Serikali ya Rwanda imesitisha shindano la urembo la Miss Rwanda kufuatia kukamatwa kwa mwandalizi wake mwezi uliopita.
Hatua hiyo imekuja baada ya uchunguzi wa unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya Dieudonné Ishimwe, mtendaji mkuu wa Rwanda Inspiration Backup, ambayo huandaa shindano hilo.
Ishimwe alikamatwa mwezi uliopita kwa madai ya unyanyasaji wa kingono kwa washindani. Hajajibu tuhuma hizo.
"Wizara ya Vijana na Utamaduni inafahamisha umma kwa ujumla kwamba shindano la urembo la Miss Rwanda limesimamishwa hadi uchunguzi ukamilike," wizara ya utamaduni ya Rwanda ilisema katika taarifa yake siku ya Jumatatu.