam' nayo ilishika nafasi ya kwanza kwenye iTunes.

Kutokana mafanikio ya kazi zake za kimuziki Zahara alifanikiwa kupata Tuzo 17 za Muziki Afrika Kusini, tatu za Metro FM na moja kutoka nchini Nigeria. Wengi walimtazama msanii huyu kwa jicho la kiburudisho kikuu kwao kutokana na sauti yake tamu na tunzi zenye kubeba hisia, hakika ameacha kumbukumbu nzuri kwa mashabiki, ambayo ni kazi zake.

Zahara alizaliwa nchini Afrika Kusini na alianza kuimba katika kwaya ya shule alipokuwa na umri wa miaka sita, akiwa na umri wa miaka tisa alijiunga na kwaya ya wakubwa kwa sababu ya sauti yake.

Zahara alizaliwa mwaka 1987 na kufariki dunia Desemba 11, 2023 jijini Johannesburg akiwa anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa ini uliokuwa ukimsumbua.

Chanzo: Mwanaspoti