Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siasa zilivyopenyezwa tamasha la Diamond Kigoma

90550 Diamond Siasa zilivyopenyezwa tamasha la Diamond Kigoma

Thu, 2 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Tamasha la kutimiza miaka kumi ya kuwa kwenye muziki kwa msanii Diamond Platnumz limejikuta likigeuka kuwa uwanja wa siasa huku msanii huyo akimtabiria Rais John Magufuli kushinda kwa asilimia 100 katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo Jumatano Januari 1, 2020 katika uwanja wa Lake Tanganyika ambapo shoo hiyo ilikuwa ikifanyika ikiwa ni kuadhimisha miaka 10 tangu Diamond alipoanza shughuli hiyo ya muziki.

Hili lilijitokeza baada ya viongozi watatu kupanda jukwaani kwa nyakati tofauti ambapo katika salamu zao walizungumzia mambo ambayo yamefanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM) tangu Rais John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho aingie madarakani Novemba 5, 2015.

Kiongozi  wa kwanza alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alitumwa na Rais Magufuli kumwakilisha katika tamasha hilo.

Japokuwa katika ratiba za tamasha hilo zilizotolewa awali hakuwapo lakini ilipofika saa 5 usiku alionekana uwanjani  hapo akiwa amevaa fulani nyeusi yenye nembo ya CCM na suruali nyeusi ambapo alikwenda kukaa walipokuwa wamekaa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga na Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa.

Katika salamu zake alisema, “Rais John Magufuli chuma cha pua  anawasalimu sana na anasema Diamond anafanya kazi nzuri kwani anaiwakilisha Kigoma, anaiwakilisha Tanzania na anaiwakilisha Afrika katika sura ya dunia makofi kwa Diamond.”

“Rais anasema Kigoma ipo moyoni mwake anaachilia fursa, makofi kwa Magufuli.”

Polepole aliongeza Diamond ameonyesha kwamba muziki ni maisha, muziki ni kazi ya heshima na staha na tunamtakia heri ya miaka kumi na miaka kumi mingine.

Naye Diamond wakati alipopigiwa simu na Rais Magufuli ikiwa ni saa 7 usiku kupitia simu ya Polepole,  aliwaambia Kigoma wana bahati sana kwani watapata wapi Rais ambaye anawapigia siku wakiwa kwenye shoo usiku.

Katika maongezi hayo yaliyochukua takribani dakika kumi, Diamond alimwambia Rais Magufuli kwamba watu wanampenda sana na ana uhakika 2020 atapita kwa kishindo.

“Baba watu tunakupenda sana na tunakuhakikishia awamu inayokuja unapita kwa kishindo sana, tunapiga mia kwa mia, Magufuli oyeeee! CCM oyeee!.

Kwa upande wake, Maganga ambaye alimshukuru Rais Magufuli kwa kuifungua Kigoma.

:Rais wetu tunakushukuru, tunakupenda  kwani tulipoanza 2015 mkoa wa Kigoma ulikuwa wa mwisho kiuchumi sasa hivi tumepanda mikoa minne juu na tuendelee tushirikiane tupande zaidi tuwe na uchumi jumuishi,” alisema Maganga

Naye Kadogosa alisema treni ya umeme ambayo miundombinu yake inatengenezwa kwa sasa pindi itakapoanza kufanya kazi itakuwa ikisafiri saa nane kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, “hii ndio kazi ya CCM, hii ndio kazi ya John Pombe Magufuli.”

Kama haitoshi Diamond wakati alipompandisha jukwaani meneja wake, Babu Tale kumpongeza katika siku yake ya kuzaliwa, alisema watu wamekuwa wakimtaka (Diamond) agombee ubunge lakini hilo haliwezi na badala yake alimuomba Tale kama ataweza kugombea mkoani Morogoro afanye hivyo na yeye atamsaidia katika hatua zote.

Chanzo: mwananchi.co.tz