Siku nyingine kama ilivyo ada, tunakutana kwenye ukurasa huu kuzungumza kama si kuyajadili masuala ya mahusiano.
Yes ni mahusiano. Hatuwezi kuishi mbali na mahusiano, tumeumbwa binadamu tushirikiane. Ndio maana nimekuwa nikisema mara kwa mara, kwenye maisha yetu haya yaliyojaa vurugu za kila namna, unahitaji mwenza sahihi wa kutulia naye.
Unapokuwa na mtu sahihi basi utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuliwazwa, kutiwa moyo na kuyafanya maisha ya mahusiano yawe sehemu salama. Maisha ya mahusiano sio ugomvi, maisha ya mahusiano ni furaha na upendo.
Chagueni kuishi kwenye furaha, kwa namna yoyote ile mhakikishe mnaitanguliza furaha yenu kuliko kitu kingine chochote. Mwanaume ampe kipaumbele mwanaume wake kuliko kitu kingine, vile vile mwanaume amthamini mwanamke wake.
Kama mada inavyojieleza hapo juu, wakati wa kuishi mtu na mtu wake suala la simu siku hizi limekuwa miongoni mwa kichocheo kikubwa sana cha ugomvi kwa wapendanao. Yaani ukisikia wapendanao wamegombana, wameshutumiana kuchepuka basi simu ndio chanzo.
Mara nyingi simu hizi ndizo zinazowambua watu ambao wanaendekeza michezo ya kutotulia na mpenzi mmoja. Licha ya kuwa na mbinu nyingi za kujilinda kupitia simu hizo lakini anayefanya ujanja huo hawezi kudumu nao milele, ipo siku tu atabainika.
Yaani unaweza kuwa unamficha mwenza wako lakini kwa kuwa unaishi naye, ipo siku yako tu utajikuta umebainika. Unaweza kujiona mjanja kwamba unafanya uchafu wako nje halafu ukirudi nyumbani unajikausha lakini mwisho wa siku za mwizi ni arobaini.
Aibu itakukumba tu siku moja. Simu yaweza kupiga ghafla bila kutegemea, yawezekana pia ukatumiwa ujumbe mfupi au hata kutumiwa picha za kimahaba na mmoja wa watu wako wa nje na bahati mbaya ulikuwa umempa mke au mume wako simu labda pengine alikuwa na dharura akakuomba umpe ili aitumie.
Hapa ndugu zangu tujiulize je, kuna ulazima wa kuwekeana mipaka ya matumizi ya simu zenu? Kwamba simu yako ni yako na ya mwenzako ni yake. Yani mwanaume akiona simu ya mwanamke wake basi anaiona kama vile kituo cha polisi.
Yaani simu ya mwanamke hata iite vipi, mwanaume ni marufuku kuipoke. Mbali tu na kuipokea, hana sababu hata ya kuangalia mpigaji ni nani. Yaani hakuna hata sababu ya kumuambia mwanamke wake simu yake inaita, anakaa kimya tu.
Mbinu hii japo yaweza kuwa si tiba sana lakini imewasaidia wengi. Maana inawafanya wasijuane yale wanayoyafanya kwa siri. Kila mmoja anaishi kwa imani tu kwamba hasalitiwi na kama anasaliti yeye basi mwenzake yawezekana naye akawa anasaliti au hasaliti.
Lakini hapa tupime, kufichaficha huku japo kunasaidia msigombane lakini je hamuoni kama kwa upande mwingine kunatoa mwanya wa watu kuwa huru? Hamuoni kama ndio mnajiwekea urahisi wa kila mmoja kufanya mambo yake kwa siri halafu kujihatarishia afya zenu?
Ndugu zangu mbinu sahihi si tu ya kufichanafichana simu bali mnatakiwa kujitambua maana nyinyi ni watu wazima. Mnatakiwa kuelewa kwamba nyinyi ni wapenzi, wachumba au wanandoa na mnapaswa kuishi vipi.
Kujiheshimu ndio kutawafanya muishi bila kufuatiliana na mjiamini na simu zenu. Ukiishi kwa kujiheshimu, hata simu yako mwenzako hawezi kuwa na shaka nayo na kutaka kuchunguzachunguza.
Zaidi atakuachia yeye mwenyewe uitumie na hata wewe hutakuwa na wasiwasi naye kutokana na jinsi ambavyo amekujengea imani na kujiheshimu.