Ni siku tatu mfululizo kwa wageni na wenyeji kujumuika kuangalia na kuburudika kwa ala na sauti maridhawa za wanamuziki kutoka mataifa mbalimbali katika majukwaa la Ngome Kongwe.
Tamasha la 21 la Sauti za Busara linaanza leo visiwani Zanzibar, katika mji mkongwe wa Stone town likiwa na kauli mbiu ‘moving diversity’ kwa maana ya kila mtu kwenye jamii ana umuhimu na nafasi sawa.
Zaidi ya wasanii 200 wakiwa kwenye makundi 27 kutoka pembe zote barani Afrika wanakutana na kutumbuiza kama sehemu ya kusherekea muziki asili na wenye ladha ya nyumbani.
Tamasha hili maarufu zaidi la muziki kwa Afrika Mashariki, linakutanisha pia wasanii kutoka Nigeria, Msumbiji, Afrika Kusini, DRC, Niger, Uganda, Zimbabwe na Kenya na maeneo mengine ya Afrika.
“Litakuwa ni tamasha la aina yake na la kiwango cha juu. Kila onyesho litafanyika kwa kuambatanisha milio ya ala mbalimbali za muziki, hivyo wasanii watatoa burudani ya aina yake na ya kusisimua,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Busara, Lorenz Herrman.
Kila kona ya jiji ni sauti za busara
Si hotel bali, si migahawa na fukwe,, unapopita kwenye maeneo mengi utagundua kuwa wageni ni wengi na kila unayemgusa atakuambia nasubiri tamasha la Sauti la Busara.
Katika mitaa ya mjini Unguja, wageni mbalimbali wamefurika tayari kushuhudia muziki wa Afrika na utamaduni wa watu wa Zanzibar.
"Nimekuja Zanzibar wakati mzuri… nakumbuka wakati napanga kuja nchini Tanzania niliona kuwa tamasha hili litafanyiika na itakuwa vyema kwangu kuhudhuria kwasababu ninapenda kufahamu vyema tamaduni za kiafrika. Muziki na chakula cha Kizanzibari ni kitu nilitaka kukishuhudia pia kwani Maisha yangu yote ilikuwa ni ndoto yangu,” amesema Allen, mtalii raia wa Norway. . BBCCopyright: BBC
Biashara kwa wazawa
Kwa upande wa wenyeji wakati huu, ndio muda ambao biashara zote hufanyika kwa faida kutokana na kuongezeka kwa watu na wageni kutoka mataifa mbalimbali
“Nina Zaidi ya miaka 10 nimekuwa nikiona tamasha hili likifanyika hapa Zanzibar. Ukweli ni kwamba muda huu ni wetu wa kupata riziki. Mimi na wenzangu tunaotoa huduma za usafiri hunifaika na tamasha hili lakini pia huwa tunapeleka wageni kwenye maduka ambapo hununua vitu mbalimbali,”anasema Awadhi Mohamed, Dereva wa taxi katika eneo la Darajani.
Maandalizi katika ubora
BBC imeshuhudia majukwaa matatu yatakayotumika katika tamasha hilo, mawili yakiwa ndani ya eneo la Ngome Kongwe na moja katika bustani za Forodhani.
Majukwaa hayo yamenakshiwa na picha mbali mbali huku mziki utakaopigwa ukitarajiwa kupigwa kuanzia majira ya jioni saa za Afrika Mashariki.
Sambamba na maonesho hayo pia waandaji wameandaa maandamano ya kilometa mbili kutoka Mnara wa Kisonge hadi eneo maarufu la Forodhani.
''Licha kuwa tuna tamaduni, dini na siasa mbalimbali. Tunaamini Afrika na dunia ni moja na tuko tayari kuiona sote tunakuwa wamoja,” anasema Mkurugenzi wa Tamasha, Journey Ramadhan.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004 tamasha hili limewaleta pamoja watu kutoka mataifa mbalimbali kote ulimwenguni na kuchocheea ukuaji wa kiuchumi visiwani Zanzibar na kuchochea kukua kwa shughuli za kitamaduni.
Kwa miaka mingi tamasha hili limekuwa likikoselewa kwa kuchochea umomonyoko wa maadali hususani masuala ya mapenzi ya jinsia moja.