Ni siku 15 zenye kila aina ya hekaheka zinazoanza leo mkoani Kilimanjaro, huwa zinabatizwa jina la ‘siku za kula na kunywa.’ Mji wa Moshi na maeneo ya Uchagani ndiyo huanza rasmi kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Ni siku ambazo mzunguko wa fedha huongezeka, pole pole foleni za magari huanza kujitokeza katika barabara Kuu ya Dar es Salaam-Arusha na katikati ya mji na wateja huongezeka katika masoko, baa, nyumba za starehe na maduka makubwa (Supermarkets).
Mbali na sherehe hizo, lakini kila Desemba huwa kunakuwa na sherehe za vipaimara kwa watoto, hususan waamini wa dhehebu la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Komunyo ya kwanza na Kipaimara kwa watoto waamini wa Kanisa Katoliki.
Sherehe hizo huongeza shamra shamra mitaani kwa kuwa karibu kila nyumba yenye ubarikio huambatana na kula na kunywa na familia zenye uwezo mkubwa wa kifedha, hufanya sherehe za watoto wao katika kumbi kubwa zikiambatana na muziki mnene.
“Yaani Desemba ni mwezi wa kula na kunywa. Kama Jumapili mbili mfululizo sasa ni mwendo wa Kipaimara kwa KKKT. Kila nyumba yenye ubarikio ni mnuso tu. Kama hupati mwaliko nenda baharini kaoge maji ya chumvi,” anasema Aneth Kelvin, mkazi wa Moshi Mjini alipozungumza na gazeti hili kuhusu sherehe hizo.
“Bro (kaka) nakuambia kama hii kitu (Kipaimara na Komunyo) inakupita jitafakari sana mahusiano yako na jamii. Sherehe zilivyo nyingi hivi unapitwaje na pilau mtu wangu? Labda kama una damu ya kunguni,” alisema kwa utani Aneth.
Siku hizo 15 hadi kufikia Januari 5 baada ya Mwaka Mpya, ni kipindi ambacho mji wa Moshi na maeneo ya Uchagani hushuhudia wingi wa magari ya kifahari kutokana na ujio wa wenyeji wa mkoa huo wanaoishi ndani na nje ya nchi.
Hivyo, kutokana na hekaheka zinazojitokeza katika siku hizo 15 kabla ya Krismasi na siku tano baada ya mwaka mpya, wenyeji wa mkoa huo wana utani wao ambao husema ni siku ambazo mtu anaondoka asubuhi kwenda kununua mkate, anarudi amelewa.
“Hao wanaokuja si unajua wengine wanakuja na masifa? Hapo pombe zinakuwa nje nje. Ni wewe tu. Mwaka mzima hayupo nyumbani, kwa hiyo anataka kuwaonyesha yeye ni mwamba. Kiukweli ni kipindi cha kula bata,” alisema Aneth Kelvin.
Mkazi mwingine, Renalda Evance ambaye ni mjasiriamali na mkazi wa Kiborlon, alisema Desemba Wachaga wengi waishio nje ya Kilimanjaro wana utamaduni wa kurejea nyumbani kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka na hii hata kwa wapare.
“Na kwa sababu hiyo kila mtu akiwa katika utafutaji wake hujiandaa kwa tarehe hizi, kwa sababu anafahamu kuwa lazima afanye matumizi. Watu wanakula na kunywa kwa furaha ya kuonana tena wakiwa wazima baada ya mwaka mzima,” alisema Renalda.
Alisema muda huo wawapo vijijini, huutumia kufanya vikao na kuangalia familia, kama kuna mtu ameyumba kiuchumi, au ametengana na mke au hafanyi mawasiliano na ndugu, basi hutumika kumrekebisha kitabia.
Basil Lema, mwenyeji wa Machame Wilaya ya Hai, alisema hutamani kuwepo nyumbani ili washerehekee sikukuu za mwisho wa mwaka wakiwa na familia kwa maana ya wazazi, ndugu, jamaa na marafiki.
Usalama ulivyoimarishwa
Kutokana na kumbukumbu zilizokuwa zikijirudia miaka ya nyuma inapofikia nyakati kama hizi, uhalifu nao huongezeka, safari hii hali ni tofauti kwa sababu Jeshi la Polisi limeimarisha doria na kudhibiti vitendo vyote vinavyoashiria uhalifu.
“Kwa kweli mwaka huu nawapa tano polisi wetu. Yaani hali ni shwari, nafikiri hata ile doria na misako iliyofanyika miezi miwili iliyopita imesaidia sana. Nampongeza RPC (Kamanda), RCO (Mkuu wa Upelelezi) na vijana wao,” alisema Hilda Alfonce.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema katika kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka 2023 na kuukaribisha Mwaka Mpya, wamejipanga kuendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
“Tutaimarisha ulinzi sehemu za ibada, mikusanyiko ya watu na kumbi za starehe na kuimarisha doria. Hii ni sambamba na kudhibiti makosa ya usalama barabarani na ajali kwa sababu nyingi husababishwa na makosa ya kibinadamu,” alisema.
Kamanda Maigwa aliyataja makosa ya kibinadamu kama mwendokasi, ulevi, kupakia mizigo kupita uwezo wa chombo, kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari na kutofuata alama za barabarani. Madereva tunawaomba watii sheria bila shuruti,” alisisitiza.
Wafanyabiashara wanena
Mmiliki wa klabu maarufu ya Peters Club, Peter Kinabo alisema kinachofanya siku hizo 15 ziwe hivyo hapa mkoani Kilimanjaro hasa Uchagani ni ile hali ya kupata wageni wengi kutoka mikoa mbalimbali ambao wengi ni wenyeji wanaorejea kula sikukuu nyumbani.
“Kibiashara kwa kweli huwa kunatokea mabadiliko makubwa ukifananisha na miezi mingine kabla ya Desemba, ingawa sio kwa wafanyabiashara wote. Mabadiliko kwa asilimia kubwa hutokea na hii husababishwa na ukwasi wa kifedha,” alisema Kinabo na kuongeza;
“Hawa wenzetu huja na ukwasi maana huwa wamejiandaa kwa takribani miezi yote 11, ikiwa kwa kufanya kazi au wengine hata kwa kukopa ili mradi tu shamrashamra za Desemba zisimtupe mkono. Mzunguko wa fedha unaongezeka, sana.”
Mkurugenzi wa Klabu ya Hugos Garden, Bosco Simba alisema kuna historia ya sherehe za Wachaga, lumbo au lumbo kisare zilizokuwa zikifanyika mwisho wa mwaka miaka hiyo, bado zinaendeleza desturi ya Wachaga mikoa yote kukutana Desemba Uchagani.
“Hili suala limeshakuwa endelevu na endapo Mchaga hatasafiri kuja nyumbani mwezi huu, hujadiliwa kwenye vikao na hata kutengwa na jamii yake. Wingi wa Wachaga kuja ni dhahiri inachangamsha mji wa Moshi kiuchumi na kiburudani,” alisema Simba.